USAID lajiondoa mitandaoni, lafunga tovuti, wafanyakazi kupewa likizo

By Vitus Audax , Nipashe
Published at 04:39 PM Feb 05 2025
USAID lajiondoa mitandaoni, lafunga tovuti, wafanyakazi kupewa likizo.
Picha: Mtandao
USAID lajiondoa mitandaoni, lafunga tovuti, wafanyakazi kupewa likizo.

Shirika la Marekani la Misaada ya Kimataifa (USAID) limejiondoa rasmi kwenye mitandao ya kijamii na kufunga tovuti yake, kufuatia agizo la Rais wa Marekani, Donald Trump, la kusitisha shughuli zake kwa siku 90 kwa ajili ya mapitio.

Tangu jana Februari 4, 2025, tovuti na kurasa za mitandao ya kijamii za USAID zilionekana kutokuwa na maudhui yoyote. Hata hivyo, kufikia Februari 5, 2025, tovuti hiyo ilianza kuonyesha taarifa rasmi kuhusu mpango wa kuwapumzisha wafanyakazi wake.

Taarifa hiyo ilieleza kuwa Ijumaa, Februari 7, 2025, saa 11:59 jioni, wafanyakazi wote wa USAID walioajiriwa moja kwa moja duniani kote watapewa likizo ya usimamizi. Hata hivyo, wafanyakazi walioteuliwa kushughulikia majukumu muhimu ya shirika, uongozi mkuu, na programu maalum wataendelea na kazi kama kawaida.

Wafanyakazi walioteuliwa kuendelea na kazi watapewa taarifa rasmi kutoka kwa uongozi wa shirika kufikia Alhamisi, Februari 6, 2025, saa 3:00 usiku.

Kwa wafanyakazi wa USAID walioko nje ya Marekani, shirika, kwa kushirikiana na Idara ya Mambo ya Nje ya Marekani, linapanga kuwarejesha nchini humo ndani ya siku 30, kulingana na taratibu na sheria husika.

Aidha, USAID imetangaza kusitisha baadhi ya mikataba ya Huduma za Kibinafsi (PSCs) na Mikataba ya Huduma ya Ushirika (ISCs) ambayo haijatajwa kuwa ya msingi.

Kwa mujibu wa shirika hilo, maombi ya kutaka kupewa msamaha kwenye uamuzi huo yatazingatiwa kwa kuzingatia sababu maalum kama vile masuala ya kifamilia, mahitaji ya matibabu, ujauzito, na changamoto za usafiri. Mwongozo zaidi kuhusu jinsi ya kuomba msamaha huo unatarajiwa kutolewa hivi karibuni.

USAID imesisitiza kuwa hatua hizi ni sehemu ya mpango wa muda, huku ikiwashukuru wafanyakazi wake kwa huduma yao na kuwahakikishia kuwa watapewa taarifa zaidi kadri hali inavyoendelea.