CHADEMA yatolea ufafanuzi hoja mbili zilizozua mjadala

By Elizabeth Zaya , Nipashe
Published at 02:18 PM Nov 15 2024
Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa CHADEMA, John Mrema.
Picha:Mtandao
Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa CHADEMA, John Mrema.

UONGOZI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) umetoka hadharani kujibu hoja mbili zilizoibuliwa hivi karibuni, yakiwamo madai ya "kuwapo fedha chafu ndani ya chama hicho", ukiwataka wenye ushahidi kuwasilisha.

Mbali na tuhuma za kuwapo fedha chafu, chama hicho kimepinga vikali madai kwamba viongozi wake wa juu wamefanya makubaliano ya siri ili kigawiwe madaraka kwenye muundo wa serikali au kipewe majimbo katika uchaguzi ujao.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa CHADEMA, John Mrema, kuibuliwa madai hayo kumesababisha wanachama, wapenzi wa chama hicho na wananchi kwa ujumla kutaka ufafanuzi rasmi.

"Hivi karibuni kumeibuka tena wimbi la hoja mbalimbali ambazo zilishawahi kuibuka siku za nyuma na ambazo zimesababisha wanachama, wapenzi wa CHADEMA na wananchi kwa ujumla kutaka ufafanuzi rasmi wa chama,”alisema Mrema.

Akijibu hoja hizo, Mrema alisema tuhuma za CHADEMA kuwa na fedha chafu au rushwa katika uchaguzi wa ndani wa chama, zimekosa ushahidi na maeneo mengine uchunguzi bado unaendelea.

"CHADEMA imekuwa mstari wa mbele kupambana na ufisadi, ubadhirifu na rushwa miaka yote. Kama chama kikiletewa ushahidi au vielelezo vya tuhuma hizo kutoka kwa mtu yeyote, tutafanyia kazi haraka iwezekanavyo kwa mujibu wa Katiba, kanuni na mwongozo wa chama dhidi ya rushwa wa mwaka 2012.

"Hivyo, tunamwalika mtu yeyote mwenye ushahidi au vielelezo vinavyotosheleza kuwezesha kuchukua hatua za kinidhamu kwa wahusika, awasiliane na Ofisi ya Katibu Mkuu au Ofisi ya Katibu yeyote wa kanda," alisema Mrema.

Akifafanua kuhusu hoja ya viongozi wa juu wa chama hicho kudaiwa kukaa vikao vya siri, Mrema alisema ni vema ikaeleweka kuwa kwa mujibu wa Katiba ya nchi, nafasi za juu za uongozi wa nchi, ikiwamo ya Makamu wa Rais, hugombewa na haitolewi mezani.

Alisema kuwa nafasi ya Waziri Mkuu hutokana na chama chenye wabunge wengi bungeni.

"CHADEMA katika vikao vyake vyote, haijawahi kujadili, kutoa au kupokea mapendekezo yoyote ya kitu kinachoitwa ‘Serikali ya nusu mkate’. Jambo hili kama linavyopotoshwa, halijawahi kuwa sera ya chama chetu. Hakijawahi kupokea, kujadili, kubeba au kuwa na ajenda na serikali katika vikao vyote vya chama au vile vya maridhiano kuhusu hoja tajwa.

"Ikumbukwe kuwa vikao vyote vya maridhiano vilifanyika mwaka 2022 na vikahitimishwa Januari mwaka 2023, ambapo Rais Samia Suluhu Hassan aliondoa katazo la shughuli za kisiasa, ikiwamo mikutano ya hadhara na maandamano. Na ni 30 na 31 palifanyika vikao vya mwisho ambapo tulishindwana, baada ya hapo hakuna kikao cha siri au hadharani kimefanyika baina ya CCM na CHADEMA," alifafanua.

Mrema alisema kuwa kwa kipindi chote cha mwaka 2023 na 2024, chama hicho kimekuwa katika programu mbalimbali zenye lengo kukihuisha kufuatia miaka saba ya kuzuiwa mikutano ya hadhara.

Kuhusu ajenda ya Katiba mpya, na madai ya mfumo huru wa uchaguzi, Mrema alisema hazijawahi kuachwa na chama hicho wakati wote wa kutekeleza programu zake kwa sababu yoyote ile kama inavyotaka kuaminishwa.

"Tunawasihi wanachama na wapenzi wetu waendelee kukilinda na kukijenga chama kirejeshe heshima yake iliyoporwa, tunawataka wanachama na viongozi wetu, kuwekeza nguvu katika uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji, vitongoji na kupuuza propaganda za kukigawa chama.

"Chama chetu kinaongozwa kwa mujibu wa katiba, kanuni, maadili, itifaki na miongozo mbalimbali pamoja na uamuzi wa vikao halali. Hii ndiyo silaha yetu kuu iliyokifikisha chama chetu hapa kilipo, tuwe makini na uchochezi, kufitinishwa kugombanishwa na mifumo iliyo nje ya mifumo rasmi ya kichama," alisema Mrema.