Sasa Uchaguzi wa Mwenyekiti wa TLP Taifa, ni kama upo, haupo

By Sabato Kasika , Nipashe
Published at 06:01 PM Jun 25 2024
Richard Lyimo (kulia), kaimu mwenyekiti, Hamad Mkadam na mwenyekiti wa wanawake Nuru Mwangila.
Picha: Sabati Kasika
Richard Lyimo (kulia), kaimu mwenyekiti, Hamad Mkadam na mwenyekiti wa wanawake Nuru Mwangila.

UCHAGUZI wa Mwenyekiti wa Chama cha TLP Taifa, ambao umepangwa kufanyika Jumamosi ijayo, huenda usifanyike.

Hatua hiyo inatokana na Makamu Mwenyekiti wa chama hicho taifa, Dominatha Rwechungura kutofautiana kauli na Katibu Mkuu Richard Lyimo kuhusu uchaguzi huo.

Wiki iliopita Dominatha amewatangazia wajumbe wa mkutano wa uchaguzi kujiandaa kwenda Dar es Salaam kuchagua mwenyekiti, lakini Lyimo ametangaza kuahirishwa kwa uchaguzi huo.

Lyimo ametangaza uamuzi huo mbele ya waandishi wa habari katika ofisi za makao makuu ya chama hicho Magomeni Usalama Dar es Salaam leo.

Ametoa baadhi ya sababu kuwa ni ukosefu wa fedha za kulipia ukumbi na pia fedha za kulisha wajumbe wa mkutano huo.

Sababu nyingine alioitaja ni kwamba mmoja wa wanaotaka kugombea hawana sifa, kwa madai kuwa alishafukuzwa katika chama kwa utovu wa nidhamu.

Makamu Mwenyekiti Dominatha Rwechungura.
Hata hivyo, kauli hiyo imepingwa makamu hiyo ambaye alitua kikao hicho akiwa baadhi ya wajumbe na wagombea.

Ujio wa makamu huyo nusura uzushe vurugu baada kuingilia kati wakati Lyimo akizungumza wakidai kuwa anadanganya.
Hata hivyo, pande zote ziliitahidi kushisha jazba huku upande wa makamu mwenyekiti ukiondoka kwenda kuzungumza na waandishi wa habari eneo la mapokezi.

Katika mazungumzo hayo, Dominatha amesema uchaguzi itafanyika kama ulivyopangwa, na kwamba hawakubali uahirishwe tena.
"Fedha za kulipia ukumbi zipo katika akaunti, Lyimo na katibu mkuu msaidizi ndio wanatakiwa kusaini zitoke, lakini hawajafanya hivyo ili uchaguzi usifanyike," amesema Dominatha.

Amesema, atahakikisha wanazitoa, na kwamba iwapo ukumbi wa awali itakuwa umechukuliwa watakodi mwingine.
"Hatutakubali uchaguzi uahirishwe kwa sababu za watu watatu akiwamo Lyimo anayegombea nafasi hiyo, anataka ndiye achaguliwe tu," amesema.

Wanachama wakizozana.
Kwa mara ya kwanza, chama kilipanga kufanya uchaguzi Januari 8 mwaka jana, lakini ukaahirishwa hadi Machi 6, lakini pia haukufanyika ukapangwa kufanyika Mei mosi mwaka huo wa 2023.

Hata hivyo, uchaguzi huo pia haukufanyika ukapanguliwa hadi Desemba 28 mwaka jana, lakini haukufanyika, baadaye ukapangwa kufanyika Januari 28 mwaka huu, nao ukapigwa kalenda.

Sasa umepangwa kufanyika Juni 29, Jumamosi ijayo, lakini nao huenda ukaahirishwa kutokana na sintofahamu ambayo imeanza kujitokeza.

Mbali na Lyimo, wagombea wengine wa nafasi ni Mhandisi Aivan Maganza, Stanley Ndamugoba,  Kinanzaro Mwanga na Abuu Changaa.

Nafasi hiyo kwa sasa inakaimiwa na Hamad Mkadam baada ya aliyekuwa mwenyekiti Augustine Mrema kufariki dunia mwaka 2022.