NAOMBA kuanza makala ya leo kwa nukuu kutoka kwa Rais Samia Suluhu Hassan aliyosema: "Mabadiliko katika sheria zetu za uchaguzi yataleta ushindani wa haki na kuwapa watu fursa ya kuwachagua wawatakao kuwaongoza,”
Hii ni nukuu ya Rais Samia katika andiko lake la miaka 30 ya Vyama Vingi nchini Tanzania. Maneno hayo ni makubwa sana na yenye maana kubwa kwa sababu yanahusu kuwapa watu fursa ya kuwachagua wawatakao.
Uhuru wa watu kuwachagua viongozi wanaowataka ndiyo haki ya tatu ndani ya katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1977. Haki kuu ya kwanza ni haki ya uraia, ya pili ni haki ya kuishi na ya tatu ni ya kuchagua na kuchaguliwa kama ilivyoainishwa katika Ibara ya 5 na Ibara ya 21 ya katiba hiyo.
Haki hii ina sharti moja tu la umri wa miaka 18 kupiga kura, umri wa miaka 21 kuchaguliwa diwani au mbunge na miaka 40 kuchaguliwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungabno wa Tanzania (JMT).
Hakuna sharti la kulazimishwa kuwa mwanachama wa chama cha siasa. Kilichofanyika kuchomekea sharti la mgombea kudhaminiwa na chama cha siasa. Ndani ya Katiba yetu ni uhuni na ubatili tu uliofanyika na Mahakama Kuu iliisha ubatilisha ubatili huo.
Kiongozi yeyote anapoandika au anapohutubia, kuna mambo mawili kwenye andiko lake au hotuba yake. Mosi, kati ya andiko la kiongozi kuna vitu ni maono, mawazo, maneno na maandishi ambayo yeye mwenyewe kutoka moyoni mwake, kichwani mwake, mawazoni mwake, yaani ni yeye mwenyewe halisi.
Pili, viongozi wana wasaidizi ambao huwa wanawaandikia nini cha kusema (talking notes) na kwa Rais wa nchi, ana wasaidizi hotuba ambao wanamwandalia nini cha kusema kwa kumwandikia, kisha Rais anapitia kile alichoandikiwa lakini si chake. Anaweza kuongeza chake au kupunguza na ndipo anakuja kuhutubia au kutoa andiko.
Wakati akihutubia, tukisikia kila Rais anachosema kwenye hotuba yake, tunahesabu kila kilichosemwa ni Rais kusema. Msikilizaji huwezi kujua kipi ni chake mwenyewe na kipi ni ameandikiwa tuu lakini si chake.
Hii pia hutokea kwa wasomaji wa habari kwenye TV zote na redio zote. Watazamaji na wasikilizaji wanamwona mtangazaji na wanamsikiliza mtangazaji. Wanajua hizo habari wametangaziwa na mtangazaji fulani, wanajua ni mtangazaji huyo ndiye anajua habari hizo, kumbe hawajui kazi ya mtangazaji wa habari ni kutangaza tu habari alizoandikiwa na wengine. Yeye kazi yake ni kusoma tu.
Vivyo hivyo kwenye hotuba za viongozi, kuna viongozi wanasoma tu hotuba walizoandikiwa na wengine lakini si mawazo yao, si maneno yaov lakini ni matamshi yao.
Kama nilivyosema kwenye habari, mtangazaji unaandikiwa kisha unapewa kuipitia habari hiyo. Kwa Radio Tanzania (RTD) taarifa ya habari ni dakika 10, mtangazaji unatakiwa kuipitia nusu saa kabla, ili uielewe na unaposoma, unasoma kitu unachokijua.
Kitendo cha kuichukua habari ambayo hujaiandika, ukaipitia na kuisoma kama vile umeiandika wewe kinaitwa ‘presence’ kwa lugha ya Kiingereza. Ndiyo maana watangazaji huitwa ‘presenters’, kazi yao ni ku-present tu.
Kuna wakati msomaji wa habari unapitia habari usiyoielewa, unapaswa uulize, ili usisome kitu usichokielewa. Lakini katika mitikasi hii na ile, kuna siku mtangazaji unakuwa umechelewa kupitia Habari kabla, hivyo unasoma tu kwa uzoefu, hata ukikutana na kitu usichokielewa, unakisoma hivyo hivyo kilivyoandikwa na wasikilizaji na watazamaji watasikia tu na kuelewa.
Lakini kwa watu makini na kitu kinachoitwa ‘graphology’, wao watam- note mtangazaji anajiumauma ulimi, hivyo unajua tuu huyu mtu hajapitia hiyo habari, hivyo anasoma kwa uzoefu tu. Anasoma kitu asichokijua, anasema kitu alichoandikiwa lakini hakijui.
Vivyo hivyo hutokea kwenye baadhi ya hotuba za viongozi. Anakuwa ameandikiwa kitu asichokijua. Anapitia hotuba, kisha anahutubia kitu asichokijua.
Maneno hayo ya Rais Samia kwenye andiko lake ni maneno makubwa, mazito sana na mimi nikayaandikia makala kwenye safu yangu gazeti za Jumapili ya Julai 10, 2022 yanye kichwa cha habari , "Rais Samia Akitekeleza Hili, Hakika Tanzania Itabarikiwa".
Sasa sheria mpya ya uchaguzi imeshatungwa ila sheria bado ina ubatili ule ule tunaoupigia kelele. Hali hiyo inayonifanya kuanza kujiuliza hivi maneno haya "Mabadiliko katika sheria zetu za uchaguzi, yataleta ushindani wa haki na kuwapa watu fursa ya kuwachagua wawatakao kuwaongoza?”
Je, ni maneno ya Rais Samia mwenyewe au aliandikiwa? Je, hii sheria mpya ya uchaguzi, yenye ubatili ule ule, italeta vipi ushindani wa haki wakati Rais Samia ameahidi "kuwapa watu fursa ya kuwachagua wawatakao kuwaongoza”
wakati sheria mpya ya uchaguzi, watu bado hawana haki ya kuwachagua viongozi wanaowataka, bali wanalazimishwa kuwachagua viongozi waliopitishwa na vyama vya siasa na si viongozi wanaowataka?
Tafsiri ya alichokisema Rais Samia na kilicholetwa kwenye sheria mpya ya uchaguzi ni vitu viwili tofauti. Kwa sababu muda bado tunao, nashauri hili liangaliwe ili sheria yetu ya uchaguzi iwe ya haki kweli kama Ibara ya 5 na 21 za katiba zinavyosema.
Wasalaam
Paskali
+255 754 270403
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED