Maofisa elimu mguu sawa matumizi mtaala mpya

By Vitus Audax , Nipashe
Published at 05:22 PM Feb 05 2025
Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza, Balandya Elikana.
Picha: Vitus Audax
Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza, Balandya Elikana.

Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza, Balandya Elikana, amewataka maofisa elimu na watendaji wa sekta hiyo kuhakikisha wanaendana na mabadiliko ya utekelezaji wa mtaala mpya wa masomo ulioanza kutumika Januari 2025.

Elikana alitoa maelekezo hayo leo, Februari 5, 2025, wilayani Sengerema, wakati akifungua Kikao cha Maafisa Elimu na Wathibiti Ubora, kilicholenga kutathmini utekelezaji wa shughuli za elimu kwa mwaka 2024 na kuweka malengo ya kuboresha sekta hiyo kwa mwaka 2025.

Katika hotuba yake, amesisitiza umuhimu wa kutathmini changamoto na mafanikio yaliyopatikana, ili kuweka mikakati madhubuti ya kuboresha elimu zaidi.

MWANZA YAENDELEA KUFANYA VIZURI KITAALUMA
 

Katibu Tawala huyo ameeleza kuwa Mkoa wa Mwanza umefanya vizuri katika mitihani ya kitaifa, hususan kidato cha nne, ambapo ufaulu umefikia asilimia 98.2.

"Hili ni jambo la kujivunia, lakini hatupaswi kubweteka. Lazima tuendelee kujitathmini na kuweka mikakati thabiti ili kuhakikisha tunapanda zaidi kitaaluma," amesema Elikana.

Pia amewataka wataalamu wa elimu kushughulikia changamoto zinazokwamisha maendeleo ya elimu, kama vile:
✅ Wanafunzi kushindwa kumudu stadi za kusoma, kuhesabu na kuandika.
✅ Changamoto za ufundishaji duni.
✅ Uboreshaji wa miundombinu ya elimu.

Ofisa Elimu wa Mkoa wa Mwanza, Martin Nkwabi.

MICHEZO NA MIUNDOMBINU YA ELIMU
 

Elikana amesisitiza umuhimu wa kuandaa mpango wa kufanikisha Mkoa wa Mwanza kufanya vizuri zaidi katika mashindano ya UMITASHUMTA na UMISETA 2025.

Aidha, ameeleza kuwa serikali inaendelea kuwekeza katika uboreshaji wa miundombinu ya elimu, ambapo mwaka 2024, sekta ya elimu mkoani Mwanza ilipokea zaidi ya bilioni 24 kwa shule za msingi na bilioni 17 kwa shule za sekondari.

Kwa upande wake, Ofisa Elimu wa Mkoa wa Mwanza, Martin Nkwabi, amesema kuwa utekelezaji wa mitaala mipya ya elimu ya msingi, sekondari na ualimu umeanza, lengo likiwa kuwawezesha wahitimu kupata ujuzi wa kujiajiri na kuajiriwa.

1