Meli kubwa ya kontena 4,000 yatia nanga Dar

By Joseph Mwendapole , Nipashe
Published at 11:47 AM Jun 25 2024
Meli iliyobeba makasha 4,000 yatia nanga bandari ya Dar.
Picha: Maktaba
Meli iliyobeba makasha 4,000 yatia nanga bandari ya Dar.

BANDARI ya Dar es Salaam imeweka rekodi kwa kupokea meli kubwa ya mizigo yenye urefu wa mita 294.1 iliyobeba kontena 4,000.

Meli ya mwisho kupokewa ilikuwa na urefu wa mita 267 hatua inayotafsiriwa kama sehemu ya mafanikio ya uwekezaji uliofanywa katika bandari hiyo.

Meneja Mizigo Mchanganyiko wa Bandari ya Dar es Salaam, Abed Gallus, amesema hayo baada ya meli hiyo kuwasili bandarini hapo na shehena hiyo.

Amesema meli hiyo ya (MSC ADU -V) imekuwa ya kwanza kubwa kuwasili katika bandari hiyo.

"Hii ni historia kwetu kwani hapo awali tulikuwa tunapokea meli zenye urefu wa mita 267, lakini sasa tuna uwezo wa kupokea meli zenye uwezo ukubwa wa mita 305 haya ni mafanikio makubwa kwetu kama Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari nchini (TPA),” amesema Abed.

Amesema uwekezaji mkubwa wa miundombinu uliofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita kupitia TPA katika Bandari ya Dar es Salaam umechangia kiasi kikubwa kuongezeka ufanisi wa kiutendaji.

Awali, bandari likuwa na kina cha wastani wa mita nane mpaka 12.7, lakini sasa kimeongezwa na kufikia mita 14.5 na kuwa na uwezo wa kupokea meli zenye urefu wa mita zaidi ya 305.

“Tunazipongeza hatua mbalimbali zinazochukuliwa na serikali ambayo imewekeza vya kutosha katika Bandari ya Dar es Salaam ikiwamo kuongeza kina na vitendea kazi katika bandari yetu na hivyo kutoa matokeo chanya ikiwamo kuanza kupokea meli kubwa,” amesema.

Aidha, moja ya faida ya kubwa kupokea meli kubwa za mizigo ni kupungua kwa gharama za kusafirisha mizigo na kuleta unafuu kwa wafanyabiashara na wasafirishaji wa mizigo, na kuchochea ushindani wa bandari zilizopo ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

"Kumekuwa na ufanisi mkubwa ikiwamo kuhakikisha upakuaji wa mizigo unafanyika kwa haraka zaidi kwani ndani ya saa 24 tuna uwezo wa kupakua wastani wa kontena 800 hivyo tunatarajia ndani ya siku tano meli hii itakuwa imeshapakua na kuondoka katika bandari yetu," amesema Abed.

Amesema Bandari ya Dar es Salaam ni miongoni mwa sita ambazo TPA inazisimamia na kwa kuliona hilo mamlaka imeendelea kuboresha nyingine ili kutoa msaada kwa Bandari ya Dar es Salaam ambayo zaidi ya asilimia 95 ya mizigo inapita katika bandari hiyo. 

"Tumeendelea kuboresha miundombinu ya bandari zetu ikiwamo pamoja na Bandari ya Mtwara na Tanga ambapo tayari tumeshanunua vifaa vya upakuaji mizigo kwani hapo awali Bandari ya Tanga, meli zilikuwa zinafungwa nje ya gati, lakini sasa hivi meli zinaingia kwenye gati,” amesema.

“Uboreshaji huu wote ni juhudi za mamlaka kuhakikisha bandari hizo zinatoa msaada kwa Bandari ya Dar es Salaam," amesema Abed.

TPA imeingia mikataba ya kiuendeshaji katika baadhi ya gati zake kwa Bandari ya Dar es Salaam ili kuongeza ufanisi na kufanya bandari hiyo kuwa kinara kwa uingizaji na usafirishaji wa mizigo kwa nchi nyingi zikiwamo za Maziwa Makuu na Kusini mwa Jangwa la Sahara.