MAMLAKA ya Rufani ya Zabuni za Umma(PPAA),imefanikiwa kudhibiti upotevu wa thamani ya zaidi ya billion 583 zilizoelekezwa kwa wazabuni ambao hawana uwezo wa kifedha na waliokosa sifa za kitaalamu za kutekeleza zabuni husika.
Hayo yamebainishwa na Katibu Mtendaji wa PPAA,James Sando, katika ufunguzi wa mafunzo ya ya moduli ya kushughulikia malalamiko na Rufaa kwa njia ya kielektoniki yalioambatana na tamko rasmi la kuanza kwa matumizi ya moduli kupitia mfumo wa NeST.
Anaeleza katika kipindi cha Machi 2021 mpaka sasa,walishughulikia mashauri 162, yaliotokana na michakato mbalimbali ya ununuzi wa umma kati ya mashauri hayo, PPAA ilizuia utoaji tuzo kwa zabuni 35, zenye thamani ya zaidi ya bilioni 583.
Anasema hatua hiyo ingechangia serikali kuingia katika mikataba ambayo ingesababisha kuwa na utekelezaji wa miradi isioridhisha,hivyo kusababisha upotevu wa fedha za umma na
kuchelewesha maendeleo stahiki kwa wananchi.
" Pia katika kipindi hiki,PPAA kwa kushirikiana na Wizara ya Fedha, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na taasisi inazosimamia ununuzi wa umma nchini, imeweza kushiriki kutungwa upya kwa Sheria ya Ununuzi wa Umma ya mwaka 2023 na Kanuni za Ununuzi wa Umma za Mwaka 2024 Sheria hiyo ilianza kutumika Juni,2024 na kanuni zake imeleta maboresho katika eneo la ununuzi na ugavi ikiwemo kupunguza muda wa kushughulikia malalamiko na rufaa zinazotokana na michakato ya ununuzi wa umma." anaeleza.
Akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Fedha,Dk. Mwigulu Nchemba,Kamishina wa Idara ya Sera ya Ununuzi wa Umma,Dkt.Frederick Mwakibinga, amesema matumizi ya moduli itasaidia kupunguza mianya ya rushwa na kuongeza uwajibikaji na uwazi.
" Rushwa ni tatizo linaloongeza ugumu wa maisha kwa wananchi wote lakini moduli hii inafaida ikiwemo kuokoa muda, gharama, kupunguza mianya ya rushwa, kuongeza uwazi na uwajibikaji pia kurahisisha zoezi zima la uwasilishaji wa malalamiko na rufaa kwa upande wa wazabuni" . anaeleza Dkt.Mwakibinga.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa PSPTB, Godfrey Mbanyi,amesema lengo la Serikali si kuzalisha migogoro mingi katika mchakato wa manunuzi kwa umma hivyo ni wakati wa kuwa wamoja na kuijenga nchi ili kupunguza migogoro , kuzingatia na kuielewa sheria na kufanya vitu sahihi.
"Fedha ikipotea Mwanza,siyo ya watu wa Mwanza ni ya Tanzania yote,Nikipata changamoto ya kiafya nikiwa Mwanza nitaenda hospitali iliopo hapa,nikikosa huduma kwa sababu ya fedha ya kununua dawa iliochezewa kiujanja ujanja maana yake umeniathiri mimi ingawa siyo Mkazi wa Mwanza hivyo wafanye kazi kwa kutanguliza maslahi ya taifa mbele na wawe na maadili". alisema
Aidha Mwenyekiti wa Chama cha Wakandarasi Taifa Mhandisi Stephen Makigo anaeleza kuwa Mamlaka ya zabuni ni suluisho katika kazi zao japo kuwa wanakabiliwa na madeni mazito.
Naye Mwenyekiti wa PPAA Jaji Mstaafu Sauda Mjasiri alieleza kuwa huo ni mwanzo siku za mbele watatanua wigo wataweza kusikiliza malalamiko kwa kutumia mtandao.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED