Hii ndiyo dawa ya kero za Muungano, ubaguzi

By Pascal Mayala , Nipashe Jumapili
Published at 09:14 AM May 26 2024
 Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Picha: Maktaba
Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

KWA wasomaji wapya, wiki iliyopita nilizungumzia kuhusu kauli za kibaguzi za kunyoosheana vidole vya Utanganyika na Uzanzibari kwamba zinasababishwa na ukosefu wa elimu ya uraia. Katika mwendelezo huo, niliahidi leo kumalizia mjadala huu kwa kuangazia chanzo cha ubaguzi huu na suluhisho la kudumu.

Baada ya Muungano, kwa miongo kadhaa, tumekuwa na Muungano wenye maelewano mazuri licha ya kuwapo kwa changamoto kadhaa kwenye kero za Muungano. Hata hivyo, moto wa Utanganyika na Uzanzibari, uliwashwa na kitendo cha Zanzibar kujiunga na Umoja wa Nchi za Kiislamu (OIC), wakati Tanzania imejinasibu ni nchi isiyo na dini. 

Wabunge 55 wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (JMT), kutokana na kukiukwa huko kwa Katiba waliunda  kundi la G-55 na kuidai serikali ya Tanganyika, ili iendelee kuwa haina dini na kuiruhusu serikali ya Zanzibar kuendelea kuwa mwanachama wa OIC.  

Bunge lilipitisha Azimio la kuanzisha serikali ya Tanganyika, jambo ambalo lilimwibua Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, kuwakemea wabunge kwa Bunge kukaa kama kamati ya Chama na kuwaeleza mfumo wa serikali tatu si sera ya Chama Cha Mapinduzi (CCM). Hiyo ilisababisha hoja hiyo ya kuundwa serikali ya Tanganyika,kufa kifo cha mende na kuzikwa jumla.  

Zanzibar nayo ililazimishwa kujitoa OIC na kuahidiwa serikali ya JMT itajiunga na OIC, kitu ambacho hakikufanyika mpaka leo. Toka wakati huo, wahafidhina wa Zanzibar wakawa na dukuduku la chini chini kuwa Zanzibar haikutendewa haki, hivyo wakaanza vuguvugu za kudai Zanzibar yenye mamlaka zaidi. 

Kabla ya hapo, aliyekuwa Rais wa Zanzibar, Aboud Jumbe, alipewa ushauri wa kisheria na aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, Wolfgang Dourado, wakaandaa hati za kisheria kudai Zanzibar yenye mamlaka kamili, taarifa zikafika kunakohusika. Aboud Jumbe akaitwa Dodoma, akaenda kama Rais wa Zanzibar, akarejea kama rais mstaafu na kusindikizwa nyumbani kwake, Mji Mwema mpaka Mungu alipomuita. Dourado  aliwekwa mahali salama, taarifa iliyotolewa ilisema kumetokea kuchafuka kwa hali ya  hewa ya kisiasa Zanzibar kulikosababisha Jumbe kujiuzulu urais wa Zanzibar. 

Baada ya Rais Nyerere kutoka Bara, alifuatiwa na Rais Ali Hassan Mwinyi kutoka Zanzibar, baadaye akaja Benjamin Mkapa kutoka Bara, akitarajiwa anafuatiwa na rais kutoka Zanzibar. Hali haikuwa hivyo, akaingia Rais Jakaya Kikwete, Wazanzibari wakajiona wamesetwa, wakakoleza hoja ya Uzanzibari. Baada  ya Rais Kikwete alifuatia  Rais John Magufuli kutoka Bara tena, Uzanzibari ukazidi kukolezwa. 

Yaliyotokea Machi 17, 2021 kwa Rais wa JMT kuwa ni Samia Suluhu Hassan kutoka Zanzibar, hoja za Utanganyika zikaanza kuibuliwa tena na wanasiasa mufilisi kuanza tena ubaguzi wa kunyoosheana vidole vya Utanganyika na Uzanzibari. 

