Shirika la Afya Duniani (WHO) limemtangaza Dk. Chikwe Ihekweazu kuwa Kaimu Mkurugenzi wa Kanda ya Afrika, huku likibainisha kuwa Mkurugenzi mpya wa Kanda atachaguliwa Mei mwaka huu.
Uteuzi huo unafuatia kifo cha aliyekuwa Mkurugenzi mteule wa WHO Kanda ya Afrika, Dk. Faustine Ndugulile, aliyefariki dunia Novemba 27, 2024, nchini India alikokuwa akipatiwa matibabu.
Baada ya kifo chake, Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, alipohudhuria hafla ya kuuaga mwili wake Desemba 2, 2024, alisema kuwa nafasi hiyo itaelekezwa kwa Mtanzania mwingine mwenye sifa.
Katika salamu zake, Rais Samia alisema: "Wanadamu tunapanga yetu, lakini Mungu anatupangia. Dk. Ndugulile ameiweka nchi pazuri, lakini Mungu amechukua kilicho chake.
"Tutaingia tena kwenye mashindano, tutatafuta Mtanzania mwenye sifa anayeweza kushindana na ulimwengu. Tutaweka mtu mwenye sifa ileile kutuwakilisha," alisisitiza Rais Samia.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED