MIEZI MITATU AJALI ZA ANGA: Zaacha simanzi kwa mataifa matatu, wamo Rais, Makamu wa Rais

By Christina Mwakangale , Nipashe
Published at 01:15 PM Jun 13 2024
news
Picha: Mtandao
Viongozi waliofariki katika ajali ya za anga hivi karibu.

KWA miezi mitatu mfululizo ajali za anga zimetikisa dunia, huku zikisababisha vifo kwa abiria waliomo ndani, wakiwamo viongozi wakuu katika nchi tatu.

Ajali hizo ni pamoja na ya Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi nchini Kenya Francis Ogolla, Aprili mwaka huu; Rais wa Iran, Ebrahim Raisi, Mei mwaka huu; Makamu wa Malawi Saulos Chilima, iliyotokea wiki hii.

Mbali na ajali hizo kusababisha vifo vya viongozi hao, zimesababisha idadi ya watu 27 kupoteza maisha wakiwamo maofisa wakuu wa serikali.

Kwa mujibu wataalam wa usafirishaji, usafiri wa anga ni miongoni mwa usafiri salama zaidi, kati ya aina tatu ambao ni anga; ardhini (reli na barabara); maji. 

Narscent Meena, rubani binafsi amezungumza na Nipashe, jana, kuhusu usalama wa usafiri wa anga na tahadhari za kuchukua kabla na wakati wa safari angani. 

“Kwanza kila ndege au helikopta kabla haijaruka tunaangalia ndege ya abiria itabeba watu wangapi, ili ndege iwe na uwiano na inakwenda wapi itaruka futi ngani, mafuta kiasi gani itabeba. 

“Pia, mhandisi anaikagua, anajidhihirisha kabla ndege haijaondoka iko sawa, anasaini na kuikabidhi kwa rubani. Kuna watu wa ‘road control’ wanahaikisha uwiano inaporuka na kutua viko sawa,” anasema. 

Anasema kwamba pamoja na ajali za ndege za viongozi kufululiza, bado usafiri wa anga ni salama, akisema mabadiliko ya hali ya hewa ghafla pamoja kupoteza mawasiliano, huweza kumuathiri rubani. 

“Tatizo la kiafya huweza kumuathiri rubani ghafla na pia rubani kuiamini ndege yake kwamba inaweza kufanya kazi vizuri, ila tahadhari huchukuliwa bila kujali imebeba viongozi au la.” 

JUNI MWAKA HUU 

Rais wa Malawi, Lazarus Chakwera, ametangaza siku 21 za maombolezo kitaifa hadi Julai Mosi, mwaka huu, kufuatia kifo cha Makamu wa Rais, Dk. Saulos Chilima, kilichotokana na ajali ya ndege, Jumatatu, wiki hii. 

Kwenye ajali hiyo, walikuwamo pia watu tisa nao wakifariki dunia. Ajali ilitokea katika hifadhi ya misitu wa Chikangawa, Juni 10, mwaka huu. 

Ndege hiyo ilikuwa unaelekea kutua katika uwanja wa Kimataifa Mzuzu, uliopo kilomita 380 kutoka Kaskazini mwa mji Mkuu Lilongwe.  

Chilima, na maofisa wengine alikuwa akisafiri kuhudhuria mazishi ya aliyekuwa Waziri wa serikali hiyo, Ralph Kasambara. 

 Mke wa rais wa zamani Bakili Muluzi, Shanil Dzimbiri ni miongoni mwa abiria waliokuwa kwenye ndege hiyo, kwa mujibu wa taarifa ya rais Chakwera. 

Ndege aina ya Dornier 228 ilitangazwa  kupotea kwenye rada ilipofikia eneo la hifadhi ya misitu Chikangawa na June 11, mwaka huu, ikathibitishwa imepata ajali. 

Chilima, alikuwa mwanasiasa maarufu katika siasa za Malawi, na kabla ya kujiunga na siasa alichangia kujua kwa kampuni ya Airtel nchini humo na kukuza mapato.  

Kisiasa, amehudumu katika kiti hicho tangu mwaka 2014 akipambana na rushwa na kukumbana na changamoto kadhaa. 

Mazishi ya kitaifa yanaangazia mchango wake katika nchi. 

Chilima alikuwa amerejea tu kutoka katika ziara ya kikazi nchini Korea Kusini, kwenye kongamano la Korea Afrika Summit, mjini Seoul, siku ya Jumapili, mwishoni mwa wiki. 

Chilima, ameacha mke Mary mmna watoto wawili. 

APRIL MWAKA HUU 

April, mwaka huu, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi nchini Kenya, Francis Ogolla alifariki kwa ajali ya helikopta. 

Rais wa Kenya, William Ruto alitangaza kifo cha Ogolla pamoja na maofisa wengine tisa wa jeshi, huku wawili wakinusurika.

 Ogolla alifariki baada ya helikopta aliyokuwa akisafiria pamoja na maofisa wengine kuanguka eneo la Kaben, Marakwet Mashariki.

 Ogolla alichukua nafasi ya kuongoza jeshi tangu April 28, mwaka jana.

 Mashuhuda walisema kuwa ilishika moto wakati wa kuanguka. Eneo hilo lilizingirwa mara baada ya ajali hiyo.

 Maofisa hao walikuwa wakichunguza eneo hilo kabla ya kutumwa kwa wanajeshi zaidi kukabiliana na wezi wa mifugo katika eneo hilo.

 Helikopta hiyo ya jeshi la Anga la Kenya aina ya Huey, ilikuwa imetoka katika shule moja ya msingi ya eneo hilo hadi ilipoanguka na kuwaka moto.

 Ogolla, aliteuliwa kuwa Mkuu mpya wa Majeshi ya Ulinzi katika mabadiliko katika jeshi, akichukua hatamu kutoka kwa mtangulizi wake Jenerali Robert Kibochi.

Kibochi alimkabidhi Ogolla kama Mkuu wa majeshi, baada ya kufikisha umri wa kustaafu.

 MEI MWAKA HUU

 Mei, mwaka huu, Rais wa Iran, Ebrahim Raisi, pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje, Hossein Amir-Abdollahian na wengine saba, walithibitishwa kufariki dunia katika ajali ya helikopta iliyotokea kaskazini-magharibi mwa Iran, kwa mujibu wa televisheni ya taifa.

Shirika la habari la serikali (IRNAA), lilisema kwamba ndani ya ndege hiyo pia alikuwamo Ayatollah Mohammad Ali Al-e Hashem, imamu wa Swala ya Ijumaa katika mji wa Tabriz, na Jenerali Malek Rahmati, gavana wa jimbo la Iran la Azabajani Mashariki.

Kamanda wa Kitengo cha Ulinzi wa Rais, Sardar Seyed Mehdi Mousavi, pia aliuawa, pamoja na walinzi kadhaa na wafanyakazi wa helikopta ambao bado hawajatajwa.