Sheria yoyote kinyume cha Katiba ni batili

By Pascal Mayala , Nipashe Jumapili
Published at 11:56 AM Jul 28 2024
Nyundo ya Mahakama.
Picha:Mtandao
Nyundo ya Mahakama.

LEO naendelea na makala elimishi za kuwafundisha Watanzania kuijua Katiba, sheria na haki. Je, wajua kuwa japo mhimili wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (JMT) ndio wenye mamlaka ya kutunga sheria haliwezi kutunga sheria kinyume cha Katiba.

Pamoja na mamlaka hayo, Bunge halina mamlaka ya kutunga sheria batili au kinyume cha Katiba kwa sababu Katiba inalizuia. Kutokana na ukweli huo, swali la kujiuliza ni kwamba je, Bunge letu limepata wapi mamlaka ya kutunga sheria batili na kwa kutumia kifungu gani? 

Si tu Bunge limetunga sheria batili, bali limeuchukua ubatili huo na  kuuchomekea kiubatili  ndani ya Katiba yetu, hivyo kuibatilisha Katiba yetu kuwa katiba yenye ubatili!. Sasa Bunge limetunga tena sheria batili ya uchaguzi na ubatili ule ule uliokwishabatilishwa na Mahakama Kuu na  kumpa Rais aitie saini kuanza kutumika. Kwa nini Bunge letu litutendee hivi? 

Kwa kuanzia, kwanza tulijue Bunge ni nini na majukumu yake ni yapi. Ibara ya 62 (1) ya katiba inasema: “Kutakuwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano ambalo litakuwa na sehemu mbili, yaani Rais na Wabunge.

Bunge la JMT  ni moja ya mihimili mitatu ya dola, yaani Serikali, Bunge na Mahakama.  Japo mhimili wa serikali ndio unaonekana kuwa ndio kila kitu kwa sababu mkuu wa mhilmili huo ni Rais wa JMT, ndie Mkuu wa Serikali na Amiri Jeshi Mkuu, hali inayofanya serikali kuonekana kama ndio mhimili uliojichimbia chini zaidi lakini kwa mujibu wa katiba yetu na kwenye majukumu ya Bunge,

Kifungu cha pili cha ibara hiyo kinasema Bunge litakuwa ndicho chombo kikuu cha Jamhuri ya Muungano (hivyo Bunge ni kuu kuliko serikali, kuliko mahakama) ambalo linapata ukuu wake na madaraka yake kutoka kwa wananchi na linatakiwa kufanya kazi zake kwa niaba ya wananchi.

Moja ya kazi kuu za Bunge ni kuisimamia na kuishauri Serikali ya Jamhuri ya Muungano na vyombo vyake vyote ukiwamo mhimili wa Mahakama, katika utekelezaji wa majukumu yake kwa mujibu wa Katiba hii, hivyo kikatiba Bunge ndicho kila kitu,si serikali, si mahakama!.

Kifungu cha (3) kinasema Kwa madhumuni ya utekelezaji wa madaraka yake Bunge laweza-

(a)      Kumuuliza Waziri yeyote swali lolote kuhusu mambo ya umma katika Jamhuri ya Muungano ambayo yako katika wajibu wake;

(b)     Kujadili utekelezaji wa kila Wizara wakati wa Mkutano wa Bunge wa kila mwaka wa bajeti;

(c)      Kujadili na kuidhinisha mpango wowote wa muda mfupi, muda wa kati au muda mrefu unaokusudiwa kutekelezwa katika Jamhuri ya Muungano, na kutunga sheria ya kusimamia utekelezaji wa mpango huo.  

(d)     Kutunga sheria pale ambapo utekelezaji unahitaji kuwapo sheria;

(e)      Kujadili na kuridhia mikataba yote inayohusu Jamhuri ya Muungano na ambayo kwa masharti yake inahitaji kuridhiwa.

