Watumishi Wizara ya Madini watakiwa kutangaza mikakati ya wizara

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 05:50 PM Nov 28 2024
Watumishi Wizara ya Madini watakiwa kutangaza mikakati ya Wizara
Picha:Mpigapicha Wetu
Watumishi Wizara ya Madini watakiwa kutangaza mikakati ya Wizara

Watumishi wa Wizara ya Madini wametakiwa kuwa vinara wa kutangaza mikakati ya wizara hiyo inavyosimamia utekelezaji wa Sera na Mipango inayopelekea kuwepo kwa matokeo chanya katika Sekta ya Madini nchini.

Hayo yamesemwa leo, Novemba 28, 2024 na Naibu Waziri wa Madini , Dk.Steven Kiruswa wakati akifungua Baraza la Wafanyakazi Wizara ya Madini jijini Dodoma.

Dk. Kiruswa amesema kuwa, Sekta ya Madini ni kichwa cha serikali hivyo kupitia mikakati yake ukiwemo wa Vision 2030 unaosema madini ni maisha na utajiri ambao una lengo la kufanya utafiti wa kina kwa asilimia 50 ifikapo mwaka 2030 , tofauti na sasa ambapo umefanyika kwa asilimia 16.

Dk.Kiruswa ameongeza kwamba, mkakati huo ni muhimu kwa taifa kwasababu utawezesha kujua kiwango cha rasilimali madini na aina nyingine za madini na uwepo wa maji jambo ambalo litafungamanisha Sekta ya Madini na sekta  nyingine za kiuchumi kwa maendeleo endelevu ya taifa.

Sambamba na hapo, Dk. Kiruswa amefafanua kuwa,  Mkakati  mwingine ni Mining for Brighter Tomorror (MBT) ambao unalenga kushirikisha vijana na wakina mama katika mnyororo wa thamani madini kwa kuwapatia vifaa vya uchimbaji , kuwaunganisha katika mfumo wa masoko, kuwaongezea ujuzi wa kutambua maeneo ya kuchimba kulingana na taarifa za utafiti hivyo ni wajibu wetu kutangaza mikakati hii kwa jamii na taifa kwa ujumla.

Kuhusu ajenda ya Nishati Safi, Dk.Kiruswa amefafanua kuwa, Tanzania ina madini mengi ya kimkakati  ambayo yanazalisha nishati safi hivyo amewataka watumishi kutumia fursa hiyo kueleza kuhusu umuhimu wa kutumia Nishati Safi ambayo ni ajenda ya kimkakati kwa Taifa.

Naye, Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi, ambaye ni Katibu Mkuu Wizara ya Madini  Mhandisi Yahya Samamba ameeleza kwamba kupitia vikao vya Baraza, wajumbe wanapata fursa ya kujadili na kutathmini utekelezaji wa mipango iliyojiwekea kwa mwaka husika.

Mhandisi Samamba ameongeza kuwa wizara kupitia taasisi zake inaendelea kuijenga sekta ya madini kwa kufanya tafiti , kuongeza thamani madini, kuongeza mapato serikalini na kutoa taarifa za uwazi kwa jamii zinazotokana na  sekta ya Uziduaji kwenye Madini, Mafuta na gesi asilia.

Kwa upande wake , Mwakilishi wa Katibu Mkuu   TUGHE Taifa , Dk.Leonia Msafiri , ameishauri TUGHE  tawi madini kuendelea kuwashawishi watumishi kujiunga  ili kuweza kupanga ajenda za maendeleo kwa maslahi ya Watumishi na Wizara kwa ujumla.

Mwakilishi wa Kamishna wa Kazi Eunice Tesha amewashauri wajumbe wa Baraza na Wanachama wa Tughe kutumia jukwaa la TUGHE kueleza changamoto zilizopo sehemu ya kazi na namna ya kutafuta suluhisho ili kuendelea kuboresha mazingira ya kazi. 

TUGHE ni Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya Tanzania kilianzishwa mwaka 1996.