Kisa cha mwanamume mkware aliyemtongoza mtalaka wake

By Adam Fungamwango , Nipashe Jumapili
Published at 09:41 AM Jun 09 2024
news
Picha: Mtandao
Upendo.

INAWEZEKANA kabisa waliosema hakuna mwanamke mbaya duniani walikuwa sahihi kabisa. Wanasema mwanamke kama anapewa matunzo, ikiwemo chakula, mavazi na akaishi kwa amani bila mikwaruzo, vituko na vipigo, basi anapendeza mithili ya malkia.

Kuna baadhi ya wanaume wanashindwa kutekeleza majukumu yao kwa wake zao na kuwafuata warembo wengine nje.

Lakini hakumbuki kuwa awali wakati anamtongoza na kumshawishi amuoe, alikuwa mzuri na mrembo, kuliko hata huyo msichana wa nje anayemfuatilia.
 Sasa utajiuliza kwa nini anamuacha mkewe na kufuata wengine mitaani?  

Kwanza ni tamaa, halafu pia amejisahau kumtunza mkewe kiasi kwamba amekuwa hapendezi tena kama zamani. Anawageukia wengine. Kilichotakiwa hapo ni kitu kidogo tu, kumjali na kumtunza mke ili arejee kwenye chati kama zamani. Baadhi ya wanaume wanaona kama wameshaanza kupitwa na wakati.

 Waswahili wana msemo wao mmoja, kondoo haoni thamani ya mkia wake mpaka ukatwe.

Huyo huyo mkeo unayemdharau siku akikuponyoka ndiyo utaona thamani yake. Unaweza ukaja kumuona ni mrembo kuliko wale unaowakimbilia barabarani.
 Nitoe kisa kimoja cha mwanaume aliyekuwa na mke kwenye ndoa ambayo iligeuka kuwa ndoano.

 Mwanamke, alinyanyaswa, akapigwa, akadhalilishwa mpaka basi. Wakati mwingine alikuwa akifukuzwa usiku wa manane mvua ikimnyeshea. Mwanaume anamfukuza aende kwao. Anampiga na kumvutia nje, ambako kuna mvua, pia usiku mkubwa ambao una hatari ya kila aina. Kisha anafunga mlango. Mke atalala mlangoni hadi asubuhi, au atatafuta sehemu salama, asubuhi anarudi kule kule kwenye moto na mateso.

 Hakuwa mjinga, alikuwa anatafuta muda na wakati sahihi. Akabeba kilicho chake akaondoka. Mume alidhani masihara, labda anaweza kurudi kesho au keshokutwa, wapi! 

Hadi talaka ikatolewa. 

Miaka mitatu baadaye jamaa alikutana na mwanamke mrembo njiani. Akapagawa, akamfuata na kueleza jinsi alivyojisikia faraja baada ya kumuona. Akamsifia alivyopendeza na akaomba awe mpenzi wake, ikiwezekana amuoe. Mwanamke akamuangalia, akatabasamu. Akaanza kufunguka moja baada ya lingine.

Majibu ya mwanadada huyo yapo katika wimbo wa Maquis Original, Sendema ya Moto, katika kibao chao kiitwacho, 'Kaiba', ambalo ndiyo jina ma mwanamke huyo. Wimbo huo ulitungwa na Tshimanga Kalala Asossa, miaka ya 1990.

 "Unachoshangaa sasa ni nini we babu? Au unafikiri siyo mimi un'tamani tena eee, basi mimi ni yule yule Kaiba, uliyekuwa unanitelekeza, unanifukuza, kwa kashfa usiku mwingi mvua ikininyeshea bila huruma eee, mama mama.

 Usinione hivi leo nimependeza, hii ni kazi nzuri ya mwezio babu kanithamini eee, basi mimi ni yule, Kaiba, uliyekuwa unamtelekeza, unanifukuza, kwa kashfa usiku mwingi mvua ikininyeshea bila huruma, mama.

 Hata hivyo, mama ngoya ee, dunia kabla hujafa hujaumbika eee, namshukuru Mungu uliniacha salama eee, mama ngoya eee, ngoya, mimi kaiba nimetulia, mama ngoya eee, ngoya mimi Kaiba ee."

 Haiitaji hata ufafanuzi kuwa kumbe mwanadada huyo ni yule aliyekuwa mkewe.

 Mwanamke sasa akaanza kumfungukia yale yote aliyokuwa akimfanyia huko nyuma, mpaka mwanaume akaona aibu.

 Aibu kubwa ilimpata kwa sababu kwanza alimtongoza mtalaka wake ambaye mwanzoni alimuona si lolote si chochote, lakini sasa amepata wa kumtunza amerudi kwenye chati, amekuwa mrembo kuliko mwanzo alipokuwa na umri mdogo. Pili kuonyesha kuwa alikuwa amemsahau kwa sababu ya urembo kuongezeka na kunawiri, kulimfanya aonekane ni kweli alikuwa hajui kutunza mke. Tatu maneno aliyopewa, mwenye hakuwa na hamu.  Kila kitu kikaishia hapo. 

Niwaambie tu wanaume kuwa hawawezi kushinda vita na mwanamke hata siku moja kama atakupania.

 Wanaume wanane kwa kumi wamejikuta wakishindwa vita na wanawake kwa sababu ya mbinu zao kabambe ikiwemo kujifanya dhaifu, wao ni wepesi kudanganywa na kushawishiwa. Mtego huo.

 Wanawake wengi wanajua wakati gani sahihi wa kumshinda mwanaume, ila wanaume wengi hawajui. 

Mwanamke ni kiumbe anayetumia hisia zake kuficha hila, njama na akili zake usizitambue. Ni rahisi kulia au kuzuga katika mbinu ili uingie mkenge.

 Ni kweli utamtesa, utamdharau na kumfanyia yote utakayoweza kumfanyia, ni mvumilivu wa mateso, lakini kumbuka ipo siku moja tu atakushinda kama anataka.  Ukimtesa, akiamua kujibu mashambulizi  wanajua muda sahihi wa kufanya hivyo.

 Mara nyingi ni pale unapodondoka kinafasi, kicheo, kihadhi, uzee na kupoteza mamlaka na sauti mbele ya watoto wako mwenyewe.

 Cha kufanya hapa kwa wanaume, ni kuwapenda, kuwajali na kuwatunza, na kwa sababu ni watu wa hisia, hupendezwa na hilo na kuwa wapole, wakarimu, huruma na upendo kwenye maisha yote ya ndoa.

Tuma meseji 0716 350534