Mdhamini mkuu wa Ligi Kuu ya NBC (NBC Premiere League), Benki ya NBC, imekabidhi kombe la ubingwa wa ligi hiyo kwa timu ya Yanga SC ya jijini Dar es Salaam huku ikiahidi kuendelea kufanya maboresho makubwa kwenye ligi hiyo katika kipindi cha miaka minne iliyosalia ya utekelezaji wa mkataba wa udhamini huo.
Hafla ya kukabidhi kombe la ubingwa huo ilifanyika mwishoni mwa wiki katika uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam ikiambatana na mchezo baina ya mabingwa hao dhidi ya Tabora United, mchezo ilioisha kwa Yanga SC kuibuka na ushindi wa magoli 3 -0.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya NBC, Dk. Elirehema Doriye aliiwakilisha benki hiyo kwenye tukio la makabidhiano hayo lililopambwa na uwepo wa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Kazi Maalum), Kapteni Mstaafu George Mkuchika pamoja na Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Wallace Karia.
Aidha, Mkurugenzi wa Fedha wa Benki ya NBC, Waziri Barnabas na Mkurugenzi wa Hazina na Masoko ya Fedha wa Benki ya NBC, Peter Nalitolela waliongoza zoezi la kukabidhi tuzo kwa mchezaji wa Yanga Aziz Ki aliyetangazwa mchezaji bora wa Ligi Kuu ya Soka ya Tanzania Bara kwa mwezi wa April sambamba na kocha timu hiyo Miguel Gamond alietangazwa kuwa kocha bora wa mwezi huo.
Akizungumza mara baada ya makabidhiano ya kombe hilo Mkuu wa Idara ya Masoko wa Benki ya NBC, David Raymond pamoja na kuipongeza timu ya Yanga SC kwa kuibuka kinara wa ligi hiyo iliyokuwa na ushindani mkubwa miongoni mwa timu shiriki, alisema benki hiyo ikiwa kama mdhamini mkuu wa ligi hiyo inaendelea kubuni mikakati mikubwa zaidi ya kuiboresha ligi hiyo ili kufikia malengo ya udhamini wake ambayo ni pamoja na kukuza vipaji na viwango vya soka nchini, kuchochea ajira kupitia michezo, kuongeza ushindani baina vilabu shiriki na kuongeza hamasa ya mchezo huo nchini.
“Kila mtu ni shuhuda wa mapinduzi makubwa ambayo tayari benki ya NBC tumeyafanya katika misimu hii mitatu ya udhamini wetu kwenye ligi Kuu ya NBC na mwaka mmoja wa udhamini wetu kwenye ligi ya Championship na ligi ya Vijana.’’
“Mbali na kuchochea ushindani kwenye ligi hizi kupitia udhamini ulioviweza vilabu shiriki kufanya usajili mzuri pia tumekuwa tukitoa huduma muhumu kwa timu hizi ikiwemo bima ya afya, mikopo ya usafiri kwa timu na zaidi tunahakikisha tunaandaa mazingira mazuri zaidi ya kuwakabidhi vikombe vyao vya ubingwa kwa kushikiriana na vilabu husika kuandaa matukio makubwa yenye kuongeza mvuto kwa mashabiki wao,’’ alisema Raymond akitolea mfano tukio la benki hiyo kuandaa helkopta maalum kwa ajili ya kuwasilisha kombe la ubingwa kwa klabu ya Yanga SC kwenye Uwanja huo.
Kwa mujibu Raymond udhamini wa benki hiyo kwenye ligi hizo umeambatana na matokeo chanya hata nje mchezo husika ambapo kupitia mnyororo wa sekta ya mchezo benki hiyo imeweza kuzalisha ajira za takribani 7,000 kupitia udhamini huo.
“Ni matokeo Chanya kama haya ya ongezeko la ajira na hamasa ya mchezo huu ndivyo vinavyotupa msukumo zaidi wa kuendelea kubuni mikakati mikubwa zaidi ili kupamba zaidi udhamini wetu. Tunaamini katika miaka hii minne iliyosalia katika udhamini wetu tutakuja na mambo mazuri na makubwa zaidi ikiwemo kubuni huduma bora za kibenki zinazolenga kuhudumia na kutatua changamoto za vilabu vinavyoshiriki ligi hizi,’’ alisema Raymond akitolea mfano huduma ya kadi za uanachama zinazotolewa na benki hiyo mahususi kwa mashabiki wa timu ya Yanga SC.
Katika kufanikisha hafla hiyo mwishoni mwa wiki benki ya NBC mbali na kushirikiana na timu ya Yanga SC kufanikisha baadhi ya matukio ikiwemo burudani kwenye mkesha maalum wa ubingwa, kuandaa helkopta maalum iliyoleta kikombe cha ubingwa kwenye uwanja huo, benki hiyo iliandaa hafla kubwa ya kukabidhi ubingwa huo kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa huku ikitoa huduma mbalimbali za kibenki kwa wahudhuriaji wa tukio hilo ikiwemo usajili wa uanachama kwa mashabiki wa timu ya Yanga waliofika kwenye uwanja huo.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED