HakiElimu yataka usawa kwa shule za Kiswahili, Kiingereza

By Elizabeth Zaya ,, Grace Mwakalinga , Nipashe
Published at 10:41 AM Nov 21 2024
Mkurugenzi Mtendaji wa HakiElimu, Dk. John Kalage
Picha: Mpigapicha Wetu
Mkurugenzi Mtendaji wa HakiElimu, Dk. John Kalage

TAASISI ya HakiElimu Tanzania, imeiomba serikali kutengeneza mazingira ya usawa kwa shule za msingi za umma zenye mchepuo wa Kiingereza na Kiswahili.

Kadhalika, imehoji sababu za  shule  hizo kutoza ada kwa madai kuwa kufanya hivyo ni kinyume cha  Sera ya Elimu ambayo inazitaka shule za umma kutoa elimu bure.

HakiElimu pia imehoji sababu za shule za mchepuo wa Kiingereza kupewa hadhi ya juu huku zenye mchepuo wa Kiswahili zikishushwa hadhi.

Taasisi hiyo ambayo imekuwa ikijihusisha na masuala ya elimu kwa muda mrefu, imehoji sababu ya shule hizo za Kiingereza za umma  kupewa  kipaumbele zaidi kwa kuboreshewa mazingira ya kujifunzia na kufundishia kuliko shule za mchepuo wa Kiswahili.

“Kwa bahati mbaya kumekuwa na kasumba ya  kuamini kuwa shule za umma za mchepuo wa Kiingereza zina hadhi kuliko za umma za mchepuo wa Kiswahili. Dhana  hii inazidi kuota mzizi na kusambaa kwa watu wengi na kusababisha matabaka ndani ya mfumo wa elimu,” alisema Mkurugenzi Mtendaji wa HakiElimu, Dk. John Kalage,  wakati akizungumza na waandishi wa habari  Dar es Salaam jana.

“Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014 Toleo la 2023 inaeleza kuwa lugha ya kufundishia kwa elimu ya msingi ni Kiswahili isipokuwa kwa ambazo zitaomba na kukubaliwa kufundisha kwa Kiingereza  kwa mujibu wa sera hiyo,” alibainisha. 

Dk. Kalage alisema lugha zote mbili zinabeba hadhi sawa katika utoaji wa elimu nchini na si kweli kwamba kwa shule za mchepuo wa Kiingereza zinakuwa na hadhi zaidi ya zile za mchepuo wa Kiswahili.

Kuhusu utozaji ada kwa shule za mchepuo wa Kiingereza, Dk. Kalage alisema shule hizo zinafanya hivyo kinyume cha sera ya utoaji elimu msingi bila ada.

“Kwa mujibu wa uchambuzi wetu, watoto hulipa kati ya Sh. 300,000 na 600,000 kiwango ambacho kinasababisha wazazi wenye kipato duni kuwahamishia watoto kwenye shule za mchepuo wa Kiswahili. Kwa  nini shule za umma za mchepuo wa Kiingereza zinakiuka sera ya elimu ambayo inazitaka shule za umma kutokutoza ada?”  alihoji.

Dk. Kalage alitolea mfano wa  ufafanuzi uliotolewa hivi karibuni na Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Hassan Bomboko, kuhusiana na Shule ya Msingi Ubungo National Housing iliyodaiwa  kwamba imeuzwa.

“HakiElimu inapongeza uongozi wa wilaya ya Ubungo kujitokeza haraka kutoa ufafanuzi juu ya taharuki hiyo, lakini tumeshitushwa na kauli ya uongozi huo kwamba shule hiyo inapandishwa hadhi kuwa shule ya umma ya mchepuo wa Kiingereza.

“Katika ufafanuzi wake, uongozi  huo ulikanusha  madai kwamba shule hiyo haiuzwi, haibinafsishwi wala kubadili umiliki wake bali iko kwenye mpango wa maboresho na kupandishwa hadhi kuwa shule ya umma ya mchepuo wa Kiingereza. Si  kweli kwamba shule kutumia lugha ya Kiingereza  ndiyo inakuwa na hadhi zaidi ya zile zinazotumia lugha ya Kiswahili,” alisisitiza Dk. Kalage.

Kwa mujibu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, mpango wa serikali kuanzisha shule zinazofundisha Kingereza, unalenga kuwapa wazazi machaguo wanayoweza kuyamudu kuamua hatima ya elimu ya watoto wao.

Lengo lingine ni kuboresha ufundishaji wa lugha ya Kiingereza kwa sababu imebaini  udhaifu mkubwa kwa wanafunzi kutumia lugha hiyo baada ya kumaliza elimu ya msingi na kuendelea na masomo ya sekondari.