64.-(1) Mamlaka yote ya kutunga sheria juu ya mambo mengine yote yahusuyo Tanzania Bara, yatakuwa mikononi mwa Bunge. Katiba hii itakuwa na nguvu ya sheria katika Jamhuri nzima ya Muungano na endapo sheria nyingine yoyote itakiuka masharti yaliyomo katika Katiba hii, ndiyo itakuwa na nguvu, na sheria hiyo nyingine, kwa kiasi inachokiuka Katiba itakuwa batili.

Hii Ibara ya 64  (5) ndiyo inayosisitiza ukuu wa Katiba kuwa ina nguvu ya sheria kuliko chombo chochote. Katiba  ina nguvu kuliko Bunge, ina nguvu kuliko serikali, ina nguvu kuliko mahakama, katiba ndiyo kila kitu.

Pia ni ibara hii, ndiyo imeipa katiba mamlaka ya juu kuliko mahakama ya kubatilisha sheria yoyote endapo itakiuka masharti yaliyomo katika Katiba.  Katiba ndiyo itakuwa na nguvu na sheria hiyo nyingine kwa kiasi inachokiuka Katiba itakuwa batili. Ibara hii maana yake ni kwamba Bunge halina mamlaka ya kutunga sheria yoyote inayokwenda kinyume cha katiba.

Hukumu ya Mahakama Kuu, katika kesi ya Mchungaji Christopher Mtikila, imezitangaza Ibara ya 39 na 63 za Katiba ya JMT  ni batili, na zimechomekewa kwenye katiba kiubatili.

Mahakama Kuu umetamka kuwa katika pingamizi ya serikali kwa hukumu hiyo kwenye Mahakama ya Rufani, Hukumu ya Mahakama ya Rufani haikubatilisha hukumu ya Mahakama Kuu kuhusu ubatili wa vifungu hivyo kwenda kinyume cha katiba bali imejikita kwenye uwezo wa mahakama kuliingilia Bunge katika utungaji wa sheria.

Kwa hiyo Mahakama ya Rufani ikajitoa kuwa mahakama si “the custodian of the will of the people”, “the custodian ni Bunge”, hivyo ikatoa uamuzi kuwa maadam ubatili huo umefanywa na Bunge, mahakama haiwezi kuliingilia Bunge katika utungaji wa sheria, hivyo Bunge ndilo likarejeshewa kuuondoa ubatili huo.

Kitendo ilichofanya Mahakama ya Rufani hapa ni kama mtu umeibiwa gari lako, ukashtaki polisi kuwa umeibiwa, kisha ukaliona gari lako, ukaripoti polisi umemkamata mwizi wako. Yule mwizi na ushahidi wa gari lako, akafikishwa mahakamani, mahakama ikatoa uamuzi kuwa ni kweli gari ni lako na mwizi ameliiba, na amekamatwa nalo lakini kwa vile mwizi huyu ni mtu anayeheshimika sana, mahakama imeamuru alirudishe gari alipoliiba. Yule mwizi hakulirudisha mpaka leo!

Bunge limetunga sheria batili kinyume cha katiba, mahakama ikatangaza sheria hiyo ni batili kwa sababu inakwenda kinyume na katiba. Bunge likafanya marekebisho ya katiba kwa hati ya dharura na kuuchomekea huo ubatili ndani ya katiba kwenye Ibara ya  39 na 63 ili kuuhalalisha ubatili huo. Mahakama Kuu ikaamuru kuwa huo uchomekeaji ni batili, ibara hizo ni kinyume cha  katiba. Mahakama ya Rufani ukaliamuru Bunge, kuuondoa ubatili huo ndani ya katiba yetu na kuifuta sheria batili ile!. Kwanini mpaka leo Bunge halijatekeleza hukumu ile ya Mahakama? Na  kama haitoshi, Bunge letu tukufu, likatunga sheria mpya ya uchaguzi yenye ubatili ule ule. Hii maana yake ni nini?

Tukutane Juma lijalo.

Pascal Mayalla

·         Mwandishi ni Mwanasheria na Wakili wa Kujitegemea anapatikana kwa namba 0754270403. Baruapepe [email protected]