MWANAMITINDO wa Kimataifa Happiness Magese ametangazwa kuwa Jaji Mkuu wa Tamasha la Ubunifu la 'Samia Fashion Festival' litakalofanyika kesho kutwa Novemba 30,2024 Visiwani Zanzibar.
Akizungumza na waandishi leo baada ya kutangazwa kuwa Jaji Mkuu wa Tamasha hilo , Magese amesema kuwa ni heshima kubwa na furaha kwake kusimama kama Jaji Mkuu wa Samia wa Fashion Festival 2024 na anajivunia kushuhudia wakati huu wa kihistoria ambao unasherehekea ubunifu, stara, na urithi wa kipekee wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan.
Amesema yeye na wengine walioteuliwa kuwa majaji wanaamini tukio hilo ni kubwa na litakalobakia katika kumbukumbu zao kwa miaka mingi ijayo kutokana na kuteuliwa kwao kuwa majaji wa Samia Fashion Festival.
“Kwa zaidi ya miaka ishirini, nimejitolea maisha yangu katika sekta ya mitindo, urembo, nimezunguka duniani nikifanya kazi na chapa kubwa na maarufu, nimeona jinsi mitindo inavyothaminiwa katika nchi za Ulaya na mataifa mengine, si tu kama sanaa bali kama alama ya utambulisho, urithi, na fahari.
“Niliposikia kuhusu mpango huu wa kipekee, sikusita, nilichukua ndege haraka kuja nyumbani kuwa sehemu ya safari hii ya kihistoria kwa tamasha hili si tu kuhusu mavazi, ni kuhusu heshima yetu kama Watanzania,”amesema.
Mwanamitindo huyo ambaye anaishi nchini Marekani kwa sasa amesema uandaaji wa Vazi la Samia alama ya stara, uongozi, na heshima ni zaidi ya mavazi ya kawaida.
Ni kazi ya sanaa inayostahili kuhifadhiwa katika makumbusho kwa vizazi vijavyo, kama heshima kwa urithi wa kiongozi huyo.Ameeleza ilikuwa ni ndoto yake ya siku nyingi kuona Vazi la Samia linakuwa ishara ya kitaifa na kimataifa, chanzo cha fahari kinachowakilisha uzuri, nguvu, na umoja wa Tanzania.
“Tukubaliane kufanya kitu cha kipekee, kitu kitakachotupeleka ulimwenguni na kuacha alama katika historia. Kwa wabunifu, wanamitindo, na wote wanaoshiriki, tambueni kuwa hampo tu katika sehemu ya tamasha, bali mnakuwa sehemu ya historia ya kizazi kitakachovutia dunia. Hebu tufanye wakati huu uwe wa kukumbukwa milele”, amesema Magese.
Mbali na Magese, wengine walioteuliwa kuwa majaji ni Idris Sultan ambaye ni Muigizaji na mchekeshaji mashuhuri, Khadija Mwanamboka ambaye ni mbunifu maarufu na mwanzilishi wa sanaa mbalimbali.
Wengine ni Jokate Mwegelo, Kiongozi mashuhuri na Malkia wa Urembo hapa nchini, Martin Kadinda ambaye ni Mbunifu maarufu wa mavazi, Faraja Nyalandu, Kiongozi wa Jami na Malkia wa Urembo pamoja Nancy Sumari.
Awali akizungumza kuhusu Samia Fashion Festival Mwanzilishi na Muandaaji wa Tamasha hilo, Mwanamboka amesema amewashirikisha wanamitindo mbalimbali na kuungana nao katika tamasha hilo ili Kusaidia watoto wanaoishi na virusi Vya UKIMWI na Saratani.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED