Simba SC yatamba kutembeza vichapo

By Somoe Ng'itu , Nipashe
Published at 07:25 AM Sep 07 2024
Wachezaji wa Simba wakifurahia moja ya goli katika mchezo wao.
Picha: Mtandao
Wachezaji wa Simba wakifurahia moja ya goli katika mchezo wao.

WAKATI inatarajia kushuka dimbani leo kucheza mechi ya kirafiki dhidi ya JKT Tanzania, uongozi wa Simba umesema hawatarudia makosa yaliyojitokeza misimu mitatu iliyopita.

Simba imeshindwa kutwaa taji la Ligi Kuu Tanzania Bara ambalo kwa misimu mitatu mfululizo limechukuliwa na wapinzani wao Yanga.

Akizungumza na gazeti hili jana, Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, alisema kikosi chao kinaendelea kuimarika, hivyo wanatarajia kupata matokeo mazuri katika kila mechi watakayocheza.

Ahmed alisema wanatarajia watawapa furaha mashabiki wao kwa kufanya vyema katika mashindano yote watakayoshiriki na hii inatokana na usajili mzuri uliofanywa.

"Ikikamilika Ubaya Ubwela, iko full pakti, ni mateso, hii Simba sio ya kawaida, hii Simba tumewekeza, na mwaka huu tumedhamiria Ubaya Ubwela," Ahmed alisema.

Aliongeza wanawaomba radhi mashabiki wao kwa kutoruhusu watazamaji katika mechi ya leo ambayo inachezwa ndani ya Kalenda ya FIFA.

Alimtaja mchezaji ambaye ni majeruhi katika kikosi chao ni golikipa, Ayoub Lakred huku akiongeza kiungo mshambuliaji, Fabrice Ngoma, amerudi kikosini baada kurudi nchini akitokea nyumbani kwao Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, kutokana na matatizo ya kifamilia.

"Mchezo huo utachezwa milango ikiwa imefungwa, kwa sasa mechi ambazo zinatakiwa kuwa na mashabiki ni zile zilizoko katika Kalenda ya FIFA tu, kwa hiyo mashabiki wetu waelewe hilo," Ahmed alisema.

Aliongeza katika mechi hiyo kocha anataka kuona wachezaji wake wakicheza bila presha yoyote na ndio sababu ya kuamua kujipima dhidi ya Maafande hao wa JKT Tanzania.

Simba inatarajia kutumia mechi hiyo ya pili ya kirafiki kwa ajili ya kujiandaana mchezo wa raundi ya kwanza ya mashindano ya kimataifa ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Al Ahly Tripoli, utakachezwa ugenini Septemba 15, mwaka huu na marudiano yakitarajiwa kufanyika hapa nchini baada ya wiki moja.