Yanga yajipanga kumaliza kazi ugenini

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 10:34 AM Sep 12 2024
Ofisa Habari wa Klabu hiyo, Ali Kamwe
Picha:Mtandao
Ofisa Habari wa Klabu hiyo, Ali Kamwe

KIKOSI cha Yanga kimeondoka nchini alfajiri ya kuamkia jana kwenda Ethiopia tayari kwa mchezo wao wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya CBE huku Kocha Miguel Gamondi akipanga kumaliza kazi ugenini.

Gamondi, alisema amekiandaa kikosi chake kuhakikisha wanapata matokeo mazuri kwenye mchezo huo wa ugenini ili kutokuwa na kazi kubwa kwenye mchezo wa marudiano.

"Tumejiandaa vizuri, nataka wachezaji watumie vizuri kila nafasi ili kazi tuimalize huko huko kwao ingawa nafahamu mchezo hautakuwa mwepesi," alisema Gamondi.

Alisema wanaenda kwenye mchezo huo wakiwa na hali ya kupambana na hawatakuwa na presha yoyote.

Katika hatua nyingine, Ofisa Habari wa Klabu hiyo, Ali Kamwe, amesema baadhi ya wachezaji ambao wako kwenye vikosi vya timu mbalimbali za taifa, wataungana na wenzao baada ya kumaliza kuzitumika timu zao katika michezo wa kusaka tiketi ya kufuzu kucheza AFCON mwakani nchini Morocco.

Alisema katika safari yao watatumia kiasi cha saa tatu au nne kabla ya kufika nchini Ethiopia kwa kuwa hawatounganisha ndege yoyote.

"Kikosi chetu kimetoa wachezaji 14 kwenye timu mbalimbali za taifa, hao wote wataungana na timu Ethiopia wakitokea kwenye majukumu yao, tunaenda Ethiopia tukiwa na matumaini makubwa," alisema Kamwe.

Alisema Yanga imekuwa na maandalizi mazuri licha ya kutokuwa na nusu ya wachezaji wake lakini hilo halijawasumbua.

Yanga ilibakiwa na wachezaji 11 tu kambini, kati ya 27 ambao iliwasajili kwani wachezaji 14 walikuwa wamekwenda kuzitumikia timu zao za taifa na kubakiwa na  wachezaji 13 lakini wawili kati ya hao, Yao Kouassi na Farid Mussa ni majeruhi.

Yanga iliingia raundi ya kwanza kwa kuitoa Vital'O ya Burundi kwa jumla ya mabao 10-0, ikishinda mabao 4-0 mechi ya kwanza na 6-0, mechi ya marudiano, michezo yote ikipigwa Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.

Mshindi wa jumla kati ya Yanga dhidi ya CBE, atatinga hatua ya makundi ya ligi hiyo kubwa barani Afrika.