WACHEZAJI wa Simba wamesema huu ni wakati mzuri kwao kuandika historia mpya kwenye soka la klabu hiyo na Tanzania kwa ujumla kwa kuwaondoa mashindanoni Mabingwa wa Afrika, Al Ahly ya Misri na wao kutinga hatua ya nusu fainali.
Akizungumza kwa niaba ya wachezaji wenzake kipa wa timu hiyo, Ali Salim, amesema wamekaa kikao wao kwa wao na kuambizana kuwa safari hii hakuna cha kuwazuia kwenda nusu fainali kama watapambana, kwani kiwango chao kwa sasa kinafanana kabisa na timu kubwa barani Afrika.
Salim amesema kikao chao kama wachezaji kilifanyika mara baada ya droo kufanyika, hivyo kwa sasa wanachosubiria ni siku ya mechi tu ili waonyeshe kile ambacho waliahidiana kukifanya.
"Naongea kwa niaba yao kuwa tunafanya mazoezi vizuri na tunapata muda wa kupumzika vizuri, timu tunayocheza nayo ni kubwa Afrika, tumeshawahi kucheza nayo mara kwa mara japo hatujawahi kufanya vizuri sana, kocha kasema tuje huku ili tuweze kufanya vizuri kwenye mechi inayokuja na sisi tuna imani hiyo.
"Baada ya droo kufanyika, kila mchezaji alionekana kuwa na imani ya kusonga mbele, na sisi wenyewe tukakutana na tukaambizana kuwa timu zilizoingia zote ni za levo yetu, hata hawa Al Ahly kwetu si wa kuwahofia kivile hapo wenzetu wamtupita kidogo," amesema Salim.
Amesema anaamini kuwa robo fainali ngumu zaidi waliowahi kucheza ni dhidi ya Kaizer Chiefs iliyochezwa Mei 15, 2021 waliyofungwa mabao 4-0 nchini Afrika Kusini, kabla ya kushinda mabao 3-0 Mei 22, mwaka huo jijini Dar es Salaam.
"Robo fainali ile ngumu sana, tulijisahau tukaruhusu mabao mengi ugenini, tukawa na mlima mrefu nyumbani, lakini hata maandalizi naamini hayakuwa mazuri kama tunavyojiandaa hivi sasa.
Ile ya TP Mazembe tuliyotoa sare na kufungwa mabao 4-1 ugenini tulitolewa kwa sababu ya ugeni tu wa mashindano, kipindi kile hatukuwa na utayari sana," amesema kipa huyo.
Kipa huyo amesema robo fainali iliyokuwa rahisi zaidi kwao ilikuwa ya msimu uliopita dhidi ya Wydad Casablanca, lakini makosa machache tu yaliwagharimu.
"Mechi na Wydad Casablanca kilichotufelisha ni kutoimaliza nyumbani, tungepata hata bao moja na nusu tu, achilia mbali mawili tulikuwa tunavuka, kule tulikaza wakapata moja, hatimaye mikwaju ya penalti ikaamua," amesema.
Aprili 29, 2023, Simba ilitolewa kwa penalti 4-3, baada ya timu hizo kushinda bao 1-0 nyumbani kila mmoja.
Wakati huo huo kikosi cha timu hiyo kinatarajia kurejea jijini Dar es Salaam kesho tayari kwa kuwavaa mabingwa wao.
Meneja Habari na Mawasiliano, Ahmed Ally, amesema maandalizi kuelekea mchezo huo yamekwenda kama yalivyopangwa.
"Mazingira ya kambi huwa yanatoa ujumbe kwa wachezaji, walivyoona tumekwenda Zanzibar hata wao wakaona kuwa hii mechi si ya kawaida, wamesema wako tayari kwenda kuipania Simba na wanafurahishwa na maandalizi yanayofanyika," amesema Ahmed.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED