MKUTANO MKUU MAALUM CCM: Macho, masikio ya Watanzania Dodoma

By Waandishi Wetu , Nipashe
Published at 08:47 AM Jan 18 2025
Sehemu ya Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi CCM Taifa (NEC), wakiwa kwenye kikao jijini Dodoma jana.
Picha: Ikulu
Sehemu ya Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi CCM Taifa (NEC), wakiwa kwenye kikao jijini Dodoma jana.

MACHO na masikio ya Watanzania Dodoma. Ndivyo ilivyo kutokana na Mkutano Mkuu Maalum wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuanza leo jijini hapa ambao pamoja na mambo mengine, wajumbe takriban 2,000 watamchagua Makamu Mwenyekiti wa CCM, Bara kwa kupiga kura ya Ndiyo au Hapana.

Nafasi hiyo inajazwa baada ya aliyekuwa akishikilia nafasi hiyo, Kanali (mstaafu) Abdulrahman Kinana, kuomba kupumzika mwishoni mwa Julai, mwaka jana. 

Mbali na kumpata Makamu Mwenyekiti Bara, Mkutano Mkuu Maalum unatarajia kupokea taarifa za utekelezaji wa kazi za serikali ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) kwa kipindi cha mwaka 2022 hadi 2024.    

 Hata hivyo, kiu kubwa ya wanachama, wapenzi, wakereketwa na wafuasi na wapenzi wa siasa kwa ujumla, ni kujua nani atachukua nafasi hiyo nyeti ndani ya CCM. 

 Nafasi hiyo, mbali na anayeshika kuwa msaidizi wa Mwenyekiti upande wa Tanzania Bara, pia ina uzito wa kipekee uliowekwa na kanuni za Maadili na Uongozi za CCM, zinazomtambua kuwa ndiye Mwenyekiti wa Kamati ndogo ya Udhibiti ya Kamati ya Usalama na Maadili Taifa ndani ya chama hicho.

 Kamati hiyo, inaundwa na wajumbe wanne, ikiongozwa na Makamu Mwenyekiti Bara kama Mwenyekiti wengine ni Mkurugenzi wa Maadili ngazi ya taifa kama Katibu na wajumbe wawili wa Kamati Kuu kutoka Zanzibar na Bara.

 Kamati hiyo ndiyo yenye wajibu wa kusikiliza, kuhoji na kupendekeza adhabu kwa watuhumiwa wenye mashtaka yanayopelekwa kwa uamuzi, kwenye vikao vya ngazi ya juu. Wakati wa uchaguzi mkuu, kamati hiyo ndiyo ambayo huchambua na kupendekeza wanachama wanaowania nafasi mbalimbali katika uwakilishi wa dola, zikiwamo za ubunge na watia nia ya urais.   

 Kwa mantiki hiyo, nafasi hii inahitaji kumpata mtu imara atakayesimamia masuala ya kimaadili hasa kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu na suala la wanachama kuzingatia maadili ni jambo la msingi. Ulegevu wowote katika nafasi hiyo unaweza kusababisha chama kupata wagombea wasio na maadili wala sifa za uongozi. 

 Pia Makamu Mwenyekiti anayetakiwa kwa wakati huu ni yule ambaye atakuja kufanya kazi ya kuivusha salama CCM katika Uchaguzi Mkuu wa 2025.

 WARITHI WATARAJIWA 

Hadi sasa kuna watu kadhaa wanatajwa na kuzungumzwa kuwa huenda wana sifa za kushika nafasi hiyo kurithi ‘viatu’ vya Kinana.

 Makada wanaotajwa kuwa huenda watashika nafasi hiyo ni Waziri Mkuu Mstaafu na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa (CC-NEC) ya CCM,  Mizengo Pinda, Abdallah Bulembo, Stephen Wasira.

 Kutokana na hekaheka za mkutano huo, Nipashe jana ilitembelea katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dodoma na kuona barabara za kuingia katikati ya jiji na kuelekea ukumbi wa mkutano huo wa Jakaya Kikwete zikiwa zimepambwa kwa bendera na mabango yanayosomeka ‘Karibuni Mkutano Mkuu Maalum wa CCM Taifa’, mengine yakionesha kazi zilizotekelezwa chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuandikwa ‘Ametekeleza’.

Pamoja na kupambwa kwa mabango hayo, upatikanaji wa vyumba katika hoteli pamoja na nyumba za kulala wageni umekuwa wa shida tofauti na wiki moja iliyopita.

WAJASIRIAMALI WAFUNGUKA

Mmoja wa wajasiriamali anayeuza sare za CCM, Trabo Bwenda, alisema ametokea mkoani Morogoro kwa ajili ya kuchangamkia fursa za mkutano huo kwa kuwa wajumbe wanahitaji kuwa na sare ili kushiriki vikao na mkutano huo.

 Mfanyabiashara wa kuku katika Soko la Miembeni, Hussein Ali, alisema kufanyika kwa mkutano huo kumeongeza mzunguko mkubwa wa biashara kutokana na kuongezeka mahitaji ya kuku choma.

 “Unajua wageni wanapokuja Dodoma hasa kwa wingi wakati huu wa mkutano wa CCM wengi wao wanajua Dodoma wanapatikana kuku wa kienyeji, hivyo kunakuwa na uhitaji mkubwa wa kuku wa kuchoma. Tumejiandaa  kuhakikisha kwa kipindi chote wanapatikana ili kukidhi mahitaji hayo,” alisema.

 Naye mamalishe Mwadawa Omary alisema wameanza kuona ongezeko la wateja wa chakula kuanzia jana kutokana na wingi wa watu ambao wamewasili kwa ajili ya mkutano huo.

 “Ninaamini kwa siku hizi tatu ambazo vitafanyika vikao vya CCM tutapata kipato kikubwa hata wenzangu wanaochoma kuku, nyama na kuuza vinywaji tunatarajia tutanufaika na mkutano huu,” alisema.

 Mtendaji wa Chemba ya Wafanyabiashara, Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA) Mkoa wa Dodoma, Ringo Ilingo, alisema fursa anazoziona kwenye mkutano huo ni kwa wawekezaji wa vyumba vya kulala wageni, watoa huduma za vyakula watanufaika na mkutano huo.

 Alisema halmashauri za mkoa wa Dodoma zinatakiwa kutumia fursa hiyo kuonesha maeneo ya uwekezaji ikiwamo wa hoteli zenye hadhi ya kimataifa na nyumba za kulala wageni zenye ubora.

“Maeneo mengi ya kulala wageni bado hayana ubora kwani hoteli nyingi bado ni nyumba za chini taasisi za fedha zinatakiwa kutoa mikopo kwa watu kuwekeza maeneo ya huduma hizi za malazi. Hivi sasa Dodoma inakwenda kuwa mji wa kitalii, hivyo lazima kuanza kujipanga,” alisema Ringo.

Pia alisema kwa sasa Dodoma kuna mahitaji makubwa ya nyama lakini uzalishaji upo chini hivyo kushauri kuwapo na wawekezaji wa machinjio za kisasa ili kuongeza uzalishaji.

 Juzi, Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Amos Makala, alizungumza kwenye moja ya vyombo vya habari kuwa wageni na wajumbe 3,500 wanatarajia kuhudhuria mkutano huo.

 Mkutano huo mkuu, jana ulitanguliwa na vikao vya Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) vikiongozwa na Mwenyekiti Rais Samia Suluhu Hassan. Vikao hivyo pamoja na kuandaa Mkutano Mkuu Maalum, pia vilitarajiwa kupendekeza jina la atakayechukua nafasi ya Kinana.