ZIKIBAKI siku 11 kabla ya Sikukuu ya Krismasi, bei za vyakula na bidhaa zimeendelea kupaa katika masoko maeneo mbalimbali nchini.
Uchunguzi uliofanywa na Nipashe, umebaini kuwa kilo moja ya maharage kwa sasa imepanda hadi Sh. 4,000 wakati awali iliuzwa Sh. 3,500 na nyama ya ng’ombe kilo imefikia Sh. 12,000 wakati awali iliuzwa kati ya Sh. 9,000 hadi Sh. 10,000 kulingana na eneo husika.
Kuku wa kisasa ambaye alikuwa akiuzwa Sh. 8,000 amefikia Sh. 11,000 na wale wa kienyeji wanauzwa hadi Sh. 30,000 wakati bei ya awali ilikuwa Sh. 20,000 hadi Sh. 25,000.
MIKOA YA KASKAZINI
Katika miji ya Bomang’ombe na Machame, baadhi ya maeneo ya Sanya Juu, Moshi Mjini (Kilimanjaro) na Arusha Mjini, kilo moja ya nyama ya ng’ombe inauzwa kwa Sh. 12,000 kwa sasa wakati awali ilikuwa Sh. 10,000.
Akizungumza na Nipashe, Joseph Laitayo, mfanyabiashara wa nyama katika mji wa Bomang’ombe, wilayani Hai, alisema nyama ya ng’ombe imepanda tangu Septemba, mwaka huu, kutokana na kupanda kwa bei ya ng’ombe mnadani.
Alisema nyama ya steki ambayo huuzwa tofauti na mchanganyiko wa nyama wa kawaida, inauzwa kwa Sh. 14, 000 kwa kilo katika baadhi ya maeneo kwenye wilaya za Hai, Moshi na Arusha.
Wakati mbuzi mmoja wa ‘ndafu’ ambayo ni maarufu kwa ajili ya shughuli mbalimbali za kifamilia, bei ya mnadani ni kati ya Sh. 250,000 hadi 300,000 kulingana na ukubwa wa mbuzi.
Wananchi mkoani Manyara, wamesema bei za vyakula muhimu, haitishi kwa kuwa bado havijapanda.
Mkazi wa Mtaa wa Komoto, Edina Charles, alisema kwa sasa wananunua kilo moja ya sukari Sh .2, 700 huku bei ya mchele ikiwa ni Sh. 2,000 mpaka Sh.2,800 kwa kilo.
Muuzaji wa vyakula vya nafaka, Ally Hamis, alisema maeneo mengi mchele unakolimwa kwa sasa wakulima ndio wanapanda, hivyo kusababisha upatikanaji wake kupungua
SINGIDA
Katika soko kuu la Singida, Ginery, Misufini, Kibaoni, Mahambe, Minga na soko la Unyankindi, bei za vyakula zimeongezeka, hivyo kuzua malalamiko kwa wananchi na wafanyabiashara wenyewe.
Vyakula vilivyopanda bei ni pamoja na viazi mviringo ambavyo vilikuwa vinauzwa kwa Sh. 90,000 kwa gunia la ujazo wa kilo 100 lakini hivi sasa linauzwa kati ya Sh. 105,000 na Sh. 110,000.
Mkungu mmoja wa ndizi (ndizi Bukoba) ambao ulikuwa unauzwa kati ya Sh. 25,000 na 27,000 hivi sasa unapatikana kwa Sh. 33,000 hadi 35,000.
Maharage ya njano ambayo yalikuwa yanauzwa kwa Sh. 2,500 hadi 3,000 kwa kilo lakini hivi sasa katika masoko hayo, yanauzwa kwa Sh. 3,500 hadi 4,000 kwa kilo huku mchele supa kwa kilo unauzwa Sh. 4,000 kutoka Sh.3,500.
Kuhusu matunda, bei ya embe ya jumla ilikuwa ikiuzwa kwa Sh. 200 lakini sasa inauzwa kwa Sh.350 wakati limau moja linauzwa kwa Sh. 500 hadi Sh. 700.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wananchi na wafanyabiashara katika masoko hayo, walisema bei hizo za vyakula zilianza kupanda baada ya msimu wa masika kuanza.
Mwenyekiti wa Soko Kuu la Singida, Hassan Mboroo, alisema wafanyabiashara wanaoleta vyakula katika masoko wamepandisha bei za vyakula wakidai ni kutokana na changamoto ya usafiri iliyosababishwa na mvua nyingi kunyesha na kuharibu miundombinu.