TANU NA ASP

Vyama vilivyopigania Uhuru na ukombozi wa Tanganyika na Zanzibar, TANU na Afro Shiraz Party (ASP) vilipoungana mwaka 1977, si wengi katika Tanzania ya sasa walikuwa  wamezaliwa. Wengi  wamezaliwa, wameikuta CCM, hivyo hawajui kwa nini TANU na ASP viliungana, na viliungana ili iweje?

 Mimi nimezaliwa miaka ya 1960, hivyo TANU na ASP zilipoungana, nilikuwa darasa la tatu, kijijini Itonjanda, nikikaa kwa bibi mzaa Baba, Bibi Wakawombwe (Mungu aiweke roho yake mahali pema peponi) baada ya Baba Mzee Mayalla (RIP) kuhusika na yale mambo fulani ya Mwanza mwaka 1976.

 Sababu ya TANU na ASP kuungana ni kuelekea kwenye serikali moja!. Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere, alisema huu muungano wa vyama vya TANU na ASP na kuzaliwa chama kipya, CCM, ni mwanzo wa safari ya kuondoka kwenye serikali mbili, kuelekea kwenye serikali moja. Je, ndoto hii ya Mwalimu Nyerere kwa Tanzania kuwa nchi moja ya JMT yenye serikali moja na rais mmoja, itakuja kutimia?

 Watanzania wanahitaji sana kuelimishwa kuhusu huu muungano wetu adimu na adhimu. Tena  ni Rais Samia, kiongozi wa kwanza wa juu aliyetoa ruhusa watu waachwe huru kujadili Muungano. Baada ya Muungano, nchi zote mbili zilitoweka, hakuna nchi ya Tanganyika wala Zanzibar, bali Tanzania ni nchi moja ya JMT yenye sehemu mbili, Tanzania Bara iliyokuwa Tanganyika na Tanzania Visiwani au Tanzania Zanzibar iliyokuwa Zanzibar.

 MKANGANYIKO WA KATIBA


 Kama nilivyosema kimataifa Tanzania ni nchi moja ya JMT, hakuna mkanganyiko wowote wa kimataifa kuhusu Tanzania.  hata hivyo, kitaifa kuna mkanganyiko wa katiba kati ya katiba ya JMT na katiba ya Zanzibar.


 Kwa mujibu wa katiba ya JMT ya mwaka 1977, Tanzania ni nchi moja ya JMT yenye sehemu mbili, Tanzania Bara na Tanzania Visiwani au Tanzania Zanzibar. Zanzibar si nchi bali ni sehemu ya JMT yenye utawala wake wa ndani.

 Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, inaiita Zanzibar ni nchi, moja ya nchi mbili zinazounda JMT!. Kitendo cha katiba ya Zanzibar kuiita Zanzibar ni nchi, kinawakanganya Watanzania kudhani kuwa nchi ya Tanganyika ndiyo pekee iliyokufa lakini Zanzibar ipo na haikufa.

 Naomba niwahakikishie Tanzania ni nchi moja ya JMT. Ile  nchi inayotajwa na katiba ya Zanzibar, yaani Zanzibar, sii kweli kuwa ni nchi, bali ni jina tu. Hayo  mabadiliko ya katiba ya Zanzibar kujiita nchi, kimuungano ni mabadiko batili lakini kwa vile mabadiliko hayo ni kwa ajili ya Zanzibar tu na hayatambuliwi na katiba ya JMT, serikali ya JMT, imeamua kuyapuuza. Lakini  kutokana na hizi kelele, tutapuuza mpaka lini? Si bora twende kwenye serikali moja haya yote yaishe?.

 Kwa vile Rais Samia anakwenda kutupatia katiba mpya, nashauri hili la mkanganyika wa katiba kati ya katiba ya JMT na Katiba ya Zanzibar, pia lirekebishwe na kwa maoni yangu, dawa pekee ya uhakika na ya kudumu ambayo ni mwarobaini wa kuzimaliza kero zote za Muungano, ni kwenda kwenye serikali moja.  

Nimalizie na hili swali, je, Tanzania sasa tumefika wakati wa kutimiza ndoto ya Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere ya uzalendo wa kweli wa JMT wa kwenda kwenye nchi moja, yenye serikali moja na rais mmoja? 

Wasalaam.

Pascal Mayalla

+255 754 270403