Kariakoo baadhi wagoma, wapo waliofungua; Mwanza wafunga

By Elizabeth Zaya ,, Elizabeth John , Nipashe
Published at 09:34 AM Jun 26 2024
Mgomo wa wafanyabiashara.
Picha: Maktaba
Mgomo wa wafanyabiashara.

WAFANYABIASHARA wa Soko la Kimataifa la Kariakoo jijini Dar es Salaam jana wamefungua maduka na kuendelea na biashara baada ya serikali kusitisha ukaguzi wa risiti za kielektroniki na ritani za kodi iliyokuwa ikifanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Asilimia ndogo ya wafanyabiashara hao, wameendelea kufunga maduka yao wakiitaka serikali kutekeleza kwa vitendo ilichoahidi.

Wakizungumza na mwandishi wa habari hii sokoni hapo, baadhi ya wafanyabiashara waliofungua maduka yao wamesema wamefanya hivyo kwa kuamini kwamba, serikali itatekeleza kwa vitendo iliyoahidi katika kikao kilichofanyika baina yake na viongozi wa wafanyabiashara.

“Jana (juzi) serikali iliahidi mwezi ujao itatatua matatizo yetu, tunaomba ifanye hivyo kwa vitendo, wapo wenzetu ambao bado hawajafungua, lakini sisi wengine tunaamini serikali tunaomba isituangushe itekeleze,” alisema Ruben Kaiza, mfanyabiashara wa duka la jumla la vipodozi.

Lucas Amon, mfanyabiashara wa nguo, amesema kero nyingine kubwa TRA kufilisi akaunti za wafanyabiashara.

“Tunaomba hizi sheria kandamizi zinazoipa TRA kufanya hivi hazifai ziondolewe, zinatuumiza sana wafanyabiashara wengi,” amesema Amon.

Baadhi ya wafanyabiashara ambao wamekutwa wakiwa wameketi nje ya maduka yao yakiwa yamefungwa, walisema wanachosubiri ni utekelezaji wa ahadi iliyotolewa na serikali.

“Sisi tunasema hatufungui mpaka tuone serikali inatekeleza kwa vitendo, mwaka jana ilitoa ahadi kama hizo na haikutekeleza. Hatufungui tunataka wazungumze kwa vitendo,” amesema mmoja wa wafanyabiashara wa duka la vitambaa kwa sharti la kutotajwa jina.

Baadhi ya wateja waliokutwa sokoni hapo akiwamo, Halima Ashraf, wameshukuru hatua ambazo serikali imechukua na kuhakikisha huduma kurejea.

“Tunashukuru leo (jana) tumepata bidhaa kwa maana jana (juzi) tulikuja tukakosa. Bidhaa nyingi tulizohitaji tumepata isipokuwa madera ndio tumekosa kwa sababu tumekuta maduka yamefungwa,” amesema Halima.

Katibu wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Mkoa wa Dar es Salaam, Riziki Ngaga, amesema tamko la viongozi linawaomba wafanyabiashara kufungua maduka yao kwa kuwa serikali imeahidi kutekeleza ilichowaahidi.

MWANZA

Wakati wafanyabiashara wa Dar es Salaam wakimaliza matatizo yao na serikali, mkoani Mwanza wamefunga maduka yao wakidai hadi kilio chao cha utitiri wa kodi kifanyiwe kazi. 

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara wa Mkoa wa Mwanza, Patrick Masagati, amesema hawatafanya biashara yoyote mpaka kodi isiyo rafiki kwa biashara zao zitakapoondolewa. 

"Tumechoka kusikia matamko ya serikali, tunahitaji mabadiliko ya sheria, yatakayokuwa na tija kwa pande zote mbili na si vinginevyo," amesema Masagati. 

Amesema viongozi wamefanya sehemu yao, lakini wafanyabiashara wameamua kugoma, ili kuishinikiza serikali ichukue hatua za kumaliza tatizo hilo.

"Jana na juzi, kulikuwa na vikao huko Dodoma, baina ya viongozi wa wafanyabiashara na uongozi wa serikali, majibu yaliyotolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Prof.  Kitila Mkumbo, ndiyo yaliyopelekea mgomo huu," amesema Masagati. 

WANANCHI

Baadhi ya wananchi akiwamo, Secilia Simon, mkazi wa Kata ya Pamba, wameomba serikali suala hilo limalizwe ili kutoleta athari kwao.

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda, akizungumza na Nipashe Digital kwa njia ya simu kuhusu mgomo huo, alisema kwa wakati huo hajafahamu kilichofanya wafanyabiashara hao wagome na kuahidi kukutana nao kesho ili wazungumze shida zao.

“Niwaombe wawe watulivu, tutajadili na tutaelewana, yale yatakayokuwa yako ndani ya uwezo wangu nitayajibu, lakini yale ya ngazi ya juu tutayapeleka sehemu husika, hivyo waendelee kudumisha amani na utulivu," amesema Mtanda.