Samia kuhudhuria mkutano wa G20 Brazil

By Romana Mallya , Nipashe
Published at 01:43 PM Nov 14 2024
Rais Samia Suluhu Hassan.
Picha:Mtandao
Rais Samia Suluhu Hassan.

RAIS Samia Suluhu Hassan anatarajia kushiriki mkutano wa viongozi wa G20 utakaofanyika Rio de Janeiro, Brazil kwa siku mbili kuanzia Novemba 18, mwaka huu.

Mkutano huo umebebwa na kaulimbiu isemayo: “Kujenga Ulimwengu wa Haki na Sayari Endelevu”.

Mwaliko huo umetolewa na Rais wa Brazil, Luiz Inacio Lula da Silva, na Rais Samia atakuwa Rais wa kwanza mwanamke kuwahi kuhudhuria mkutano wa viongozi wa G20.

Pia ni Rais wa kwanza wa Tanzania kuhudhuria mkutano huo wa viongozi wa G20 tangu kupanuka kwa kundi hilo kutoka G8 hadi G20 mwaka 2009. 

Kwa mujibu wa taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, historia inaonesha kuwa Rais mstaafu wa Awamu ya Tatu, Hayati Benjamin Mkapa na Rais mstaafu wa Awamu ya Nne, Dk. Jakaya Kikwete, walishiriki mikutano ya G8 iliyofanyika mwaka 2005 na 2008 mtawalia.

Ushiriki huo wa Rais Samia katika mkutano wa viongozi wa G20 unaashiria kuongezeka kwa ushawishi na mwonekano wa Tanzania katika jukwaa la kimataifa.

 Wakati huo huo, Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo, katika mkutano wake jana na mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao nchini, aliwahakikishia  Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, unaotarajia kufanyika Novemba 27, mwaka huu, utakuwa huru, haki na wenye uwazi zaidi.

“Tunapojiandaa na mchakato huu muhimu wa kidemokrasia, serikali ilifanya kampeni kuhusu uandikishaji wapiga kura kwa nia ya kuhakikisha kila mwananchi anayestahili wakiwamo wanawake, vijana, watu wenye ulemavu na wenye mahitaji maalum wanapata fursa na nafasi ya kujiandikisha na kutekeleza haki zao za msingi za kikatiba,” alisema.

Kadhalika alisema Thabit Kombo iliyofanyiwa marekebisho ijulikanayo kama Toleo la 2024 imekamilika na hivi karibuni na itachapishwa rasmi na kupatikana kwa wadau wote.

Alisema sera hiyo itaendelea kuweka mkazo katika diplomasia ya uchumi na katika kanuni zilizopo za kulinda maadili ya kijamii.

Pia alisema inakuja na masuala ya ziada katika nyakati za kisasa ikiwa ni pamoja na matumizi ya Lugha ya Kiswahili kama nyenzo madhubuti ya diplomasia ya nchi.

“Ninapenda kuwafahamisha kuwa Tanzania itaendelea kubaki kuwa taifa dhabiti katika bara hili linalofurahia amani, usalama na utulivu na tutawekeza zaidi katika eneo hili ili kudumisha hali hiyo.

“Tanzania bado ina dhamira ya dhati ya kusimamia misingi ya utawala bora, haki za binadamu na kiraia na kudumisha demokrasia na maadili yetu ya kidemokrasia, kwa kuzingatia katiba, mifumo yetu ya kisheria na taratibu zilizowekwa kama taifa huru,” alisema.

Balozi Kombo alisisitiza dhamira ya serikali ya utekelezaji wa falsafa ya 4R za Rais Samia ambazo ni maridhiano, mageuzi, ustahimilivu na kujenga upya taifa.