TAMWA yamlilia Pudenciana Temba

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 09:46 AM Jun 26 2024
Pudenciana Temba.
Picha: Maktaba
Pudenciana Temba.

MWENYEKITI wa Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA), Joyce Shebe, amesema amepokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha aliyekuwa mhariri wa gazeti la Daily News, Pudenciana Temba, ambaye ni miongoni mwa wanahabari wanawake aliyetumikia tasnia ya habari kwa weledi mkubwa.

Pudenciana alifariki dunia jana katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) alikokuwa akipatiwa matibabu kwa muda mrefu.

Akimwelezea alivyomfahamu, Joyce amesema alijipambanua hadi kufikia ngazi ya uhariri, akifanya kazi katika tasnia hiyo takribani miaka 30, akiandikia gazeti la Daily News.

“Mpaka anafariki alikuwa amefikia ngazi ya uhariri kwenye magazeti ya serikali TSN. Kwa upande wa TAMWA amekitumikia kwa uadilifu akiwa ni kundi la pili katika wale waliojiunga TAMWA, ukiachilia mbali waanzilishi,” amesema.

Joyce amesema ameshiriki katika harakati nyingi za TAMWA ikiwamo miradi mbalimbali, mafunzo na alijipambanua katika eneo la sekta ya afya.

“Alijiunga katika taasisi moja ya kimataifa inayojihusisha na masuala ya malaria, ukizungumza waandishi waliokuwa wakishiriki katika mikutano au mafunzo miongoni mwao alikuwa ni yeye,” amesema.

Joyce amesema pengo lake ni kubwa kwa kuwa katika eneo la habari za Kiingereza, wanahabari wengi hawakimbilii huko, hivyo walitamani aendelee kuwapo ili kuwanoa zaidi.

“Hatuna la kusema isipokuwa tunamshukuru Mungu kwa ajili yake kwa maisha yake na tutaendelea kumuenzi na tunamwombea pumziko la amani, tupo pamoja na familia tutaendelea kushirikiana nao mpaka atakapopumzishwa,” amesema.