Samia ataja mawili ya Mafuru yatabaki kumbukumbu kwake

By Restuta James , Nipashe
Published at 01:49 PM Nov 15 2024
Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan akitoa heshima za mwisho kwenye jeneza lenye mwili wa aliyekuwa Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango Marehemu Lawrence Nyasebwa Mafuru katika viwanja vya Karimjee Jijini Dar es Salaam jana.
PICHA: IKULU
Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan akitoa heshima za mwisho kwenye jeneza lenye mwili wa aliyekuwa Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango Marehemu Lawrence Nyasebwa Mafuru katika viwanja vya Karimjee Jijini Dar es Salaam jana.

RAIS Samia Suluhu Hassan, amemlilia aliyekuwa Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango, marehemu Lawrance Mafuru, na kueleza namna alivyoisaidia nchi katika nyakati mbili ngumu.

Amezitaja kuwa ni wakati wa tatizo la uhaba wa dola uliomlazimu kuunda kamati akiwamo Mafuru na nyingine iliyohusu ujenzi wa miradi na kutoa ushauri chanya uliosaidia kukwamua masuala hayo.

Rais Samia aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam, katika shughuli ya kuaga mwili wa Mafuru, aliyefariki dunia kwa ugonjwa wa saratani ya damu.

Alisema aliposikia Mafuru amefariki, alikumbuka alivyofanikisha kutatua tatizo la uhaba wa fedha za kigeni nchini, takribani mwaka mmoja uliopita.

Mwaka jana, Benki Kuu ya Tanzania (BoT), ililazimika kuuza Dola za Marekani milioni mbili kwa benki kila siku, ili kukabiliana na uhaba wa sarafu hiyo nchini. Uhaba huo ulisababisha baadhi ya wafanyabiashara, kuiuza kinyemela kwa bei ya ulanguzi.

“Tulipopata changamoto ya dola ndani ya nchin, niliunda kamati ambayo iliongozwa na (Nehemia) Mchechu akisaidiwa na Mafuru. Kamati ilifanya kazi kubwa na siku ya kufanya wasilisho mbele yangu, kuweka mpango mezani wa kuleta dola ndani ya nchi, Mafuru aliniambia, Mheshimiwa tukiufuata mpango huu, kama tulivyouleta nchi itaondokana na tatizo hili si muda mrefu.

Na leo wote ni mashahidi, badala ya kuzibembeleza benki kutupa dola, sasa zinatuita tukachukue dola kwao. Badala ya kulalamika nchi haina dola, nimesikia juzi wazalishaji wanalalamika, nchi haina shilingi,” alisema Rais Samia.

Alisema kwa kuwa Mafuru ameondoka, atawatumia wataalamu wengine kurejesha shilingi kwenye mzunguko wa uchumi.

“La pili, tulikumbwa na changamoto ya miradi katika sekta ya ujenzi na nikaita mkutano pale Zanzibar, katika kikao kile tulijadili mengi.

“Mwisho nikawaambia, katika hali kama hii tuliyofika, kati yenu mmoja angekuwa Rais, mngeamuaje? Nikasema leo najivua urais, ninampa Lawrance Mafuru na nikamwambia, Lawrance nyanyuka, wewe sasa ndiye Rais, ungefanyaje?

“Alisimama kwa unyenyekevu mkubwa, akaniambia mimi siyo Rais na urais uko mbali na mimi, lakini katika hali kama hii, akatoa mchango wake ambao hakika ulitutoa pale tulipokuwa na tukaweza kusonga mbele. Ndugu zangu, nimepoteza, tumepoteza kwenye taifa hili,” alisema Rais Samia.

Mbali ya kumsadia katika nyakati hizo mbili, Rais Samia alisema Mafuru alikuwa mshauri wake binafsi hata kabla hajamteua kusimamia taasisi za umma.

Alisema mwaka jana alimteua kuwa Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango, nafasi aliyoishika hadi alipopatwa na umauti, kazi aliyoifanya kwa uaminifu ndani ya mwaka mmoja.

Alisema hadi umauti unamkuta, Mafuru alikuwa anasimamia dhamana ya kuandika Dira ya Taifa ya Maendeleo (Vision 2050), ambayo wiki hii amekabidhiwa rasimu ya kwanza.

Alisema katika utumishi wa umma akianzia Hazina, Mafuru alifanya mageuzi na kuweka mifumo ya kitaasisi, ambayo yameendelea kufanyika kwa manufaa ya nchi.

Aliwashauri watumishi wa umma na sekta binafsi, kujifunza uchapakazi, ubunifu na uaminifu wake, kwa kutoa mchango wao wote katika nafasi wanazopewa ili kuacha alama chanya.

Awali, Msajili wa Hazina, Nehemia Mchechu, alisema Mafuru ndiye aliyefanya maboresho makubwa ya muundo wa ofisi hiyo.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo, alisema Mafuru alitoa mchango mkubwa kwa taifa na amefariki dunia bila deni, kwa kuwa alitumia karama alizopewa na Mungu kujenga familia na nchi.

Dk. Mkumbo alisema katika kuandika Dira ya 2050, walizungumza na Mafuru akiwa hospitalini India na kuweka maoni yake ukurasa kwa ukurasa wa rasimu hiyo.

Akisoma wasifu wa Mafuru, Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Dk. Tausi Kida, alisema alizaliwa Juni 20, 1972 mkoani Mara na kusoma shule za msingi na sekondari hapa nchini, kisha kujiunga Chuo Kikuu cha Dar es Salaam hadi ngazi ya shahada ya uzamili katika usimamizi wa biashara.

Alisema amefanyakazi sekta binafsi kwenye benki kadhaa hadi mwaka 2016, alipoteuliwa kwenye utumishi wa umma, akiwa Msajili wa Hazina.

 Alisema Mafuru alianza kuugua saratani ya damu Agosti mwaka huu na kutibiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), kisha akahamishiwa Apollo nchini India, ambako alipoteza maisha akiwa na umri wa miaka 52.

Katika ibada hiyo ya kitaifa, iliongozwa na Askofu Mkuu wa Kanisa la Waadventista Wasabato (SDA), Jimbo la Kaskazini mwa Tanzania, Mchungaji Mark Malekana, aliwakumbusha waumini kwa Zaburi ya 90:1-3.

Viongozi wengine waliohudhuria ni Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, mawaziri, makatibu wakuu, manaibu Spikawa Bunge, wafanyabiashara, Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete na Waziri Mkuu mstaafu, Mizengo Pinda.

Akitoa salamu za familia, mdogo wake, Maendeka Mafuru, aliishukuru serikali, Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Prof. Mohamed Janabi na watumishi wa Idara ya Dharura hospitalini hapo, kwa namna walivyopambana kuokoa maisha yake na kuuushukuru ubalozi wa Tanzania nchini India, kwa namna walivyokuwa sehemu ya familia.