JESHI la Polisi linamshikilia Deogratias Mbuya (40) makazi wa Legho Kilema, Wilaya Moshi mkoani Kilimanjaro kwa tuhuma za kumuua Baba mkwe wake aliyejulikana kwa jina Tibrus Mneney (72) baada ya kushindwa kutatua mgogoro wa ndoa.
Tukio hilo lilitokea jana Novemba 13,2024 katika Kijiji cha Legho Kilema, wakati wa kikao cha familia cha usuluhishi baina ya mtuhumiwa na mkewe, kilichokosa suluhu.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa, amethibitisha tukio hilo, akieleza kuwa ugomvi ulianza baada ya mtuhumiwa kuanza kumshambulia mama mkwe wake, Biritha Mneney (58), na baba mkwe aliingilia kati. Mtuhumiwa alimjeruhi Tibrus kwa kumkata na kitu chenye ncha kali shingoni, kichwani, na mkononi, na kusababisha kifo chake kutokana na kuvuja damu nyingi.
"Mtuhumiwa alikuwa na mgogoro wa ndoa na mkewe akimtuhumu kutoka nje ya ndoa mara baada ya kufanyiwa upasuaji kutokana na matatizo ya kiafya. Baada ya kushindwa kupata suluhisho alianza kumpiga mama mkwe( Biritha Mneney (58 ) ndipo baba mkwe (Tibrus Mneney) alipoingilia kati na kuanza kukatwa katwa ,"alisema Kamanda.
Kamanda amesema , mara baada ya mtuhumiwa kutekeleza tukio hilo, alitoroka na msako mkali uliendelea hadi leo Novemba 14 alipokutwa kwenye nyumba bovu ya Revocatus Mbuya akiwa hawezi kuongea na kueleza hivi sasa amelazwa katika Hospitali ya rufaani ya kanda KCMC kwa uchunguzi na matibabu zaidi.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED