Marufuku kubeba chakula, silaha na vifurushi treni ya SGR ikianza safari kesho

By Pilly Kigome , Nipashe
Published at 04:44 PM Jun 13 2024
Mkurugenzi wa TRC Masanja Kadogosa.

SHIRIKA la Reli Tanzania (TRC) limetangaza mifumo minne ya ukataji tiketi wa safari za SGR ikiwemo na kutoa katazo la kutoingia na chakula na vifurushi hatarishi ndani ya treni kwa safari zitakazoanza kesho Dar es Salaam kwenda Morogoro.

Mifumo huo ukiwemo wa kukata kwa pesa taslimu katika madirisha ya kukatia tiketi,  kukata tiketi  kwa kupitia 'control number', Tiketi Mtandao na ule wa TVM.

Akizungumza katika uzinduzi wa matayarisho ya kuelekea safari hiyo, Mkurugenzi wa TRC Masanja Kadogosa amesema nauli kwa daraja la kawaida Dar es Salaam Morogoro itakuwa ni Sh.13,000 na nauli nyingine itategemea na umbali wa safari. Na kwa safari zitakazotumia vichwa mchongoko kwa daraja la Juu (High Class) express kwa daraja la 'Loyal' nauli zake zitaanzia Sh.100,000 hadi 120,000 na kwa daraja la Biashara (Business) zitaanzia 70,000.

Aidha aliwatoa hofu watanzania na kuwahakikishia usalama wa abiria na mizigo utakuwepo kwa saa 24 kuanzia mwanzo wa hadi mwisho wa safari ndani na nje ya treni kwani ulinzi umeimarishwa katika vituo vyote kwakuweka ulinzi na usalama na doria katika safari hizo.

Afisa Biashara TRC Lilian Msele  amefafanua kuwa katazo la kuingia na chakula ni kwa abiria  bali watakaoruhusiwa ni wazazi wenye watoto chini ya miezi sita wataruhusiwa kubeba uji na maziwa na watawekewa mifumo ya kuwalisha watoto hao.

Vilevile katika daraja la Juu (Economy)mizigo itakayoruhusiwa ni ile iliyo chini ya kilo 30 na kwa daraja la Kawaida mizigo itakayoruhusiwa ni ile ya chini ya kilo 20.