Mawakili wa Dk. Slaa wazusha tafrani kortini

By Grace Gurisha , Nipashe
Published at 08:27 AM Jan 18 2025
Aliyekuwa Balozi, Dk. Wilbroad Slaa, akiwa chini ya ulinzi wa askari Magereza wakati akitolewa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam jana, kuelekea mahabusu baada ya kukosa dhamana.
Picha: Iman Nathaniel
Aliyekuwa Balozi, Dk. Wilbroad Slaa, akiwa chini ya ulinzi wa askari Magereza wakati akitolewa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam jana, kuelekea mahabusu baada ya kukosa dhamana.

JOPO la mawakili wa mwanasiasa mkongwe nchini, Dk. Wilibrod Slaa, likiongozwa na Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Boniface Mwambukusi, limemwashia moto Hakimu Mkazi Mkuu Beda Nyaki wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, baada ya kutokusikiliza maombi ya kupinga dhamana ya mteja wao.

Moto huo ulianzishwa jana na Wakili Hekima Mwasipu ndani ya chumba cha wazi namba mbili cha mahakama hiyo, baada ya Hakimu Nyaki kukubaliana na jopo la mawakili wa serikali kwamba wasubiri kwanza uamuzi wa pingamizi la uhalali wa hati ya mashtaka ndipo maombi ya kupinga dhamana yasikilizwe. 

Baada ya tu hakimu kukubali kwamba kesi inaahirishwa hadi Januari 23, 2025  kwa ajili ya uamuzi huo, Wakili Mwasipu alisimama na kuzungumza kwa sauti ya juu kwa kutuhumu kwamba kinachoendelea si haki kwa mteja wao.

Wakili Mwasipu aliwageukia mawakili wa serikali na kuwaeleza kwamba wanachokifanya si haki kwa kuwa  Dk. Slaa ni mzee ana miaka 76 ni mgonjwa pia ni kama mzazi wao.

"Hebu mwangalieni huyu mzee ni kama mzazi wenu. Anaweza  kuwazaa nyie, hivyo  mnachokifanya si haki. Tulishakubaliana  sasa hivi mnakataa, si haki hata kidogo huyu mzee ni mgonjwa nyie," alidai Mwasipu. 

Sauti ya Mwasipu ilimsimamisha kwa hasira na jazba Mwambukusi ambaye alipiga vitabu vyake juu ya meza huku akidai kwamba si haki kwa sababu tayari walishakubaliana kusikiliza pingamizi pamoja na maombi hayo, hivyo kwa nini hakimu abadilike.

Chumba cha mahakama kiliendelea na mrindimo wa kelele, huku mmoja wa jopo la mawakili hao akimtaka Hakimu Nyaki kama hawezi kusikiliza kesi hiyo ajitoe kuliko kufanya anachokifanya.

Wakati hayo yote yanaendelea, Hakimu Nyaki alikuwa kimya akiwaangalia tu kwa sababu ni hali ambayo ilisababisha taharuki na asijue nini cha kufanya kwa kile ambacho kimetokea mbele yake kutoka kwa mawakili wa Dk. Slaa.

Kutokana na ukweli kwamba tayari Hakimu Nyaki alikuwa ameshapanga tarehe ya usikilizwaji kwa kesi hiyo, alitoka katika chumba hicho bila kutoa mashambulizi yoyote wala kujibu.

Kelele hizo ziliendelea huku wakidai kwamba hawaondoki mahakamani hapo bila Dk. Slaa.  

Hata hivyo, askari Magereza waliokuwa ndani ya chumba hicho, takribani sita, walimwondoa Dk. Slaa haraka na kumpeleka moja kwa moja ndani ya basi la Magereza na kuondoka.

Baada ya hapo, mawakili walidai kwamba wanakwenda kufungua shauri la maombi ya mapitio Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kutokana na kutoridhishwa na uendeshaji wa kesi hiyo unavyoendelea.

Wakati  hayo yote yanaendelea, Dk. Slaa alikuwa akitabasamu tu na alipoulizwa na ndugu yake mmoja mbona haonekani kushtuka, alisema hayo ni mambo ya kawaida katika masuala ya siasa, Dk. Slaa amerudisha rumande.

Mbali na Mwambukusi na Mwasipu, mawakili wengine wanaomtetea Dk. Slaa ni Edson Kilatu, Peter Madeleka, Sanga Melikiole, Sisty Aloyce na Mwanaisha Mndeme.

Jopo la mawakili wa serikali linaongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi Tawabu Issa, Clemence Kato, Michael Ngoboko, Nura Manja wakisaidiana na mawakili wa Serikali Abdon Bundala na John, lilikuwa kimya likiangalia kinachoendelea wakati mawakili wa Dk. Slaa wakizusha tafrani hiyo .

Hakimu Nyaki alisema ni vyema maombi ya dhamana yakasikilizwa baada ya uamuzi wa kupinga uhalali ya hati ya mashtaka kutolewa.

Awali, wakiwasilisha pingamizi juu ya hati hiyo ya mashtaka, Madeleka alidai kuwa anawasilisha pingamizi lao chini ya Kifungu 131 A (1)(4) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA)  Sura ya 20 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2021.

"Kwa mujibu wa rekodi za mahakama kesi hii imeletwa mara mbili tofauti huku upelelezi ukiwa haujakamilika na sheria iko wazi kwamba ni marufuku kuleta kesi ya jinai ambayo haipo serious mahakamani kama upelelezi haujakamilika," alidai Madeleka. 

Alidai kuwa katika kifungu hicho kimetaja kesi ambazo zinatakiwa kuletwa kwa mahakamani bila upelelezi kukamilika, shtaka analoshtakiwa nalo mteja wao lipo chini ya sheria ya mtandao. 

"Kwa mtu yeyote aliyesoma sheria vizuri na kuhitimu na mwenye akili timamu hawezi kushindwa kuelewa kwamba mashtaka ya mtandao sio mashtaka serious yaliyotajwa kwenye sheria hii."

"Kwa hiyo kwa kuwa wenzetu wasomi na nguli wa sheria wamethibitisha upelelezi haujakamilika wala hawajakiona hicho kifungu wanaomba tarehe nyingine ya kutajwa sisi tunaona hicho kinatosha kuiondoa kesi hii."

 Alidai kuwa kesi ya namna hiyo inapopelekwa mahakamani upelelezi unatakiwa uwe umekamilika, kwa maana hiyo Mahakama ni sheria iliundwa kwa Katiba kwa mujibu wa kutenda haki." Ni takwa la lazima la Katiba yetu kesi ifuatwe mteja wetu aachiwe huru kwa sababu limeletwa kinyume cha sheria."

Akijibu hoja hizo, Wakili Issa alidai kuwa katika tafsiri ya kawaida katika hicho kifungu lipo shtaka ambalo linaendana na la kuchapisha taarifa ya uongo, tafsiri yake ni kuweka wazi taarifa ambazo zinahatarisha usalama wa umma, ni miongoni mwa mashtaka ambayo hayana dhamana.

Dk. Slaa anatuhumiwa kusambaza taarifa za uongo kupitia mtandao wa X ( Twitter),

ilidaiwa kuwa kosa hilo alilitenda Januari 9, mwaka huu ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia mtandao huo wa kijamii, kupitia jukwaa lililosajiliwa kwa jina la Maria Salungi Tsehai @MariaSTsehai kwa lengo la kupotosha umma.