Yanga kumaliza kazi mbele ya Vital O

By Shufaa Lyimo , Nipashe
Published at 07:55 AM Aug 24 2024
KOCHA wa Klabu ya Yanga, Miguel Gamondi.
Picha: Mtandao
KOCHA wa Klabu ya Yanga, Miguel Gamondi.

KOCHA wa Klabu ya Yanga, Miguel Gamondi, amesema licha ya kuwa mbele kwa mabao 4-0 dhidi ya wapinzani wao wa leo, Vital O ya Burundi kwenye mchezo wa mzunguko wa pili hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, bado kazi yao haijaisha mpaka baada ya dakika 90.

Yanga walipata ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya wapinzani wao hao kwenye mchezo wa kwanza wiki iliyopita uliochezwa kwenye uwanja wa Azam Complex na leo wanarudiana kwenye uwanja huo.

Gamondi, alisema licha ya kuwa mbele kwa ushindi huo, bado hawatawadharau wapinzani wao hao katika mchezo wa leo utakaochezwa saa 1:00 usiku.

"Huwa sipendi kusikiliza mpinzani anawaza au kuongea nini mara nyingi natumia muda wangu kuandaa timu yangu kuwa bora, timu yangu ina wachezaji  bora hivyo sina wasiwasi na mchezo huo, lakini lazima tuchukue tahadhari na kutowadharau wapinzani wetu licha ya kuwa mbele,” alisema Gamondi. 

Alisema ana matumaini makubwa na wachezaji wake kutokana na mbinu alizowapa ili kujilinda na kushambulia dhidi ya wapinzani wao hao ambao anaamini watarudi na nguvu mpya. 

“Bado mchezo hatujamaliza, kuna dakika 90 nyingine, tutakuwa makini sana kwenye kumaliza mchezo huu, tupo tayari kwa mchezo,” alisema Gamondi.

Aidha, golikipa, Abutwalib Mshery ambaye alizungumza kwa niaba ya wachezaji wenzake alisema wamefanya maandalizi ya kutosha na kwa kufuata maelekezo waliyopewa na kocha wao katika uwanja wa mazoezi. 

“Hatuwadharau wapinzani wetu kwa sababu tutumeshinda mechi ya kwanza, mchezo wa leo tutaingia kama tunaanza upya mashindano haya lakini pia hamasa ya goli la Mama (Rais Samia)inaongeza chachu ya kufanya vizuri zaidi,” alisema Mshery.

Kwa upande wake  kocha wa Vital’ O, Sahabo Parris aliesema mechi ya kwanza waliku wawanaitizama na kuangalia namna ya kuwafunga Yanga na walicheza vizuri lakini haikuwa bahati kwao.

Alisema anaimani kubwa na timu yake kufanya vizuri na kuweza kuwapa ushindani mkubwa Yanga zaidi  ya mechi iliyopita.

“Ninaimani kubwa na wachezaji wangu, tumejiandaavizurinaushindiupo, tunaweza kurudisha mabao manne, huu ni mpira na lolote linaweza kutokea,” alisema Parris. 

Nahodha  wa timu hiyo, Ndayishimiyie Hussein, alisema mchezo uliopita walifungwa na wapinzani wao kwa kuwa hawakutumia vizuri nafasi zao.

Alisema wamejipanga na wamefanyia kazi mapungufu yao na wapo tayari kutoa ushindani mbele ya Yanga leo.

Katika hatua nyingine, kikosi cha Azam FC nacho leo kinaingia uwanjani jijini Kigali, Rwanda kwa ajili ya mchezo wa marudiano dhidiya APR ya nchini humo.

Azam wanaingia uwanjani wakiwa mbele kwa bao 1-0 kufuatia ushindi walioupata katika mchezo wa kwanza uliochezwa wiki iliyopita kwenye uwanja wa Azam Complex.

Kikosi hicho cha ‘Wanarambaramba’ hao wanahitaji ushindi wowote au matokeo ya sare kuweza kusonga mbele kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa wa Afrika.