BASHAR al-Assad, Hosni Mubarak, Zine al-Abidine Ben Ali, Muammar Gaddafi na Ali Abdullah Sale ni wakuu wa nchi zenye asili ya kiarabu, wakiziongoza nchi kwa vipindi tofauti, wengi kuanzia mwaka 2011.
Waliongoza nchi zao, kwa vipindi tofauti ingawa uongozi wao ulitajwa ni wa ‘mkono wa chuma’ hasa tafsiri hiyo ikitoka kwa nchi za Magharibi na Ulaya, kwa kile kinachoelezwa ni kuminya demokrasia na haki za binadamu.
Uchambuzi wa BBC, unaaeleza kwamba Rais Assad wa Syria, aliondolewa wiki hii na waasi na kukimbilia uhamishoni, ameingia kwenye orodha ya viongozi mashuhuri wa nchi za Kiarabu, waliopinduliwa tangu kuanza kwa maandamano katika nchi za kiarabu yapata mwongo mmoja nyuma.
Hadi mwishoni mwa mwaka 2010, wengi wa viongozi hao wa nchi za Kiarabu, hawakuwahi kufikiria kwamba wangekumbana na mzozo ambao ungeziangusha serikali zao.
Nchi za Kiarabu za Mashariki ya Kati na Kaskazini mwa Afrika, zilitikiswa na dhoruba ya mabadiliko ambayo yaling'oa viongozi ambao hapo awali walidhaniwa kuwa hawawezi kushindwa.
Mwenendo huo, umeendelea hadi kiongozi wa mwisho ambaye aliondolewa madarakani na dhoruba ya mabadiliko, Rais wa Syria, Bashar al-Assad.
TUNISIA
Rais wa zamani wa Tunisia, Zine al-Abidine Ben Ali, alikuwa kiongozi wa kwanza wa nchi ya Kiarabu ambaye serikali yake ilipinduliwa baada ya dhoruba ya mapinduzi wa kiraia.Zine al-Abidine Ben Ali, aliitawala Tunisia kwa miaka 23, alikimbia na familia yake hadi Saudi Arabia Januari 2011, baada ya maandamano ya mwezi mzima dhidi ya serikali yake, ambayo yalichochea wimbi la mapinduzi katika nchi za Kiarabu.
Waandamanaji hao waliishutumu serikali yake kwa kushindwa kutoa ajira kwa raia wengi wa nchi hiyo hasa vijana na kuwashutumu maafisa wa serikali kwa ufisadi.
Maandamano hayo yalizuka baada ya kijana mmoja kujichoma moto baada ya kudhulumiwa na polisi Desemba 17, 2010.
Mohamed Bouazizi alifariki Januari 4, 2011, lakini kujitoa kwake kulisambaa kwenye mitandao ya kijamii, na hivyo kuzua ghasia za umma zilizompindua Zine El Abidine Ben Ali.
MISRI
Hosni Mubarak alitawala Misri kwa miaka 30 kabla ya maasi ya nchi za Kiarabu. Mabadiliko ya serikali nchini Tunisia yalichochea kuondolewa Mubarak, nchini Misri
Mubarak alijiuzulu baada ya wiki kadhaa za maandamano dhidi ya serikali yake, yaliyoanza Januari 25 katika uwanja wa Tahrir mjini Al Khahira.Waandamanaji hao waliishutumu serikali yake kwa kushindwa kutatua tatizo la ukosefu wa ajira, ongezeko la umaskini na kukithiri kwa rushwa.
YEMEN
Ali Abdullah Saleh, alikumbwa na hilo, baada ya miezi kadhaa ya maandamano yaliyopindua serikali za nchi za Kiarabu, dhoruba hiyo ilifika nchini mwake.Baada ya miezi kadhaa ya upinzani kati ya wananchi na serikali, Rais Sale alikubali kung'atuka madarakani.
Sale alikubali kukabidhi madaraka kwa makamu wake, Abd-Rabbu Mansour Hadi, baada ya maandamano ya ghasia yaliyosababisha shambulio la bomu kwenye ikulu ya rais.
Aliondoka madarakani Novemba 23, 2011, baada ya kupona majeraha aliyoyapata wakati wa shambulio la bomu kwenye Ikulu yake na shinikizo kutoka ndani na nje ya nchi.
LIBYA
Muammar Gaddafi naye alifikiwa. Wimbi la mabadiliko liliifikia Libya, liliipindua serikali ya kiongozi wake aliyekaa madarakani kwa muda mrefu zaidi, Muammar Gaddafi, baada ya kuwa mamlakani katika nchi hiyo kwa miaka 42.
Gaddafi alikuwa kiongozi wa kwanza kuuawa, baada ya wimbi la kupinduliwa kwa tawala katika nchi za Kiarabu.
Gaddafi aliingia madarakani Septemba 1969, baada ya mapinduzi ya ghafla na kumuangusha Mfalme Idris anayeungwa mkono na Uingereza.
Wakati akiwa madarakani, Gaddafi alishutumiwa kuwaunga mkono waasi katika nchi nyingine na moja ya mambo aliyojizolea umaarufu nayo ni kuhusika kwake katika kulipua ndege ya Pan Am katika anga ya Lockerbie, Scotland, Desemba 1988.
Shambulio hilo liliua abiria wote 259 waliokuwa ndani ya ndege hiyo, 190 kati yao walikuwa Wamarekani.
Maandamano dhidi ya serikali yake yaligeuka kuwa vita vya wenyewe kwa wenyewe, vikosi vya serikali na waasi vilipigana kwa muda wa miezi minane.
Oktoba 20, 2011, wapiganaji waasi walitangaza kifo cha Gaddafi, ambaye walisema aliuawa katika mji alikozaliwa, Sirte. Aliuawa akiwa na umri wa miaka 69.
Hata hivyo, wapo wanaomwona kuwa ni mtu aliyejaribu kuunganisha bara la Afrika. Katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwaka 2009, Gaddafi alitoa hotuba kwa zaidi ya saa moja, jambo ambalo lilikuwa kinyume na kanuni.
Aliikosoa mfumo wa kura ya turufu ya viti vya nchi tano katika baraza ya Umoja wa Mataifa na kutaka mfumo huo ufutwe. Kisha akakosoa vikali hatua ya Marekani kuvamia nchini ya Iraq.
SYRIA
Rais wa hivi karibuni zaidi ambaye serikali yake ni Bashar al-Assad, baada ya kundi la waasi kuongoza maasi dhidi ya serikali yake Jumapili, Desemba 8, 2024.Familia ya Assad imeitawala Syria kwa miaka 53. Rais Bashar al-Assad alichukua madaraka mwaka 2000, baada ya babake kutawala kwa miaka 30.
Miaka 13 iliyopita, alitumia nguvu kuwakandamiza waandamanaji na kisha kukawa na vita vya wenyewe kwa wenyewe. Zaidi ya watu nusu milioni wameuawa na wengine milioni 12 wamelazimika kukimbia makazi yao.
Lakini Jumatano wiki iliyopita, kundi la Kiislamu, Hayat Tahrir al-Sham (HTS), lilifanikiwa kufanya mashambulizi mabaya kaskazini magharibi mwa nchi hiyo, baada ya kushirikiana na makundi mengine ya waasi.
Waasi hao waliuteka mji wa pili kwa ukubwa nchini Syria, Aleppo na kuelekea kusini hadi mji mkuu, Damascus, ambako walizidi nguvu jeshi la Syria.
Russia, baadaye ilitangaza kuwa Assad na familia yake wamepewa hifadhi ya kisiasa huko Moscow.
KWA MSAADA WA MTANDAO
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED