Vyama 14 vya siasa vyasema vimeridhishwa na matokeo ya uchaguzi

By Imani Nathaniel , Nipashe
Published at 04:29 PM Nov 28 2024
Mwenyekiti wa Tanzania Labour Party ( TLP) Wilaya ya Kinondoni, Bakari Makame.
Picha: Imani Nathaniel
Mwenyekiti wa Tanzania Labour Party ( TLP) Wilaya ya Kinondoni, Bakari Makame.

VYAMA 14 vya siasa vimesema Uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliofanyika jana ulikuwa huru na haki.

Aidha vyama hivyo vimeipongeza serikali chini ya Rais Dk.Samia Suluhu Hassan, kwa maandalizi mazuri tangu mwanzo wa kupata wagombea, kampeni na upigaji kura.

Vyama hivyo vimetoa tamko hilo mapema leo  Dar es Salaam, vilipokuwa vikitoa tathimini ya uchaguzi uliofanyika Novemba 27 mwaka huu.

Mwenyekiti wa Tanzania Labour Party ( TLP) Wilaya ya Kinondoni, Bakari Makame, amesema vyama hivyo vimeridhishwa na mwenendo mzima wa uchaguzi huo na matokeo yaliyotangazwa.

“Uchaguzi uliofanyika ulikuwa wa amani, huru na kulikiwa hakuna vurugu. Kwa upande wa Wilaya ya Kinondoni uchaguzi ulikuwa mfano kwa wilaya zote,” amesema Makame.

Kwa upende wa Katibu wa Chama cha African Democratic Alliance (ADA- TADEA) Wilaya ya Kinondoni,Ziada Athuman,amesema ingawa vyama hivyo vingi vilisimamisha wagombea katia mitaa, vijiji na viyongoji licha ya kuto kushinda lakini kushindwa huko hakutokani na kasoro za uchaguzi.

1


“Mwenyekiti wa ADA TADEA taifa Juma Ally Khatibu alitembelea vituo vyote vya uchaguzi na kuridhishwa na hali ya usalama, amani na utulivu,” amesema.

Katibu wa Chama cha Makini Mkoa wa Dar es Salaam, Issah Omary, amesema demokrasia ilitawala katika uchaguzi huo na vyama vimeridhishwa na matokeo.  

Amempongeza Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa ( TAMISEMI) Mohammed Mchengerwa, kwa maandalizi mazuri ya uchaguzi yaliyo toa fursa ya wananchi na vyama kushiriki katika uchaguzi huo.

Kaimu Mwenyekiti wa Chama cha Kijamii ( CCK) Emmy Mwakidole, amesema ufanisi wa uchaguzi huo kuwa huru ulichagizwa na maandalizi ya vifaa na usimamizi.

“ Maandalizi yalikuwa mazuri. Vifaa vyote vilikuwa katika vituo vya kupigia kura na ulinzi ulikuwa mzuri. Tunaoongeza na tunawapongeza walioshinda,” ameeleza.

Vyama vingine vilivyo shiriki tamko hilo ni NRA na NLD.