Simba yavutwa sharubu nyumbani

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 07:31 AM Oct 05 2024
news
PICHA: JUMANNE JUMA
Kipa wa Coastal Union, Levy Matamp (kushoto), akiwahi kudaka mpira dhidi ya beki wa kati wa Simba, Abdulrazak Hamza (aliyeruka juu), katika mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara iliyochezwa kwenye Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam jana.

IKITOKA nyuma, Coastal Union ilifanikiwa kurudisha mabao yote mawili iliyoruhusu kipindi cha kwanza na kulazimisha sare ya mabao 2-2 dhidi ya Simba katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliochezwa kwenye Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam jana.

Wafungaji wa mabao hayo, Hassan Abdallah na Ernest Malonga, walikuwa wamemsoma kipa wa Simba, Moussa Camara, mwenye tabia ya kuacha lango lake mbali na kupachika mabao mepesi katika mechi hiyo na kugawana pointi.

Wakiwa nyuma kwa mabao 2-0, Hassan, aliupata mpira akiwa nje ya eneo la hatari, akapiga mpira wa juu uliokwenda moja kwa moja wavuni na kumwacha Camara asijue la kufanya.

Dakika ya 71, Malonga naye alifunga bao la pili baada ya Coastal Union kufanya shambulio la kushtukiza, kwa mguu wa kushoto alipiga juu, ukampita Camara na kujaa wavuni.

Baada ya mabao hayo, ndipo wachezaji wa Simba walionekana kushtuka wapo kwenye mechi na si mazoezi kama walivyokuwa wakifanya awali.

Haikucheza kwa kasi wala kiwango kilichozoeleka, wachezaji wakipiga pasi nyingi bila sababu yoyote, hawakutengeneza nafasi kama ilivyo kawaida, ikionekana kabisa waliingia wakidhani wanacheza na timu dhaifu.

Kipindi cha kwanza ilipata nafasi nyingi za kufunga, lakini wachezaji wake hawakuwa makini kuzitumia.

Ni sare ya kwanza kwa Simba baada ya michezo minne ya ushindi, huku Camara akiruhusu nyavu zake kutikiswa pia kwa mara ya kwanza.

Sare hiyo inaifanya Simba kupanda hadi nafasi ya pili na ikifikisha pointi 13 huku ikiishusha Fountain Gate iliyokuwa kwenye nafasi hiyo kutokana na kuwa na uwiano mzuri wa mabao ya kufunga na kufungwa.

Pamoja na sare hiyo, bado Coastal Union inasalia nafasi ya 13 licha ya kufikisha pointi tano, imepata sare ya pili katika Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu.

Mechi ilianza taratibu kila timu ikionekana kusoma mchezo wa mwenzake, na ikicheza kwa dakika 15 bila ya kila upande kufanya shaambulizi lolote la maana langoni.

Coastal Union ilikuwa na mpango mkakati wa kukaa nyuma ya kuwaachia Simba mpira ambao walikuwa wakifanya kazi ya kuifungua ngome ya Wagosi wa Kaya.

Baada ya magolikipa wote kuwa likizo, hatimaye dakika ya 15, Jean Charles Ahoua, alimwamsha, Matampi, baada ya shuti lake kutoka nje kidogo ya lango.

Alimegewa pande nje kidogo ya eneo la hatari na Debora Fernandes, kabla ya kupiga shuti hilo lililomshughulisha kipa huyo kwa kuruka, lakini mpira ulitoka nje ya lango.

Simba ilifanikiwa kuandika bao la kwanza dakika ya 25 baada ya kufanya shambulizi ambalo hakuna aliyetarajia kuwa lingezaa bao.

Beki wa kulia, Shomari Kapombe, alitoka na mpira kwenye wingi ya kulia akiwa amepewa pasi na Joshua Mutale, akaupiga ndani ya lango ukamkuta tena winga huyo wa Mzambia ambaye aliupiga mpira wa juu, Matampi aliruka juu na kuudaka, lakini alipofika chini ulimponyoka mbele ya Leonel Ateba na Mohamed Hussein 'Zimbwe Jr', ambaye aliukwamisha wavuni na kuandika bao la kwanza katika mchezo huo.

Pamoja na kufunga bao hilo, Coastal Union bado hawakushawishika kuondoka langoni mwao, badala yake waliendelea kujaza wachezaji wengi, lakini wakishambulia kwa kushtukiza, mashambulizi ambayo hayakuwa na hatari sana kwa wapinzani wao.

Dakika 14 baadaye, straika raia wa Cameroon, Ateba alifunga bao lake la pili msimu huu, pia kwenye mchezo huo kwa penalti baada ya beki, Abdallah Denis 'Viva', kuunawa ndani ya eneo la hatari kutokana na harakati za kuokoa hatari hiyo.

Mabadiliko ya timu zote ya kipindi cha pili yaliisaidia zaidi Coastal Union badala ya Simba.