Maandamano Kenya, Rais Ruto atoa neno

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 12:13 PM Jun 25 2024
RAIS wa Kenya, William Ruto.
Picha: Maktaba
RAIS wa Kenya, William Ruto.

RAIS wa Kenya, William Ruto, amesema kwamba yuko tayari kufanya mazungumzo na maelfu ya vijana waliofanya maandamano kwa amani wiki iliyopita kwa lengo la kupinga mapendekezo ya nyongeza ya kodi.

Maandamano hayo yaliandaliwa kwenye mitandao ya kijamii na vijana Wakenya wengi wenye umri mdogo maarufu kama (Gen-Z) ambako wakati wa utekelezaji wake waliyarusha moja kwa moja kwenye mitandao ya kijamii.

Ilielezwa kuwa vijana hao wameendelea kuonyesha msisitizo juu ya kutoridhishwa na sera za kiuchumi za serikali ya Rais Ruto.

Ikiwa ni tamko lake la kwanza tangu kufanyika kwa maandamano hayo, Rais Ruto jana alisema “Ninajivunia sana vijana wetu, wamepiga hatua mbele kwa kufanya maandamano ya amani na ninataka kuwaambia kwamba tutawashirikisha.”

Aliongeza kuwa serikali yake itafanya mazungumzo na vijana ili kwa pamoja walijenge taifa la Kenya liwe kubwa zaidi.

Aidha, licha ya kauli ya kiongozi wa taifa hilo bado upande wa waandaaji wa maandamano hayo ya kupinga ongezeko la kodi haujatoa majibu kama wanakubaliana na wito wa Rais Ruto au la huku wakiitisha maandamano mengine ya kitaifa leo.

Hata hivyo, pamoja na Rais Ruto kuyaita maandamano hayo kuwa ni ya amani, wanaharakati wa haki za binadamu wameripoti vifo vya waandamanaji wawili vilivyotokana na maandamano Alhamisi mjini Nairobi.

Ilielezwa kuwa maandamano hayo kwa kiwango kikubwa yalikuwa ya amani, lakini maofisa wa Jeshi la Polisi walirusha mabomu ya kutoa machozi na maji ya kuwasha kwa siku nzima ili kuwatawanya waandamanaji waliokuwa karibu na Bunge.

Kwa mujibu wa taarifa ya Tume ya Haki za Binadamu ya Kenya, kijana Evans Kiratu (21), alipigwa bomu la kutoa machozi wakati wa maandamano hayo na alifariki akiwa hospitalini.

Polisi ya Kenya ilisema inachunguza madai kukusu kupigwa risasi na maofisa wa polisi kijana mwenye umri wa miaka 29 jijini Nairobi baada ya maandamano hayo. Huku Mamlaka Huru ya Kusimamia Jeshi la Polisi nchini Kenya (IPOA) ikisema imeorodhesha kifo hicho kuwa ni matokeo ya kupigwa risasi na polisi.

Vile vile, mashirika kadhaa, likiwamo la ‘Amnesty International Kenya’ yalisema takriban watu 200 walijeruhiwa katika maandamano hayo yaliyohusishwa maelfu ya vijana walioingia barabarani kupinga mswada wa sheria ya kuongeza kodi Kenya.

Serikali ya Rais William Ruto inayokabiliwa na uhaba wa fedha ilikubali kufanya mabadiliko baada ya mamia ya waandamanaji vijana kukabiliana na polisi katika mji mkuu wa Kenya.

KUHUSU KODI

Pia serikali nchini humo umetetea mipango ya kuongeza kodi kwa kiwango cha dola bilioni 2.7 (Sh. trilioni 7) ili kupunguza nakisi ya bajeti nchini humo. Na kwamba nyongeza za kodi zilizopendekezwa zinahitajika ili kuijaza hazina yake na pia ni hatua itakayoisaidia Kenya kupunguza utegemezi wa kukopa kutoka nje.

Kenya ina mlima wa deni, na gharama za kushughulikia ulipaji wa madeni zimeongezeka kutokana na kushuka kwa thamani ya sarafu ya nchi hiyo katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, hali inayoifanya serikali ya Rais Ruto kuwa kwenye kipindi kigumu.

Waandamanaji walisema ongezeko la kodi mpya zinazopendekezwa katika muswada wa sheria ya fedha, zitaathiri uchumi na zitaongeza gharama za maisha kwa Wakenya ambao tayari wanakabiliwa na hali ngumu.

Kenya ni mojawapo ya nchi zenye uchumi unaokua katika eneo la Afrika Mashariki lakini theluthi moja ya watu wake milioni 51.5 wanaishi katika umaskini.

DW