SALAMU za pongezi zimeanza kumfikia Donald Trump, kwa mgombea wa chama cha Republican.
Pongezi hizo zilianza kumiminika kutoka kwa wakuu wa nchi tofauti duniani, mara tu Trump alipotangaza ushindi wake katika uchaguzi wa rais wa Marekani.
Waziri Mkuu wa Uingereza, Keir Starmer, amempongeza mgombea wa chama cha Republican, Trump kwa kile alichokielezea kama "ushindi wake wa kihistoria" na "uhusiano maalumu" kati ya nchi zao mbili "utaendelea kustawi."
Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron, ameelezea utayari wake wa kufanya kazi pamoja. Macron alisema: "Hongera kwa Rais Donald Trump. Tuko tayari kufanya kazi pamoja kama tulivyofanya kwa miaka minne, kwa amani na ustawi zaidi."
Rais wa Tume ya Muungano wa Ulaya, Ursula von der Leyen, amesisitizia umuhimu wa uhusiano, Ulaya na Marekani.
Kansela wa Ujerumani, Olaf Scholz, pia amempongeza Trump, akisisitiza haja ya kufanya kazi na Marekani "kukuza ustawi na uhuru."
Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan, amemuelezea Donald Trump kama "rafiki yangu" baada ya kutangazwa mshindi wa uchaguzi wa rais wa Marekani, akielezea matumaini yake kwamba "uhusiano kati ya Uturuki na Marekani utakuwa imara."
Mfalme Abdullah II wa Jordan, pia amempongeza Donald Trump kwa ushindi wake katika uchaguzi wa Marekani, akisisitizia umuhimu wa kuimarisha hatua za pamoja za "kuhakikisha kuna amani na utulivu wa kikanda na kimataifa."
Rais wa Misri, Abdel Fattah el-Sisi, pia amempongeza Trump, akisisitiza nia yake ya kufanya kazi pamoja kuleta amani na utulivu katika Mashariki ya Kati.
Emir wa Qatar, Sheikh Tamim bin Hamad Al Thani, alielezea nia yake ya kufanya kazi na Trump tena, akisema katika chapisho kwenye jukwaa la X, "Natarajia kuimarisha uhusiano wetu na ushirikiano wa kimkakati, na kuimarisha juhudi zetu za pamoja za kukuza usalama na utulivu katika kanda na ulimwengu."
CHANZO: BBC
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED