DIRA 2050: Wataka sheria kuongeza walipakodi

By Restuta James , Nipashe
Published at 11:06 AM Jun 26 2024
Rais wa Chemba ya Wanawake Wafanyabiashara Tanzania (TWCC), Mercy Silla.
Picha: Maktaba
Rais wa Chemba ya Wanawake Wafanyabiashara Tanzania (TWCC), Mercy Silla.

WANAWAKE wametaja mambo matano wanayotaka kuyaona katika Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, kubwa zaidi likiwa ni sheria na sera zilenge kuongeza idadi ya walipakodi badala ya kila mwaka wa fedha kupandisha viwango vya kodi.

Vilevile, wametaka maendeleo ya rasilimali watu, mazingira wezeshi ya ufanyaji biashara, kuimarisha ujuzi na elimu ya ufundi pamoja na ujumuishaji wananchi kwenye masuala ya kifedha yapewe kipaumbele.

Wanawake hao kutoka sekta binafsi wameyasema hayo jijini Dar es Salaam, mbele ya Sekretarieti ya Tume ya Mipango inayokusanya maoni ya wananchi kwa ajili ya maandalizi ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Rais wa Chemba ya Wanawake Wafanyabiashara Tanzania (TWCC), Mercy Silla, amesema wanawake wanahitaji mazingira wezeshi ya ufanyaji biashara na elimu ya ujasirimali yapewe kipaumbele katika dira mpya.

"Wanawake wana kiu katika masuala ya kodi, wengi wako katika biashara ndogo na za kati (SME). Tunataka tuone serikali ikiweka mikakati mahsusi ya kunyanyua mwanamke. 

"Dira itamke kutakuwa na sera ya kumnyanyua mjasiriamali mdogo ili aweze kukua na kuchangia kwenye uchumi," amesema.

Mercy amesema wanawake wanataka kuwapo mfumo rahisi wa kurasimisha biashara ambao utapunguza tozo za mamlaka na taasisi za serikali kulingana na sekta anayofanyia biashara.

“Kuwe na kituo kimoja cha kulipia kila kitu. Mjasiriamali akirasimisha biashara, alipie katika dirisha moja usajili, leseni, viwango vya ubora na vyote vinavyohusiana na biashara yake.

"Tunaamini sehemu kubwa ya kodi itatoka kwa hawa walio wengi. Pia tozo zipunguzwe hasa kwa hawa wanaoanza biashara, utafiti unaonesha kwamba zipo kama 15 hivi," amesema.

Mwenyekiti wa Umoja wa Waokaji Tanzania (TBA), Fransisca Lyimo, amesema wajasiriamali wanatamani kuona sheria, sera na mipango ya nchi ikitengeneza mazingira rafiki ya ulipaji kodi na tozo za serikali.

"Kwa hali ilivyo ni kama Mamlaka ya Mapato (TRA) inatumia nguvu kubwa kudai kodi kwa sababu mwananchi haoni umuhimu wa kulipa kodi. Tunapendekeza elimu itolewe ili kuliko kuongeza tozo na kodi kila mwaka (tax rate), serikali iongeze walipakodi (tax base)," amesema.

Amesema kuongeza kodi kila mwaka kunapunguza idadi ya walipakodi na hivyo kusababisha watu wachache walipe na kundi kubwa lenye uwezo likishindwa kufanya hivyo.

Mwanzilishi na Mwenyekiti mstaafu wa TWCC, Jacqueline Maleko, amesema Dira ya 2050 ije na mpango wa kuunganisha rasilimali zinazotengwa kumwinua mwanamke ili tija ionekane kwa urahisi.

"Unakuta Halmashauri wana fungu, TASAF, benki na wadau mbalimbali wanatoa fedha, tukiweza kuziunganisha tunaweza kuwainua wengi kwa haraka," amesema.

Rais wa Sauti ya Wanawake Wajasiriamali (VOWET), Maida Waziri, amesema wanataka dira iweke mikakati ya kuongeza idadi ya wanawake katika ngazi za uamuzi na kuwapa fursa ya kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo.

Katika mkutano huo wanawake waliotoa maoni ni kutoka sekta mbalimbali, zikiwamo uchimbaji madini, nishati, ukandarasi, biashara, kilimo, usafiri na uzalishaji.