Simba, Al Hilal kujiuliza

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 07:06 AM Aug 31 2024
Kocha Mkuu wa Simba, Fadlu Davids
Picha: Mtandao
Kocha Mkuu wa Simba, Fadlu Davids

HAKUNA kulala, ndio kinachoonekana kwa wawakilishi wa Tanzania Katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika, Simba ambao wanatarajia kuikaribisha Al Hilal ya Sudan katika mechi ya kirafiki ya kimataifa itakayochezwa leo kwenye Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam.

Hata hivyo, katika mchezo wa leo, Simba huenda ikamtambulisha straika wake mpya, Leonel Ateba, ambaye alikuwa nyota wa mwisho wa kimataifa kusajiliwa.

Ateba, hajaonekana katika michezo miwili ya Ligi Kuu Tanzania Bara ambayo Wekundu wa Msimbazi wamecheza dhidi ya Tabora United na Fountain Gate kutokana na kukosekana kwa vibali.

Kocha Mkuu wa Simba, Fadlu Davids, amewaambia mashabiki wa timu hiyo leo itakuwa ni nafasi nzuri kumwona mchezaji huyo kwa mara ya kwanza kwa sababu atamtumia, huku pia akiendelea kumpa nafasi straika wa Mtanzania, Velentino Mashaka, ameshapachika mabao mawili.

Fadlu alisema Mashaka ameanza kumpa mwangaza mzuri na anaamini ataendelea kuwa 'moto'.

"Ateba kesho (leo) ndiyo atakayeongoza mashambulizi kwa sababu nataka nimwone kwa uzuri zaidi katika mchezo mkubwa kama huu, nadhani na mashabiki nao watapata fursa ya kumwona baada ya kukosekana mara mbili, lakini pia kuna Valentino, naye atapata nafasi, ni kijana mzuri ambaye katika mechi zote mbili amefunga bao moja akitokea benchi. Mukwala naye itategemea kama akichelewa kwenda katika  kikosi cha taifa atacheza, lakini kama akiondoka mapema hatakuwepo," alisema Fadlu.

Aliongeza pia atatumia mechi hiyo kuwapa nafasi wachezaji wengine ambao hawakutumika kabisa kwenye mechi mbili za Ligi Kuu walizocheza ili wawe na utimamu wa mwili vizuri.

Simba itaanza kutupa karata yake katika mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika ugenini Septemba 13, mwaka huu dhidi ya Al Ahly Tripoli huku mchezo wa marudiano utafanyika wiki moja baadaye kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.