SERIKALI inaendelea na ukamilishaji wa taratibu za kuanzisha Mfuko wa Nishati Safi ya Kupikia ili kuweka ruzuku itakayowawezesha wananchi wa kipato cha chini kumudu bei ya gesi.
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Khamis Hamza Khamis, aliiarifu Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira jana jijini Dodoma, alipowasilisha taarifa ya utekelezaji wa maazimio ya Bunge yaliyotokana na taarifa ya mwaka ya shughuli za kamati iliyowasilishwa bungeni Februari, mwaka jana.
Alisema kanuni za usimamizi wa miradi ya biashara ya kaboni zimebainisha ruzuku kupitia hakimiliki za kaboni zinazopatikana kutokana na kupunguza matumizi ya nishati inayochafua mazingira, hivyo ruzuku hiyo ni sehemu ya juhudi za kitaifa za kutekeleza malengo ya kupunguza gharama kwa watumiaji wa nishati safi.
Khamis aliieleza kamati hiyo kuwa katika jitihada za kupunguza gharama za matumizi ya nishati mbadala, serikali imetia saini makubaliano ya awali na wawekezaji kuhusu ruzuku ya Sh. bilioni 8.64 kwenye nishati safi ya kupikia na majiko 452,455 yamepata ruzuku.
Aidha, Naibu Waziri alisema serikali inaendelea kuhamasisha matumizi ya nishati mbadala kwa njia mbalimbali ikiwamo utoaji wa elimu kwa umma kupitia vyombo vya habari na ziara za viongozi.
Pia alisema Ofisi ya Makamu wa Rais inaendelea kushirikiana na wadau wengine wakiwamo Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kuhamasisha na kuhimiza halmashauri zote za vijiji kuainisha misitu yote ya vijiji yenye sifa ya kuingizwa kwenye mpango wa biashara ya kaboni.
Alisema uhamasishaji wa jamii kuhusu umuhimu wa biashara ya kaboni katika kuhifadhi mazingira na kuongeza kipato kwa jamii unaendelea kutolewa kwa wananchi.
Pia alisema serikali inaendelea kusimamia na kuhakikisha mikataba ya biashara ya kaboni inanufaisha wananchi na inafanyika kwa mujibu wa kanuni za usimamizi wa biashara ya kaboni.
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira inayoongozwa na Mwenyekiti, Jackson Kiswaga, iliipongeza Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kuwakutanisha wadau na kujadili changamoto za mazingira ili kuzipatia ufumbuzi.
Pia ilisisitiza elimu ya mazingira iendelee kutolewa ili wananchi wapate uelewa na kuachana na vitendo vya uharibifu wa mazingira vikiwamo uchomaji na ukataji wa miti.
Kamati ilisema elimu ya nishati safi ipewe msukumo kwa kuwa wananchi wengi, hususan wa maeneo ya vijijini, hawana uelewa wa umuhimu wa matumizi ya nishati safi ya kupikia, hivyo kwa kuwapa elimu wataachana na matumizi ya kuni na mkaa.
Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Mhandisi Cyprian Luhemeja, alisema hadi kufikia Desemba 30, mwaka jana, maombi ya miradi 65 ya biashara ya kaboni yalipokewa.
Alisema jumla ya miradi sita imepata barua za kukubaliwa kuanza mchakato wakati miradi sita imetimiza vigezo na hatua za kupatiwa barua inaendelea.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED