Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) umeanzisha Mradi wa Tuinuke Pamoja, wenye lengo la kuondoa umasikini, kuongeza ushiriki wa kifedha, uongozi, na kutumia mitandao ya kijamii kama nyenzo ya kuwapa wanawake wa vijijini fursa zaidi za kiuchumi na kijamii.
Akizungumza katika uzinduzi wa mradi huo jijini Dar es Salaam leo, Mkurugenzi Mtendaji wa TGNP, Lilian Liundi, amesema Tuinuke Pamoja ni hatua muhimu katika kuhamasisha jamii kuhusu usawa wa kijinsia, haki sawa, na kutokomeza ukatili wa kijinsia.
Mradi huo wa miaka mitatu unafadhiliwa na Ubalozi wa Ireland nchini Tanzania kwa kushirikiana na Mfuko wa Aga Khan. Awamu ya kwanza ya mradi itatekelezwa mkoani Dodoma, ambako zaidi ya wakufunzi 10 watachaguliwa kuwa mabalozi wa mabadiliko, wakihamasisha jamii kuhusu haki za kijinsia na maendeleo.
"Tumewachagua wanawake na wanaume wachache kuwa viongozi wa mabadiliko katika maeneo yao. Pia, mradi huu utatoa mafunzo ya mbinu za uchambuzi wa kijinsia na utafiti wa vitendo (PAR), ambazo zitawasaidia washiriki kuwa na ufanisi katika utekelezaji wa shughuli hizi," amesema Lilian.
Yusuph Kidanke, mmoja wa washiriki kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Kondoa, Dodoma, amesema kuwa mradi huu utasaidia kuongeza uelewa wa usawa wa kijinsia, hasa katika maeneo ambako wanawake wamekuwa wakifanya kazi za kilimo peke yao.
"Mafunzo haya yatasaidia kuongeza uzalishaji wa chakula kwa kaya, kwa sababu watu watapata uelewa wa umuhimu wa kugawana majukumu," amesema Kidanke.
Kwa upande wake, Meneja wa Mradi wa Tuinuke Pamoja kutoka Mfuko wa Aga Khan, Nestory Mhando, amewataka washiriki kutumia fursa hii kutatua changamoto zinazoikabili jamii zao ili kuchochea maendeleo ya kiuchumi kwenye kaya zao.
Mhando amesisitiza kuwa Tuinuke Pamoja haujazingatia tu masuala ya kijinsia na kiuchumi, bali pia unalenga kuwawezesha wanawake vijijini kuwa sehemu ya mabadiliko makubwa ya kijamii.
"Tunataka wanawake wa vijijini wapate fursa sawa za kimaisha, wawe na sauti katika maamuzi, na kutumia rasilimali kwa maendeleo yao na ya familia zao," ameongeza.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED