Simba yaitisha Coastal Union

By Somoe Ng'itu ,, Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 07:30 AM Oct 04 2024
Kocha Mkuu wa Simba, Fadlu Davids.
Picha:Mtandao
Kocha Mkuu wa Simba, Fadlu Davids.

USHINDI mnono ndio matarajio ya Kocha Mkuu wa Simba, Fadlu Davids, kuelekea mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Coastal Union kutoka jijini Tanga utakaochezwa leo kwenye Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam.

 Hata hivyo Kaimu Kocha Mkuu wa Coastal Union, Joseph Lazaro, amesema endapo watatumia udhaifu wa Simba, timu hiyo inafungika.

Akizungumza na gazeti hili jana, Fadlu alisema ameendelea kulifanyia kazi suala la kukosa nafasi za wazi kwa wachezaji wake, na anaamini wakitumia vizuri nafasi watakazo zitengeneza watapata ushindi mnono katika mechi hiyo itakayochezwa kuanzia saa 10:15 jioni.

"Nimelifanyia kazi suala ya kukosa nafasi, utakumbuka Leonel Ateba katika mchezo uliopita dhidi ya Dodoma Jiji alikosa mabao kama mawili akiwa ndani ya boksi, ni kweli katika mchezo wa mpira wa miguu huwezi kupata kila nafasi na huwezi kushinda mabao matatu au manne kila mchezo, lakini tutajitahidi tuwe tunatumia vizuri nafasi zinazopatikana," Fadlu, raia wa Afrika Kusini alisema.

Kocha huyo alisema ana wasiwasi wapinzani wao wanaweza kuingia na mfumo wa kupaki basi, hivyo tayari ametengeneza mpango mkakati wa kuhakikisha wanafungua mianya.

"Kama wapinzani wetu watakuja na mfumo wa kuzuia, basi tunajaribu kuwalazimisha kuachia mianya, lakini pia na sisi inabidi tuwe makini kwa sababu wapinzani wetu ni wazuri wanapokuwa na mpira.

Tunaiheshimu Coastal Union, tuliiona ikicheza kwenye mechi za Ngao ya Jamii, ikacheza michezo miwili ya kimataifa ya Kombe la Shirikisho, kwa sasa imeonekana kuimarika kwa hiyo itakuwa na mechi ngumu, lakini tumejipanga kutimiza malengo yetu," alisema Fadlu.

Naye Lazaro aliliambia gazeti hili katika mchezo huo, kila timu inahitaji kupata matokeo chanya, lakini wao wanayahitaji zaidi.

Lazaro alisema anawafahamu vyema wapinzani wao na wamejiandaa kuwadhibiti ili kuhakikisha wanavuna pointi katika mchezo huo.

"Kila mtu anahitaji matokeo, lakini sisi tunahitaji zaidi kwa sababu nafasi tuliyopo si rafiki, tunajua tunacheza na timu gani, wakoje, tucheze nao vipi, kwa sababu ni timu ambayo mchezaji mmoja tu anaweza kuamua matokeo, na wanao (wachezaji), kama watatu hivi," Lazaro alisema.

Aliongeza Simba pia ina udhaifu wake na endapo watautumia vyema, wanauwezo wa kupata ushindi.

"Pamoja na mazuri, wao pia wana udhaifu na wanafungika," alimaliza beki wa kushoto wa zamani wa timu hiyo.

Simba haijafungwa mchezo wowote wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Coastal Union tangu Ligi Kuu msimu wa 2019/2020, ikiwa imecheza michezo 12, ikishinda michezo 10 na sare mbili.

Msimu huu Wekundu wa Msimbazi wamecheza michezo minne, wameshinda yote, ikikusanya pointi 12 na mabao 10 kibindoni huku haijaruhusu nyavu zake kutikiswa wakati Coastal Union walioshuka dimbani mara sita, wameshinda mechi moja, sare moja na kupoteza minne, ikiwa na pointi nne.

Wakati huo huo, Singida Black Stars imetamba itaondoka na ushindi katika mechi yake ya leo dhidi ya Mashujaa FC ingawa wanaamini mchezo huo utakuwa mgumu na wenye upinzani.

Kocha Msaidizi wa Singida Black Stars, Dennis Kitambi, alisema jana anatambua ugumu wa mchezo huo na kuahidi licha ya kucheza ugenini lakini watapata ushindi.

"Tunafahamu Mashujaa ni timu ngumu ambayo hairuhusu magoli kirahisi, nimeandaa vizuri wachezaji wangu kuhakikisha tunapata matokeo mazuri katika mchezo wetu huo," alisema Kitambi.

Mechi nyingine ya ligi hiyo itakayochezwa leo kwenye Uwanja wa CCM Sokoine jijini Mbeya itakuwa ni kati ya wenyeji KenGold dhidi ya JKT Tanzania.