MABAO 22 yamefungwa katika michezo 13 ya Ligi Kuu Tanzania Bara iliyochezwa mpaka sasa, 19 yakifungwa kwa njia ya kawaida na matatu kwa mikwaju ya penalti.
Kwa mujibu dawati la takwimu la michezo la gazeti hili, jumla ya mabao 18 yamefungwa ndani ya eneo la hatari na manne yamefungwa nje ya boksi.
Takwimu zinaonyesha mabao hayo yamegawanyika sehemu tatu, ambapo 14 yamefungwa kwa mguu wa kulia na wachezaji wa timu mbalimbali za ligi hiyo, matatu yamefungwa kwa mguu wa kushoto na matano yamefungwa kwa vichwa.
Mabao matatu ya mguu wa kushoto yamefungwa na Joshua Ibrahim wa KenGold huku Valentino Mashaka wa Simba akifunga, Agosti 17 wakati timu hiyo iliposhinda mabao 3-0 dhidi ya Tabora United na Heritier Makambo wa Tabora United, akifunga kwa penalti dhidi ya Namungo.
Takwimu pia zinaonyesha mabao 14 tu yamefungwa katika mechi za raundi ya kwanza msimu huu iliyokuwa na michezo minane, ikiwa ni machache kuliko yaliyofungwa raundi hiyo msimu uliopita ambapo jumla ya mabao 22 yalifungwa.
Msimu uliopita, Ligi Kuu Tanzania Bara ilianza kwa Geita Gold kushinda bao 1-0 dhidi ya Ihefu, JKT Tanzania kuichapa Namungo bao 1-0, Dodoma Jiji ikaichapa Coastal Union mabao 2-1, Mashujaa ikashinda mabao 2-1 dhidi ya Kagera Sugar, Azam ikaibabua Tabora United mabao 4-0, Simba ikashinda mabao 3-2 dhidi ya Mtibwa Sugar, Singida Fountain Gate na Prisons zikatoka suluhu na Yanga ikapata ushindi wa mabao 5-0 dhidi ya KMC.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED