CCT yaibuka na hoja nne uchaguzi mitaa

By Maulid Mmbaga , Nipashe
Published at 01:39 PM Nov 15 2024
 Mwenyekiti wa CCT, Askofu Dk. Fredrick Shoo.
Picha:Mtandao
Mwenyekiti wa CCT, Askofu Dk. Fredrick Shoo.

JUMUIYA ya Kikristo Tanzania (CCT) imeibua hoja nne, ikiwamo kuvisisitiza vyombo vya dola kuwa haitarajii kuona yaliyotokea katika uchaguzi wa mwaka 2019/20 yakijirudia tena.

Kwa mujibu wa jumuiya hiyo, Watanzania wana haki ya kugombea nafasi za uongozi na kuwachagua viongozi wanaowataka bila shinikizo lolote. 

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa CCT, Askofu Dk. Fredrick Shoo, alisema wameendelea kushuhudia siku za karibuni watu kupotea na wengine kuuawa kuelekea kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa, hivyo wanakemea vitendo hivyo na kuzitaka mamlaka husika kufanya ufuatiliaji wa kina utakaosaidia kupatikana majibu ili kuondoa taharuki na hofu iliyoko kwenye jamii. 

Pia alisisitiza umuhimu wa uchaguzi wa serikali za mitaa kusimamiwa na na kufanyika kwa haki na usawa, pamoja na kufanyika marekebisho ya katiba ili kuondoa changamoto zinazoathiri mchakato wa uchaguzi kila wakati.

 "Kumekuwapo na malalamiko kuwa baadhi ya wagombea hususani wa vyama vya upinzani wamewekewa vikwazo. Baadhi  ya ofisi zimekutwa zimefungwa wakati wa kurudisha fomu na fomu nyingi  hazikubandikwa au zimebandikwa vibaya na kusababisha kuharibika au kutodumu kwa muda mrefu kwenye mbao za matangazo. 

"Pia tumeshuhudia changamoto katika mchakato wa kukata rufani ambako siku ya kupokea rufani baadhi ya wasimamizi walifunga ofisi na kuzuia mapingamizi mengi, jambo linalosababisha malalamiko miongoni mwa wagombea. 

Tunasisitiza kwamba kuelekea uchaguzi mkuu wa 2025, kama hakutachukuliwa hatua stahiki kutakuwa na changamoto zile zile katika chaguzi zijazo," alisema Askofu Dk. Shoo. 

Alisisitiza wananchi kwamba ni muhimu kufuatilia kampeni kwa makini na kuchagua viongozi wanaoonekana kuleta maendeleo ya kijamii pamoja na  kudumisha amani na utulivu kabla, wakati na baada ya uchaguzi.

 Pia alihimiza wananchi kuepuka vishawishi vyovyote vya kiitikadi au namna yoyote inayoweza kusababisha uvunjifu wa amani pamoja na kumtanguliza Mungu katika kipindi hiki muhimu cha uchaguzi kwa ajili ya maendeleo  na ustawi wa taifa. 

Wakati huo huo, alishauri mamlaka husika kwamba endapo mgombea hana mpinzani sheria inaelekeza apigiwe kura ya NDIYO au HAPANA ili kutoa haki kwa wananchi kuchagua viongozi wanaowataka. 

Hata hivyo, alisisitiza vyama vya siasa kufuatilia na kusimamia kampeni za wagombea kutoka katika vyama vyao na kuhimiza ustaarabu na kuheshimiana katika kunadi sera za chama husika bila kutumia lugha mbaya za matusi au maudhi zinazoweza kuhatarisha amani ya nchi. 

"Tunahamasisha vyama vyote vinavyowania nafasi za uchaguzi kuweka mawakala waadilifu katika kusimamia upigaji kura, kuhesabu, kujumlisha na kutangaza matokeo ili kuepuka sintofahamu baada ya uchaguzi na kutupeana lawama. 

"Tunatoa wito kwa wasimamizi wa uchaguzi kutekeleza majukumu yao kwa uwazi, usawa kwa kuzingatia sheria zilizowekwa bila upendeleo wa aina yeyote. Tunatumia fursa hii kuishauri wizara husika kuwachukulia hatua pale inapothibitika wasimamizi wamefanya kwa makusudi au kwa uzembe. Hii itasaidia kurejesha imani kwa wananchi," alisema. 

Kuhusu kampeni za wagombea, Askofu Shoo alihimiza mamlaka na vyombo vyote vinavyohusika kutoa nafasi sawa kwa vyama vyote vya siasa vinavyogombea kufanya mikutano yao kwa uhuru na usawa bila kubughudhiwa.

 Pia alihimiza viongozi na wahusika wote kudumisha uwazi katika hatua ya kuhesabu na kujumlisha kura kwa kuzingatia sheria na kanuni zilizowekwa bila upendeleo ili kudumisha amani baada ya uchaguzi.

 Alisisitiza kuwa mamlaka husika kuzingatia usawa na uwazi katika kutangaza matokeo halisi ya uchaguzi kwa mujibu wa muda uliowekwa na bila ucheleweshaji wowote ambao mara nyingi husababisha kukosekana kwa imani na matokeo husika.