Ramovic atamba Yanga kuimarika

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 09:51 AM Dec 21 2024
Sead Ramovic.
Picha:Mtandao
Sead Ramovic.

BAADA ya ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Mashujaa FC iliyoupata juzi kwenye Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam, Kocha Mkuu wa Yanga, Sead Ramovic, ametamba kuwa kikosi chake sasa kimeanza kuimarika, akiongeza kuwa siku kadhaa baadaye kitarudi kama kilivyokuwa huko nyuma, huku straika Prince Dube akifunguka 'hat-trick' ya kwanza katika Ligi Kuu.

Akizungumza baada ya mchezo huo, Ramovic alisema anawapongeza wachezaji wake kwa kupambana kuhakikisha timu inapata ushindi katika mchezo mgumu uliokuwa na matukio ya kushangaza.

"Nawapongeza pia wapinzani wetu kwa kutupa mchezo mgumu, tulitawala sana kipindi cha kwanza, lakini mwisho wa mchezo mmeona ubao umesomeka mabao 3-2, ilikuwa ni mechi ngumu kama tulivyoitarajia, lakini kwa yote haya naona sasa kikosi kimeanza kuimarika taratibu ingawa bado hakijawa kwenye ubora unaotakiwa," alisema.

Kocha huyo alibainisha pamoja na kutawala dakika 45 za mwanzo, lakini walikuwa bora zaidi kwa dakika 25 tu ambapo walicheza kwa kasi kubwa kiasi cha kufanikiwa kufunga mabao mawili, baadaye wachezaji wake walionekana kukata pumzi kutokana na kutokuwa na utimamu wa mwili kwa asilimia 100.

"Nafikiri tulikuwa bora sana dakika 25 za mwanzo na tukafunga mabao mawili, baada ya hapo mnaweza kuona tulihangaika na tatizo kubwa ni utimamu wa mwili, tulishuka kwa sababu tulicheza kwa kasi kubwa mwanzo, tunahitaji tuendelee kujiboresha kwenye eneo hilo, ila nimefurahishwa mno na kiwango cha wachezaji wangu, ikizingatia kuna safari za mara kwa mara ambazo zinachosha wachezaji," alisema kocha huyo raia wa Ujerumani.

Baada ya ushindi huo, Yanga imepanda kutoka nafasi ya nne hadi ya tatu ya msimamo ikiwa na pointi 30, nyuma ya Simba iliyo nafasi ya pili na pointi zake 31, huku Azam FC ikiwa kileleni na pointi zake 33.

Hata hivyo, Azam imemaliza mechi zake 15 za mzunguko wa kwanza, huku Simba na Yanga zikiwa zimecheza michezo 12 kila moja.

Katika mchezo wa juzi, ilipatikana 'hat-trick' ya kwanza kwenye Ligi Kuu, ikifungwa na straika Dube, aliyesajiliwa mwanzoni mwa msimu akitokea Azam.

Hadi anapata 'hat-trick' hiyo alikuwa hajafunga bao lolote kwenye ligi msimu huu, lakini alipachika mabao matatu, akiwa pia ni mchezaji bora wa mechi.

"Kilikuwa kipindi kigumu sana kwangu, lakini wanachama na mashabiki wa Yanga, viongozi na wachezaji walinionesha upendo, walinisapoti, kwa hiyo tuzo hii ya mchezaji bora pamoja na 'hat-trick' ni zawadi kwa Wanayanga wote, tumeshinda wote," alisema Dube.

Kocha Mkuu wa Mashujaa FC, Mohamed Abdallah 'Bares' alilalamikia safu yake ya ulinzi kufanya makosa mengi na kusababisha kufungwa mabao rahisi.

"Niwapongeze Yanga wamepata ushindi, kikubwa ni kwamba tumefanya makosa ambayo wao wameyatumia.

"Kama unacheza na timu ambayo unajua mkikosea tu wachezaji wake wanaweza kukuadhibu, basi unabidi ujichunge sana, hatukufanya hivyo, tumeadhibiwa.

"Mfano tulikuwa tunatafuta bao la kusawazisha ili matokeo yawe 2-2, lakini tukafungwa bao la tatu rahisi sana, inavunja moyo hata kwa wale ambao wanapambana mbele kutafuta mabao, tumeruhusu  mabao rahisi, hasa la tatu ni la kizembe sana, imeleta shida sana," alilalamika kocha huyo.

Baada ya kipigo hicho, Mashujaa inabaki na pointi zake 19, ikiwa imemaliza mechi zake za mzunguko wa kwanza ikiwa nafasi ya saba.