KARIBU tena msomaji wangu tuendelee na vipengele vingine vyanzo vya matatizo ya ndoa nyingi. Hii ni sehemu ya tatu na ya mwisho katika eneo hilo.
Tayari nimejadili vyanzo kadhaa labda kwa faida ya wale ambao hawakubahatika kusoma safu hii nao wapate mwanga kidogo. Nilitaja ndoa zilizofanyika pasipo Mungu kuhusika(wakati ulikuwa adui wa Mungu).
Kingine ndoa kwa sababu ya kupata mimba kwa bahati mbaya, kujihusisha kimapenzi kabla ya ndoa, ndoa zilizofungwa baada ya mtu kwenda kwa mganga wa kienyeji, ndoa zilizofungwa kwa shinikizo la wazazi.
Chanzo kingine kulawitiwa/kubakwa wakati wa udogo, ndoa ambazo wahusika waliwahi kufanya agano la damu na mtu mwingine (Agano la Amini). Pia ndoa zilizojengwa katika misingi ya bora kuolewa/kuoa kuliko kuishi hivi hivi.
Msomaji wangu, leo tumalizie vyanzo vingine nilivyoweza kukuandalia kwenye safu yetu hii ya Maisha Ndivyo Yalivyo. Kipo chanzo ndoa zilizojengwa katika misingi ya muonekano wa nje. Muonekano wa nje hauwezi kukufanya uwe na ndoa ya kudumu.
Mara zote uzuri wa mtu hupotea kadiri siku zinavyoaidi kwenda mbele. Wanawake wengi wana tabia ya kusema, ‘bado natafuta mwanaume, awe mzuri, mrefu. Na kama mwanaume hana mwonekano mzuri siwezi kukubali anioe”.
Sawa, unaweza kutafuta warembo wa kila namna, lakini ujue kwamba uzuri/mwonekano wa nje hupotea baada ya muda fulani. Utakapopotea, ndipo chanzo cha matatizo ya ndoa huanza.
Chanzo kingine ni ndoa zilizojengwa katika misingi ya mali. Kama ndoa yako imejengwa katika misingi ya mali, haitaweza kudumu. Ni vizuri kuishi maisha mazuri, lakini utajiri na mali ni vitu vya kupita. Hutaweza kujenga msingi wa ndoa yako katika mali!
Kama kuna wanawake wa kuwahurumia, ni wale wanaozunguka na kutangaza, “mtu atakayenioa anatakiwa awe mtu tajiri, awe na angalau magari mawili, awe na akaunti kama sita hizi za benki.
Siwezi kuolewa na mtu anayeishi nyumba ya kupanga. Lazima awe na uwezo wa kusafiri nchi za nje kwa ajili ya kufurahia. Sitaki mateso! Tamaa za namna hii zitakufanya ujikute unaingia katika makosa makubwa sana.
Pia wapo vijana wa kiume ambao hutafuta wanawake wenye uwezo wa magari, kazi nzuri. Wanapoona wanawake wa aina hii huanza maombi. Baada ya siku chache huja na maono kuwa wameoneshwa.
Kwa kutokujali hujikuta wameoa wanawake ambao watawafanya wasiwe na hatma nzuri ya maisha yao. Mara nyingi wanawake wa aina hiyo wanakuwa ni wale waliokata tamaa ya kusubiri kuolewa.
Hivyo, kijana yoyote atakayekuja mbele yao ni hiari yao. Hawa hujikuta wameingia katika kifungo pasipo wao kufahamu.
Ndoa zilizojengwa katika misingi ya unabii wa kishetani. Ninapoongelea unabii wa kishetani haimaanishi kutembelea waganga wa kienyeji, au wapiga ramli.
Hapa ninamaanisha kuna watu ambao wanahudhuria kwenye majengo ya manabii wa uwongo ambao hujifanya malaika wa nuru ili waue hatma za vijana.
Wao hupenda kusema, “bwana amesema, utakapokuwa unakwenda utakutana na mke wako chini ya mti kesho, umfuate huyo ndiye mke wako ambaye bwana amekuchagulia”.
Hapo mtu atachanganyikiwa; maana hatafahamu ni mti upi anatakiwa kukutana na huyo mke/mume atakayefunga naye ndoa; na hivi ndivyo watu wengi wamejikuta wakioa mabomu.
Ni kweli watumishi wa Mungu wana sehemu ya kukushauri juu ya mwanamke/mwanaume unayetaka kufunga naye ndoa. Lakini unatakiwa kuwa makini maana nyakati za leo wapo watu wanaojiita watumishi wa Mungu kumbe siyo. Unaweza kujikuta umeunganishwa na mtu asiye sahihi na hatma yako yote ikapindishwa!
Ndoa zilizojengwa katika misingi ya kumilikishwa mke/mume katika umri mdogo. Ni kitendo kinachofanyika sana katika baadhi ya nchi za Afrika.
Wazazi humposa/humtoa binti yao akiwa na umri mdogo sana miaka 13 au 15 kuolewa na mtu tajiri katika jamii hiyo, au humpa mtemi. Binti huyo hutunzwa na kulelewa katika nyumba ya mumewe mpaka atakapokua.
Msingi wa mwisho kwa leo ni ndoa za mitala/wake wengi. Wanawake wengi hujikuta wameingia katika ndoa za wake wengi kwa kusukumwa. Baada ya muda wanatafuta njia kujinasua katika ndoa hiyo.
Je, una maoni, kisa? Ujumbe 0715268581. Namba ipo pia WhatsApp.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED