Pamba mechi 10 bila ushindi

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 11:02 AM Oct 30 2024
Nembo ya Timu ya Pamba Jiji.
Picha: Mtandao
Nembo ya Timu ya Pamba Jiji.

KOCHA mkongwe nchini, Juma Mgunda, ameanza na mguu mzuri kwenye kikosi cha Namungo kwa kupata ushindi wa kwanza tangu alipochukua mikoba ya kuifundisha timu hiyo huku akiiongezea Pamba Jiji FC rekodi yao mbaya ya kutoshinda kufikia mechi 10 hadi sasa msimu huu.

Katika mchezo huo uliopigwa juzi usiku kwenye Uwanja wa Majaliwa, Ruangwa mkoani Lindi na Namungo kushinda 1-0, bao hilo pekee lilifungwa na Ibrahim Mkoko dakika ya 12, na kuifanya timu hiyo kupata ushindi wa kwanza baada ya kupoteza mitatu mfululizo.

Mara ya mwisho kushinda ilikuwa ni Septemba 28, ilipoifunga Prisons bao 1-0, baada ya hapo ilichapwa 1-0 dhidi ya Azam, ikazabwa mabao 2-0 dhidi ya Singida Black Stars, kabla ya kukutana na kipigo cha mabao 3-0 dhidi ya Simba Ijumaa iliyopita.

Wakati ikisulubiwa na Simba kwenye Uwanja wa KMC, Mwenge, Dar es Salaam, Mgunda alikuwa amekaa jukwaani akishuhudia kwani ilikuwa ni siku moja tu tangu atangazwe kujiunga nayo.

Ushindi huo unaisogeza juu kidogo timu hiyo hadi nafasi ya 11, ikifikisha pointi tisa, ikicheza michezo tisa, ikishinda mitatu na kupoteza sita, ikiwa haijatoka sare hata mchezo mmoja.

Namungo na Yanga ndizo timu pekee kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara hazijaonja ladha ya sare.

Kipigo cha bao 1-0 ilichokipata Pamba Jiji kinaendeleza mlolongo wa matokeo mabovu ya timu hiyo tangu ilipopanda daraja msimu huu.

Ikiwa imeshacheza michezo 10, haijashinda hata mchezo mmoja ikiwa ni timu pekee ambayo haijaonja utamu wa ushindi kwenye Ligi Kuu, ikipoteza michezo mitano na sare tano.

Inakamata nafasi ya 15 kwenye msimamo wa Ligi Kuu wenye timu 16, ikiwa ina pointi tano tu mpaka sasa, ikiizidi KenGold inayoburuza mkia ikiwa na pointi moja tu mkononi hadi sasa.