NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko, amesema serikali itaendelea kushirikiana na sekta binafsi, hususan shule binafsi ili kuboresha sekta ya elimu nchini.
Akizungumza katika Mkutano Mkuu wa Chama cha Wamiliki wa Shule Binafsi Tanzania (TAPIE) jana jijini Dar es Salaam, Dk. Biteko alisema serikali haiwezi kuacha wadau wa elimu wakilalamika kwa kuwa uwapo wao unaisaidia serikali.
“Nataka niwahakikishie serikali imeendelea kukutana na TAPIE mara kwa mara na hapa namwelekeza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu, Jenista Mhagama, kuratibu mkutano wa pamoja kati ya TAPIE na Wizara za Ardhi, Fedha, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) ili kujadiliana kwa pamoja na kupata suluhu ya changamoto zinazowakabili,” amesema.
Dk. Biteko pia ameitaka TAPIE kuzingatia masharti yaliyoainishwa katika barua na vyeti vya usajili wa asasi zao kwa kuwa kuna baadhi hukiuka masharti, hivyo kusababisha migongano isiyo ya lazima na mamlaka zilizokasimiwa kusimamia sheria,
kanuni, taratibu na miongozo ya uendeshaji wa asasi za elimu.
Pia ameitaka kufuata sheria na kanuni za utoaji elimu, kuhimiza na kuimarisha maadili, nidhamu na malezi bora kwa watumishi na wanafunzi walio chini ya asasi zao.
Amesema suala la uadilifu katika shughuli za uendeshaji na usimamizi wa mitihani ya kitaifa lisisitizwe na kutiliwa mkazo ili kupata wataalam wenye sifa stahiki.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, alizipongeza shule binafsi kwa kufanya uwekezaji mkubwa
ambao sasa unavutia baadhi ya wanafunzi kutoka nchi zingine kusoma nchini.
“Tunapozungumza kuwa tunaenda na elimu ya miaka 10 tunaamini sekta binafsi ina msaada mkubwa katika hili kwa sasa. Tutaanza na ujenzi wa shule 100 za sekondari za ufundi na ni imani yangu kuwa tutashirikiana vizuri na sekta binafsi”, amesisitiza.
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Elimu, Utamaduni na Michezo, Husna Sekiboko, amesema serikali imeweka mazingira wezeshi katika sekta binafsi na sasa kuna zaidi ya shule 500.
“Tunaipongeza sekta binafsi kwa kutoa ajira na Bunge tunatambua mchango wa TAPIE. Tutawaunga mkono katika
kuboresha sekta hii ya elimu.
“Kuhusu leseni ya kuanzisha shule, Kamati yangu inaungana na TAPIE tunaomba Serikali izungumze na wadau ili kusaidia kupiga hatua ya utekelezaji wa mitaala iliyowekwa,” amesema.
Pia ameitaka TAPIE kulinda mikataba ya watumishi walio chini ya taasisi zao ikiwa ni pamoja na kuwasilisha michango yao katika mifuko ya hifadhi ya jamii.
Rais wa TAPIE, Mahmoud Mringo, amesema chama hicho kinalenga kuisaidia serikali kwa kuwa na uwekezaji unaoleta tija katika sekta ya elimu nchini na hivyo kuiomba kuendelea kusaidia katika utatuzi wa changamoto zinazowakabili.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED