Simba Queens, Yanga dimbani tena Novemba

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 07:38 AM Oct 04 2024
   Simba Queens, Yanga   dimbani tena Novemba
Picha:Mtandao
Simba Queens, Yanga dimbani tena Novemba

WATANI wa jadi nchini, Simba Queens na Yanga Princess watakutana katika mechi ya mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania itakayochezwa Novemba 13, mwaka huu kwenye Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam.

Timu hizo zitarudiana katika mchezo wa mzunguko wa pili utakaofanyika Machi 4,  mwakani kwenye uwanja huo huo.

Yanga Princess itashuka dimbani katika mechi hiyo ikiwa na kumbukumbu ya kupata ushindi wa kwanza wa penalti 4-3 ambao wameupata kwenye mechi ya hatua ya nusu fainali ya pili ya michuano ya Ngao ya Jamii iliyochezwa juzi jijini.

Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), mabingwa watetezi, Simba Queens watafungua pazia la msimu mpya wa 2024/2025 kwa kuwakaribisha Mlandizi Queens mechi itakayochezwa Oktoba 9, mwaka huu kwenye Uwanja wa KMC Complex wakati Yanga Princess itaanzia ugenini dhidi ya Bunda Queens siku hiyo hiyo.

Alliance Girls watakuwa nyumbani kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza kuwakaribisha JKT Queens wakati Gets Program ya Dodoma itawafuata Mashujaa Queens (zamani Amani Queens), kwenye Uwanja wa Isamuhyo, Dar es Salaam na Fountain Gate Princess itakuwa na kibarua dhidi ya Ceasiaa kutoka mkoani Iringa.

Ligi hiyo inayoshirikisha timu 10 imepangwa kumalizika Mei 6, mwakani kwa Fountain Gate Princess kuwavaa Mlandizi Queeen, Mashujaa Queens yenyewe itapambana na Bunda Queens huku JKT Queens itawafuata Gets Program, Alliance Girls itapapatuana na Simba Queens huku Yanga Princess ikiwaalika Ceasiaa kwenye Uwanja wa KMC Complex.

Simba Queens ilitwaa ubingwa wa ligi hiyo msimu uliopita bila kufungwa, pia ikishinda Ngao ya Jamii kwa kuwafunga JKT Queens kwenye mchezo wa fainali.

Bingwa wa ligi hiyo atapata nafasi ya kuiwakilisha Tanzania Bara katika mashindano ya kimataifa ya Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), yanayofanyika kila mwaka.

Wakati huo huo, Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu cha Wanawake Tanzania (TWFA), Somoe Ng'itu, amewapongeza wadau wa soka waliojitokeza katika mechi za hatua ya nusu fainali ya Ngao ya Jamii zilizofanyika juzi.

"Tunawashukuru kwa kujitokeza kushangilia timu zao, tunawaahidi msimu mpya utakuwa na ushindani zaidi, kwa sababu kila timu imejipanga na imejiandaa vyema," Somoe alisema.