JENGO LILILOPOROMOKA Samia: Kuna shida katika nondo, kuta

By Halfani Chusi , Nipashe
Published at 10:14 AM Nov 21 2024
DK. SAMIA: KARIAKOO ENDELEENI KUFANYA BIASHARA

RAIS Samia Suluhu Hassan amerejea nchini akitokea Brazil na kwenda moja kwa moja Kariakoo, jijini Dar es Salaam kuwafariji wafanyabiashara na wananchi kufuatia tukio la kuporomoka kwa jengo kulikosababisha vifo vya watu 20 na makumi wengine kujeruhiwa.

Vilevile, Mkuu wa Nchi amesema kuwa baada ya kutembelea eneo la tukio, amebaini kulikuwa na "shida katika usimamizi wa ujenzi wa jengo hilo", akitaja maeneo mawili mahususi nondo na kuta hazikuwa na ubora.

Akizungumza na wananchi baada ya kutembelea eneo la tukio, Rais Samia alisema kuwa watu waliofariki dunia kutokana na tukio hilo lililotokea Jumamosi asubuhi, ilikuwa 20 kufikia jana saa tatu asubuhi.

Rais alielekeza maduka ambayo yako mbali na eneo la tukio, yafunguliwe ili wafanyabiashara waendelee na kazi na kueleza kuwa majeruhi wanaopatiwa matibabu, wamebaki watatu na hali zao zinaendelea kuimarika.

Alisema jengo hilo limeporomoka kwa kuwa ujenzi wake hausimamiwa vizuri, kwamba hata kwa macho ya kawaida, linaonekana ujenzi wake haukuzingatia viwango stahiki.

Rais Samia aliyekuwa anazungumza kwa hisia za huzuni, alisema jitihada za serikali zililenga kuwaokoa wote walionaswa katika ajali hiyo wakiwa hai lakini isivyo bahati wengine imeshindikana.

Alisema tukio hilo limegusa hisia za wengi na si msiba wa wafiwa pekee, bali wa taifa zima.

"Tumeguswa na tukio hili, hata wenzetu waliokolewa bila shaka hawako sawa, lakini Mungu ana kazi nao, wajipe moyo na waendelee na shughuli zao kama kawaida," alisema.

Rais Samia alisema alipokea taarifa za tukio hilo akiwa Brazil alikoalikwa kushiriki "mkutano wa wakubwa wa dunia" -- G20, akatoa maelekezo na jana alikwenda kushuhudia hali ilivyokuwa na kubainisha kwamba janga lilikuwa kubwa.

"Maelekezo niliyopata nimeona hali na umoja wa watanzania katika majanga haya, janga hili kwangu tangu niingie madarakani kwa ukubwa ni la tatu.

"Lakini katika majanga yote tumeona watanzania wanavyojitoa kusaidia, kazi imefanyika kwa bidii na weledi mkubwa kunusuru watanzania wenzetu.

"Tukio hili limetupa ujumbe mkubwa wa kuangalia usalama wa majengo yetu Kariakoo. Wakati ninaonyeshwa, ukiliangalia lilivyojengwa, kuta zake na nondo, halikusimamiwa vizuri," alisisitiza Rais Samia.

Alisema tukio hilo ni somo kwa serikali na mpango uliopo kupitia tume iliyoundwa ni kuingia Kariakoo kuangalia ubora wa majengo mengine.

Rais pia aliwapongeza wananchi kwa kutokukimbilia kuchukua mali za wafanyabiashara baada ya janga hilo na kujikita katika uokoaji.

Alisema mali zote zilizopo ndani ya jengo hilo zitahifadhiwa mahali salama na kisha baadaye wataitwa wahusika kwa ajili ya kuzitambua. 

Rais Samia alisema taarifa itakayotolewa na timu iliyoundwa baada ya kukagua majengo, wataiweka bayana na kama itashauri kubomoa baadhi ya majengo yatabomolewa.

Alisema kuwa hata taarifa za tume iliyoundwa mwaka 2003 kwa kazi kama hiyo, zitajumuishwa na za timu mpya iliyoundwa na kufanyia kazi ushauri wa tume zote.

Pia aliwataka watendaji wa serikali na mtu mmoja mmoja kutimiza wajibu wake, akitolea mfano wa jengo lililoporomoka lilijengwa kwa vibali, lakini hakukuwa na usimamizi mzuri katika kutazama ubora wake.

ATEMBELEA MUHIMBILI

Akiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Rais Samia alitembelea baadhi ya wodi walimolazwa majeruhi wa ajali hiyo.

Akizungumza na baadhi ya wagonjwa hao, Rais Samia aliwapa pole na kuwataka wasikate tamaa kwa kuwa watapona na kurejea katika hali zao za awali.

Katika moja ya wodi, Rais Samia alimjulia hali mmoja wa waathirika wa tukio hilo aitwaye Jonas. Sehemu ya mazungumzo yao ilikuwa hivi:

Rais Samia: "Unaendeleaje Jonas, Pole! Ulikuwa unafanya nini Kariakoo?

Jonas: Nilikuwa ninamsaidia baba kuuza duka.

Rais Samia: Ulikuwa dukani kumsaidia baba, Mungu amekusaidia, Inshallah utapona! Madaktari wanawatibia, usijali utapona, ugua pole Jonas!

Jonas: Asante Mheshimiwa Rais!

Mmoja wa manusura waliokuwa Muhimbili jana, alisema ni mtahiniwa wa Mtihani wa Taifa wa Kidato cha Nne na alikuwa amefanya mitihani saba, alipaswa kufanya mtihani wa mwisho juma hili, lakini hajaufanya.