Kesi ya mauaji ya mtoto kutajwa Januari 27

By Paul Mabeja , Nipashe
Published at 10:35 AM Jan 14 2025
Kesi ya mauaji ya mtoto kutajwa Januari 27.
Picha: Mtandao
Kesi ya mauaji ya mtoto kutajwa Januari 27.

KESI ya mauaji ya kukusudia ya mtoto Greyson Kanyenye (6), aliyekuwa akiishi Ilazo, jijini Dodoma, inayowakabili washtakiwa Kelvin Joshua (27) ambaye ni dereva bodaboda na Tumaini Msangi (28), bondia, imeahirishwa hadi Januari 27, mwaka huu itakapotajwa tena.

Washtakiwa hao wawili walifikishwa kwa mara ya kwanza katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Dodoma Desemba 30, 2024 kwa kosa la kuua kwa kukusudia tukio lilitokea mtaa wa Ilazo jijini Dodoma, Kata ya Ipagala Desemba 25, mwaka jana.

Hakimu Mkazi Daraja la kwanza, Charles Eligy, aliahilisha kesi hiyo jana hadi Januari 27, mwaka huu itakapotajwa tena huku washtakiwa wote wawili wakiendelea kusota mahabusu kutokana na kosa lao kukosa dhamana.

“Shauri hili linaahirishwa hadi Januari 27, mwaka huu litakapotajwa tena na washtakiwa wote wawili mtaendelea kubaki mahabusu kutokana na kosa lenu halina dhamana,” alisisitiza Hakimu Eligy.

Awali, Wakili Mwandamizi wa Serikali, Patricia Mkina, aliiambia mahakama hiyo kuwa kesi hiyo ilikuja jana kwa ajili ya kutajwa na upelelezi bado unaendelea.

“Mheshimiwa hakimu shauri hili lilikuja leo mbele yako kwa ajili ya kutajwa na upelelezi bado unaendelea hivyo kwa ridhaa yako tunaomba utupangie siku nyingine kwa ajili ya kutajwa tena,” alisema Mkina.

Desemba 30, mwaka jana, Wakili Mkina akisoma hati ya mashtaka, alisema washtakiwa wote wawili walifanya kosa la mauaji ya Greyson Desemba 25, 2024.

Baada ya kusomewa mashtaka hayo Hakimu Mkazi Denis Mpelembwa, alisema mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza mashauri ya mauaji.

“Kosa la mauaji halina dhamana hivyo mtarudi mahabusu hadi kesi yenu itakapotajwa tena Januari 13, 2025,” alisema Hakimu Mpelembwa.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, George Katabazi, akizungumzia tukio hilo Desemba 25, 2024, alisema mwili wa mtoto huyo ulikutwa ndani ya nyumba ukiwa na majeraha shingoni.

Katabazi, alisema tukio hilo lilitokea majira ya saa 1:00 asubuhi katika mtaa wa Bwawani, Ilazo Extension jijini Dodoma, nyumbani kwa Ofisa Uvuvi wa Mtera, Hamis Mohamed.

Alisema, Hamis na mama wa mtoto huyo walitoka kwenda matembezini na kumwacha chini ya usimamizi wa dereva bodaboda maeneo ya Ilazo, Kelvin Joshua.

Alisema, inadaiwa kuwa bodaboda huyo walimfahamu kupitia huduma ya usafiri anayoitoa kwa familia hiyo.

“Bodaboda huyu aliachiwa mtoto ili amwangalie kipindi ambacho watakuwa kwenye matembezi wawili hao wakati wa usiku, lakini waliporudi mtoto hawakumwona hadi asubuhi majira ya saa 1:00 walipomkuta mtoto kwenye chumba akiwa ameuawa akiwa na alama za kupigwa na kitu kizito shingoni,” alisema.

Kadhalika, Kamanda Katabazi alisema Jeshi la Polisi mkoani hapa linamshikilia bodaboda huyo kwa ajili ya uchunguzi zaidi wa tukio hilo.

“Tumemkamata bodaboda huyo kwa ajili ya uchunguzi wa tukio hili ambapo yeye amekanusha kuhusika na jambo hili, lakini tunaendelea na uchunguzi ili kubaini nini hasa kilitokea kwa mtoto huyu na kupelekea kifo chake,” alisema Katabazi.

Aidha, kamanda huyo alitoa wito kwa wazazi kuacha tabia ya kukabidhi watoto wao kwa watu ambao hawawajui vizuri ili kuepusha matukio kama hayo.