Namungo yaipa jeuri KMC, yajipanga kuivuruga Simba

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 02:00 PM Nov 02 2024
Kocha Mkuu wa KMC, Abdihamid Moallin.
Picha:Mtandao
Kocha Mkuu wa KMC, Abdihamid Moallin.

BAADA ya kupata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Namungo katika mechi ya Ligi Kuu Bara iliyochezwa kwenye Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam juzi, Kocha Mkuu wa KMC, Abdihamid Moallin, ameitumia salamu Simba, akisema watakwenda kutoa ushindani watakapokutana keshokutwa.

Ushindi huo ni wa pili mfululizo kwa KMC baada ya pia kuifunga Prisons mabao 2-1, nyumbani kwake kwenye Uwanja wa CCM Sokoine jijini, Mbeya.

Akizungumza baada ya kumalizika kwa mchezo huo juzi, kocha huyo raia wa Somalia, alisema ushindi wa mechi mbili mfululizo unampa 'jeuri' ya kuamini watawapa 'tabu' Simba kutokana na  kikosi chake kuendelea kuimarika.

"Tulipata nafasi nyingi hatukuzitumia, lakini tumepata ushindi wa bao moja ni muhimu kwetu, tunashangalia, lakini tunakwenda kujiandaa na mchezo mwingine mkubwa dhidi ya Simba, inabidi tuwe tayari kukabiliana nao, nadhani kwa sasa kikosi changu kipo imara kupambana na timu yoyote, tunaamini tutafanya vizuri pia dhidi yao," alisema Moallin.

Bao ya KMC katika mechi hiyo lilifungwa dakika ya pili na Rashid Chambo, ambapo matokeo hao yamewapandisha Kino Boys hadi nafasi ya sita katika msimamo wa ligi ikifikisha pointi 14 baada ya kucheza michezo 10.

Naye Kocha Mkuu wa Namungo, Juma Mgunda, alisema kuzubaa kwa wachezaji wake na kutokuwa na utayari wa miili yao mwanzoni mwa mchezo huo kuliwafanya wapoteze mechi hiyo.

 "Tumefanya makosa ya kutokuwa na utayari katika dakika za mwanzoni, wenzetu wakatuadhibu, lakini hii ni changamoto kwangu lazima nirekebishe hili, naamini siku hadi siku kikosi kitazidi kubadilika.

Kwa sasa tunakwenda kujipanga ili kufanya vizuri zaidi katika mechi zinazokuja," alisema kocha huyo ambaye aliiongoza timu yake kushinda bao 1-0 dhidi ya Pamba Jiji.

Kipigo hicho kinaifanya Namungo kusalia na pointi tisa, ikiwa kwenye nafasi ya 12 ya msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.