Mfanyabiashara wa ndizi, Robert Kiato, alisema bei hizo za vyakula zinaweza kupanda zaidi kadri mvua zinavyoendelea kunyesha, huku changamoto ya kusafirisha vyakula kwenda kwenye masoko ikizidi kuwa kubwa.
DODOMA MOTO
Katika soko kuu la Majengo jijini Dododma, bei ya kilo ya nyama imepanda kutoka Sh. 8,000 mwezi uliopita hadi kufikia Sh. 11,000 kwa sasa na kilo ya mchele ambayo ilikuwa Sh. 1,600 kwa sasa inauzwa Sh. 3,000.
Bidhaa zingine zilizopanda ni unga wa sembe kutoka Sh. 1,000 kwa kilo hadi kufikia 1,500, maharage kilo ni Sh. 3,600 kutoka Sh. 3,000 na mafuta ya kupikia lita moja Sh. 5,000 kutoka Sh. 4,500.
Bei ya samaki aina ya sato imepanda ambapo kilo moja imefikia Sh. 14,000 kutoka Sh. 12,000 huku samaki aina ya sangara aliyekuwa akiuzwa Sh. 10,000 kwa sasa ni Sh. 12,000.
Salum Abubakar alisema hali ya bei ya vyakula jijini humo hivi sasa imeendelea kupanda na kuzitaka mamlaka husika kuingilia kati kudhibiti hali hiyo.
Alisema hali hiyo isipoangaliwa mapema inaweza kuwa mbaya zaidi hasa itakapofikia mwezi Januari na Februari wakati mvua za masika zitakapokuwa zimekolea.
Akizungumza na gazeti hili muuza bucha la nyama eneo la Kikuyu Hassan Maliseli, alisema sababu za kupanda kwa bei hiyo kunatokana na upatikanaji adimu wa ng'ombe katika baadhi ya machinjio, lakini pia inahusisha kupanda huko na msimu wa sikikuu.
Nipashe imeshuhudia katika soko la majengo, Dodoma, sado moja linauzwa Sh. 7,000 badala ya Sh. 3,500, huku ndoo ya lita 20 vinauzwa Sh. 22,000 badala ya Sh. 18,000 ya awali.
Muuzaji wa vitunguu sokoni hapo, Aisha Selemani, alisema upatikanaji wa bidhaa hiyo kutoka kwa wakulima umekuwa changamoto, hali inayochangia bei kuongezeka.
Erick Moses, muuzaji wa mayai ya jumla, alisema trei mayai imepanda kutoka Sh. 8000 kwa bei ya jumla mpaka Sh. 10,000 na kwa wauzaji wa rejareja inauzwa Sh. 12,000, huku yai moja likiuzwa Sh. 400 badala ya Sh. 300.
Alisema kupanda kwa bei ya mayai kunatokana na msimu wa sikukuu lakini pia, walanguzi wa bidhaa hiyo wamekuwa wengi na kusababisha wafugaji kushindwa kumudu soko la wateja.
HALI DAR ES SALAAM
Mfanyabiashara wa mchele na maharage kwa bei ya jumla katika Soko la Tandale, Kassim Said, alisema mwezi Novemba na Desemba, bei za mazao hayo hupanda kwa sababu wakulima huyaficha wakisubiri msimu wa mvua uanze.
Alisema maharage yanayotoka mkoani Tanga wanauziwa na wakulima kwa Sh. 2,900 kwa kilo na wao huuza Sh. 3,300 na yakifika madukani yanauzwa Sh. 3,800.
Mfanyabiashara wa nyanya kwa bei ya jumla Soko la Mabibo , Ramadhani Seif, alisema walilazimika kupandisha bei ya matenga ya nyanya kutoka Sh.35,000 hadi Sh.50,000 kwa sababu wakulima wanawauzia Sh.25,000 hadi Sh. 35,000, kulingana na ubora wa nyanya zilizoko kwenye tenga.
Mfanyabiashara wa vitunguu katika soko la Mabibo, Charles Michael, alisema kwa sasa wananunua gunia la vitunguu kwa wakulima wa mkoani Njombe, kwa Sh. 100,000 kutoka Sh. 50,000, hivyo kulazimika kuuza bei ya jumla ya Sh. 180,000 kutoka Sh. 100,000.
Amina Juma, mkazi wa Sinza, alisema kwa sasa kitunguu kimoja kinauzwa kati ya Sh. 500 hadi 600.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED