Mfungaji bora wa Zanzibar aanza kuwatisha Aziz Ki, Fei Toto Ligi Kuu

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 10:08 AM Sep 17 2024
Mfungaji bora wa Zanzibar aanza  kuwatisha Aziz Ki, Fei Toto Ligi Kuu
Picha: Nipashe Digital
Mfungaji bora wa Zanzibar aanza kuwatisha Aziz Ki, Fei Toto Ligi Kuu

MFUNGAJI bora wa Ligi Kuu Zanzibar, Selemani Mwalimu, ameanza kuwa tishio kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara, akipachika mabao matatu katika mechi nne ambazo ameichezea timu yake ya Fountain Gate, akikaa juu ya kilele cha orodha ya wafungaji bora wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Juzi kwenye Uwanja wa Tanzanite Kwaraa, straika huyo alipachika bao moja, likiwa ni la tatu mfululizo kwake kwenye Ligi Kuu, akiisaidia timu yake kupata sare ya mabao 2-2 dhidi ya Dodoma Jiji FC.

"Nashukuru Mungu nimeanza vizuri Ligi ya Tanzania Bara, naamini nitafanya vema kama nilivyokuwa nikifanya Zanzibar, mimi kazi yangu ni kufunga, naomba tu nisipate majeraha, nitaendea kufunga," alisema mchezaji huyo aliyesajiliwa na Fountain Gate msimu huu akitokea KVZ ya Zanzibar.

Akiwa na timu hiyo Zanzibar aliibuka mshindi wa kiatu cha dhahabu akimaliza akiwa na mabao 20, na 'asisti' saba, jambo ambalo liliwavutia mabosi wa Fountain Gate.

Akiwa katika ligi mpya, hakufunga kwenye mechi ya kwanza dhidi ya Simba, Agosti 25, mwaka huu, timu yake ilipochapwa mabao 4-0, Uwanja wa KMC uliopo Mwenge, Dar es Salaam, lakini baada ya hapo alifunga bao moja kila mchezo.

Alifunga bao moja, Agosti 29, timu yake ikiichapa Namungo mabao 2-0, Uwanja wa Majaliwa, Ruangwa, Lindi, akipachika lingine, Septemba 11, mwaka huu, na kuipa ushindi wa mabao 2-1 timu yake dhidi ya KenGold, kabla ya juzi kufanya tena hivyo dhidi ya Dodoma Jiji na kuipa sare timu yake inayoshika nafasi ya tatu ikiwa na pointi saba.